26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Jaji Mutungi aitisha kikao cha baraza la vyama vya siasa

Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

OFISI ya Msajili wa Vyama imeitisha  kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa  kinachotarajia kufanyika Januari 10 na 11, mwakani mjini Unguja, Zanzibar.

Mkutano huo uliopaswa kufanyika Desemba 21 na 22, mwaka huu lakini uliahirishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ambaye ndiye Mkuu wa Sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa kwa ajili ya kupisha uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 19, mwakani umeitishwa tena baada ya kuwapo kwa mashauriano baina yake na Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Elimu kwa Umma wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Mnanka, ilieleza kuwa viongozi hao wameona ni vyema kikao hicho kikafanyika kwa kuwa wagombea karibu wote wamepita bila kupingwa.

“Lengo la kuitisha mkutano huu mapema  ni kuwezesha Baraza kuandaa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018 na kuyawasilisha katika kamati husika ya Bunge inayoanza shughuli zake Januari 14, 2019,” ilisema taarifa hiyo.

Pia ilisema mkutano huo wa kawaida wa baraza hilo unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Bima Zanzibar uliopo eneo la Madema, Barabara ya Michenzani, Mjini Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Kamati ya Uongozi kitakachofanyika Januari 8, mwakani ili kufanya maandalizi ya kikao cha baraza hilo.

Pia ilisema kikao cha baraza hilo nacho kitatanguliwa na semina kwa wajumbe wa kuhusu utaratibu wa kutunga sheria, itakayotolewa na ofisi ya Bunge.

Ilisema semina itafanyika Januari 9, mwakani katika ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge, Zanzibar zilizopo eneo la Tunguu.

Pia ilisema baadhi ya ajenda za kikao zitakazojadiliwa ni pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu baraza hilo, kujadili muswada wa Sheria mpya ya Vyama vya Siasa na uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa baraza hilo.

Taarifa ya msajili kuitisha mkutano huo imekuja wakati wiki iliyopita viongozi wa vyama 10 vya upinzani walitoa tamko jijini Dar es Salaam la kutoridhishwa na uamuzi wa kuahirisha kikao hicho.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles