29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

JAJI AINYOSHEA KIDOLE DOLA UVUNJAJI HAKI ZA BINADAMU 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM



JAJI Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Eusebia Munuo, amesema mihimili ya dola hususani Serikali, Bunge na Mahakama imekuwa ikichangia kuvunja haki za binadamu.


Amesema haki za binadamu zinalindwa kwa kusaini na kuridhia mikataba hivyo ni vizuri watu wafahamu uwepo wa haki hizo kitaifa ndani ya Katiba, kisheria na utekelezaji wake kwa misingi ya kuziheshimu.


Jaji Munuo alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2016 iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).


“Haki za binadamu zinaheshimiwa lakini pia huvunjwa na mihimili ya dola hususani Serikali, Bunge na Mahakama.
“Tunapozindua taarifa hii tujielekeze kuangalia matuko yanayohusu haki za binadamu nchini kwa kutazama wajibu wa mwananchi wa kawaida pamoja na dola katika kuhakikisha hali ya haki za binadamu inaboreshwa nchini,” alisema Jaji Munuo.


Jaji Munuo pia alisema nchini Tanzania kuna sheria ambazo haziendani na ulinzi wa haki za binadamu ambazo zinahitaji kuondolewa au kurekebishwa. 


 “Ripoti ya Jaji Francis Nyalali ilibaini zaidi ya sheria 40 kandamizi na kazi ya kuziondoa bado haijafanikiwa vya kutosha.
 “Changamoto nyingine ni kuendelea kutungwa kwa sheria zenye vifungu kandamizi kwa ulinzi wa haki za binadamu kama vile Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,” alisema.


Jaji huyo pia alisema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi kutokana na kuwapo kwa matukio ya ukatili na mauaji ambayo yanaonekana kuota mizizi nchini.


Kwa mujibu wa jaji huyo, haki ya kuishi ni haki ya kikatiba kwani Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaainisha haki hiyo.
“Watu kujichukulia sheria mkononi imekuwa mtindo wa maisha, mauaji yatokanayo na imani za kishirikina, mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi, mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe na mengine yanayofanana na hayo ambayo yanatia doa nchi yetu,” alisema.


Alisema elimu ya utii wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na dhana ya uwajibikaji katika kudai haki ni mambo ya msingi kuzingatiwa ili kupunguza matukio hayo yanayotishia amani na mshikamano wa nchi.


Awali mtafiti kutoka LHRC, Paul Mikongoti, alisema ripoti hiyo ilijikita kuangalia masuala mbalimbali kama vile haki za kiraia, haki za kisiasa, haki za makundi maalumu na upatikanaji wa huduma za kijamii.


Kwa mujibu wa mtafiti huyo, kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hasa kwa wanawake na watoto kutokana na kuendelea kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Alisema kati ya Januari hadi Juni mwaka jana, matukio ya ukatili wa kijumla yalikuwa 7,475 ambayo yalihusisha vipigo, kunyimwa stahiki zao, ubakaji, kulazimishwa kufanya mapenzi, kuchomwa moto, kuvamiwa na silaha, kukabwa na mengine mengi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles