‘Badilini mtazamo kuhusu ugonjwa wa Lupus’

0
639

Aveline Kitomary -Dar es salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Lupus Awareness and Support Foundation (LASF), Hajrrath Mohamed, ameitaka jamii ibadilishe mtazamo hasi kuhusu ugonjwa wa Lupus ambao unahusishwa na Ukimwi huku akikemea matukio ya unyanyapaa kwa wanaougua.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam juzi, Hajrrath alisema hali ya ugonjwa wa Lupus kuhusishwa na ushirikina pia inawapa wakati mgumu wagonjwa hao.

“Lupus ni ugonjwa wa kurithi, unatokea pale kinga za mwili zinapoacha kazi ya kulinda na badala yake kushambulia mwili.

“Lakini watu wengi hawana uelewa kuhusu ugonjwa huo, hivyo wagonjwa wamekuwa wakipata shida kutokana na jamii inayowazunguka kuwa na mitazamo hasi.

“Wapo wanaohusisha ugonjwa huo na Ukimwi na wengine wanaamini ugonjwa huo ni kulogwa kitu ambacho si kweli, hali hiyo imefanya wagonjwa wasiweze kujiamini hata katika utendaji wa kazi zao, pia tunanyanyapaliwa sehemu za shule hata za kazi,” alisema Hajrrath.

Alieleza kuwa changamoto hizo zinazojitokeza zinawafanya wagonjwa wengi wa Lupus kushindwa kujitokeza hadharani na kubakia kujificha.

“Wakati naanza kupata ugonjwa wa Lupus nilikuwa naogopa kuonana na watu, hata kutoka nje ya nyumba naogopa kwa sababu watu wananiangalia sana, wengine wananisema vibaya, hivyo nilikuwa nakaa tu chumbani, hata wageni wakija sitoki chumbani.

“Nawatia moyo wagonjwa wa Lupus wasijifiche, wajitokeze ili chama kiweze kuwajua na kuungana pamoja kama chama, hivyo kila mmoja ajikubali kwa jinsi alivyo,” alishauri.

Hajrrath ambaye ni mwanzilishi wa chama hicho, alisema malengo hasa ni kujua idadi ya wagonjwa, kukabiliana na changamoto za wagonjwa wa Lupus na pia kutoa elimu kwa jamii.

“Mpaka sasa tokea mwaka jana kwa Mkoa wa Dar es Salaam wagonjwa waliojitokeza ni 12, lakini wengine bado hawajiamini. Tukiwa wengi pia na sisi Serikali itatuangalia, tutapata dawa,” alisema.

Hajrrath aliiomba Serikali kuuangalia ugonjwa huo kwa jicho la tatu kwani bado wagonjwa hupata changamoto nyingi ikiwamo za dawa na madaktari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here