22 C
Dar es Salaam
Sunday, May 28, 2023

Contact us: [email protected]

Jamii Forums, FUWAVITA kushirikiana kukuza uelewa juu ya changamoto za walemavu

Na Brighiter Masaki, Dar es Salaam

Baada ya Ripoti ya Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) ya 2020 kuonesha kuwa asilimia 49 ya Wanawake Viziwi Tanzania wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na ukandamizwaji wa haki zao.

Shirika la Asasi za Kiraia, lisilo la kiserikali la Jamii Forums na Furaha ya Wanawake Viziwi Tanzania (FUWAVITA) imeanzisha ushirikiano wa kikazi kwa lengo la kukuza uelewa wa wadau mbalimbali juu ya changamoto zinazowakabili viziwi na walemavu kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo, amesema kuwa Jamii Forums ni Asasi ya Kiraia inayojishughulisha na uraghabishi wa Haki za Kidijitali, Utawala Bora, Demokrasia na Uwajibikaji.

“FUWAVITA na Jamii Forums ambao ni waratibu wa mtandao mashuhuri wa kijamii wa JamiiForums zinazindua ushirikiano wa kikazi kwa lengo la kukuza uelewa wa wadau mbalimbali juu ya changamoto zinazowakabili viziwi na walemavu kwa ujumla.

“Zikiwemo ukatili, unyanyasaji na mifumo hafifu inayopelekea watu wenye ulemavu hasa wanawake viziwi kukwamishwa katika upataji wa huduma za kijamii kama elimu, afya, misaada ya kisheria, misaada ya kifedha katika mabenki” amesema Melo

Ameongeza kuwa Ripoti ya Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) ya 2020 ilionesha asilimia 49 ya Wanawake Viziwi Tanzania wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na ukandamizwaji wa haki zao.

Pia wanaishi katika mazingira magumu na tegemezi kutokana na ufinyu wa fursa za kielimu na ajira hali inayowapelekea kuishi katika mazingira duni na umasikini.

“Elimu ya Viziwi Tanzania iko nyuma ikilinganishwa na makundi mengine kutokana na miundombinu hafifu na upungufu wa wataalam wa lugha ya Alama.Takwimu zinaonesha ni viziwi wachache wanaofika ngazi ya juu katika elimu ya sekondari na Chuo Kikuu.”

“Asilimia kubwa ya wanawake viziwi hukwamishwa katika safari ya elimu kwa sababu ya uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kutokuwepo kwa usawa kwenye ushindani wa ngazi ya kitaifa.

“Lakini pia, bado mifumo ya ajira za Serikalini na Sekta Binafsi, siyo wezeshi kwa hata viziwi wachache waliosoma, kuhitimu na kupata maarifa ya kazi.

“Changamoto zilizopo ni pamoja na mifumo hafifu na ukosefu wa wataalamu wa lugha za alama katika maeneo ya kazi na ufinyu wa rasilimali za kuwalipa wataalamu wa lugha za alama,”amesema Melo

Kwa upande wake Mkurugenzi wa FUWAVITA, Aneth Gerana, ambaye ni kiziwi na muajiriwa pia amesema kuwa shirika limesajiliwa mwaka 2008 kwa Lengo la kuongeza maarifa na ujuzi kwa Wanawake Viziwi Tanzania ili waweze kujikwamua kutoka katika umasikini.

“Changamoto anazokumbana nazo kazini huminya uwezo wake wa kufanya kazi kwa weledi.

Pia Changamoto hizo za viziwi katika ajira zimepelekea wengi kukata tamaa ya kuajiriwa hivyo kupelekea kuwa tegemezi kwa familia na wenza wao.

“Serikali kupitia Sera ya nchi ya watu walemavu ya Julai 2010 (kifungu cha 2.2) imewajumuisha viziwi katika kundi la vipaumbele wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.

“Bado sera hizi zinakosa usimamizi madhubuti unaowajibisha wadau mbalimbali nchini wanapokiuka Haki za walemavu na hasa Wanawake Viziwi.” amesema Aneth.

Aidha amesema kuwa lli kuweza kutatua changamoto hizi, zinahitajika jitihada za wadau mbalimbali katika kuimarisha, mifumo kuwa wezeshi inayokidhi mahitaji ya viziwi katika nyanja za elimu, ajira, huduma za kisheria, kiafya, kiuchumi.

“FUWAVITA inatumia fursa hii kuwasihi wadau mbalimbali kuunga juhudi malengo yao lakini pia kukaribisha uwekezaji katika tafiti zitakazobaini mazingira ya viziwi walioko maeneo mbalimbali nchini.”

“Uwepo wa taarifa zilizofanyiwa tafiti utazisaidia Serikali, mashirika binafsi na Asasi nyingine za Kiraia kuweza kufikisha huduma kwa kundi la Wanawake Viziwi na Walemavu kwa ujumla,”ameongeza Aneth

Pia, tunazisihi mamlaka zinazosimamia sheria na sera za makundi ya walemavu kuongeza ufuatiliaji na uwajibishaji ili tupunguze matukio ya unyanyasaji na ukandamizaji wa Haki za Walemavu na hasa wanawake viziwi.

“Tunatarajia kupitia mashirikiano haya na Jamii Forums, vilio vya wanawake viziwi vitaweza kuzifikia mamlaka na watanzania wengi ili kuwe na jamii inayozitambua changamoto za walemavu na kuwa katika sehemu ya kuzitafutia suluhu,” amesema Aneth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,167FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles