23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jamhuri yabanwa kesi ya kina Mbowe

Kulwa Mzee, Dar es salaam

WAKILI wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Profesa Abdallah Safari, amewabana mawakili wa Serikali akidai kwamba wanasahau kama waliwahi kuacha mahakama wakaenda Ikulu, lakini sasa wanapinga washtakiwa kwenda nje ya nchi kikazi.

Profesa Safari alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba wakati akiwasilisha maombi ya kuahirisha kesi hiyo.

“Mheshimiwa Hakimu, mawakili wa Serikali wanasahau haraka sana, waliwahi kukimbia mahakama wakaenda Ikulu kesi ikaahirishwa, leo wanapinga Esther Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini) kwenda Bunge la Ulaya,” alidai Profesa Safari.

Akiwasilisha maombi ya kuahirisha kesi hiyo, alidai mshtakiwa Dk. Vicent Mashinji (Katibu Mkuu Chadema) yuko kwenye kesi Songea, Matiko kaalikwa pamoja na wabunge wenzake watano kwenda Kigali nchini Rwanda kushiriki mkutano Septemba 25-28.

Alidai mwaliko mwingine ni wa kwenda Bunge la Ulaya, atakuwa huko kuanzia Oktoba 13 hadi 18, hivyo aliomba kesi ije kwa utetezi Oktoba 7 na 8.

Pia aliomba muda huo wa utetezi ili wajiandae kwani wana mashahidi wengi zaidi ya nane wa upande wa mashtaka.

Akijibu Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai washtakiwa wanatakiwa kufuata kalenda ya mahakama, suala la kuomba muda wa kujipanga kuanza utetezi ni hoja mpya.

Alidai katika barua ya Matiko, safari ya Kigali inahusu wabunge sita akiwemo yeye mwenyewe, hivyo haoni sababu kwanini aende safari hiyo aache kesi.

Wakili Nchimbi alidai kwa safari zote mbili haoni sababu ya Matiko kwenda na kuacha kesi.

Alidai mshtakiwa anaweza kushindwa kufika mahakamani kwa sababu ya ugonjwa ama msiba.

Akijibu kwa mara nyingine, Profesa Safari alidai hawajavunja amri yoyote ya mahakama, walichokifanya wao ni kuomba ahirisho kwa sababu wateja wao wanasafiri na pia wajiandae kwa utetezi.

“Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu wa uchungu, kuhoji Matiko kusafiri na kuona kwamba asiende sababu kuna wabunge wengine, huo wivu.

“Washtakiwa hawa hawawezi kudanganya, hawana sababu ya kudanganya. Matiko anaenda kwenye Bunge la Ulaya unahoji, safari za nje nani anaweza kwenda kienyeji enyeji.

“Tunakuja kwenye suala la kitaifa, yule Dk. Mashinji sawa na Waziri Mkuu, mawakili wa Serikali wanasahau kama waliwahi kukimbia mahakama wakaenda Ikulu kesi ikaahirishwa, lakini leo wanapinga Matiko kwenda Bunge la Ulaya,” alidai Profesa Safari.

Hakimu Simba baada kusikiliza hoja zote, aliahirisha kesi hadi leo kwa uamuzi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles