Jafo awashukia maofisa utumishi

0
916
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleman Jafo

YOHANA PAUL – MWANZA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleman Jafo amesema maofisa utumishi wa halmashauri nyingi, wamekuwa kikwazo kwa walimu kupandishwa vyeo na mishahara.

Aliyasema hayo jijini Mwanza juzi,wakati wa hafla ya utoaji tuzo na zawadi kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri Wilaya ya Nyamagana iliyoandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya hiyo.

Alisema walimu wengi,wanafanya kazi kubwa shuleni, lakini wanapoamua kujiendeleza kielimu ili wapande madaraja, baadhi ya maofisa utumishi wamekuwa na tabia za makusudi kutobadili taarifa za walimu hao na kusababisha Serikali kutopata taarifa  wanaostahili kupandishwa madaraja.

“Suala la kupanda madaraja walimu waliojiendeleza, limekuwa likilalamikiwa sana,mimi na ofisi yangu tunaendelea kulifanyia kazi kila siku kuhakikisha wote wenye sifa wanapandishwa madaraja.

“Mbali na juhudi inazofanya wizara yangu kuondoa malalamiko ya upandishwaji madaraja, kumekuwa na tatizo la ucheleweshwaji wa taarifa za walimu kutoka kwa maofisa utumishi, changamoto inayosababisha kutopata stahiki zao kulingana na madaraja yao.

“Natoa agizo kwa maofisa utumishi wa halmashauri zote kuhakisha wanatuma taarifa za walimu wote waliopanda madaraja kulingana na elimu zao wizarani ili watambuliwe Serikali ndani ya wakati na kuwatengea bajeti,” alisema Jafo.

“Umefikia wakati sasa watumishi wote wa Serikali walioaminiwa na rais wetu, watambue thamani ya mwalimu kulingana na kazi kubwa wanayoifanya na kwani kila mmoja wetu amepitia mikononi mwa mwalimu hivyo tuache tabia ya kidhalilisha waalimu kwa sababu ya vyeo vyetu,”

Akisoma risala kwa niaba ya walimu,  Ofisa Elimu Wilaya ya Nyamagana, Ephrahime Maginge alisema wanaunga mkono juhudi za Serikali kuboresha maendeleo ya elimu,ingawa bado kuna changamoto za ucheleweshaji wa madai yao.

Alisema wilaya hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa, inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha shule zote za wilaya hiyo zinafanya vizuri kanda ya ziwa na kitaifa kwa ujumla.

“Walimu wilaya ya Nyamagana wanamuponge rais wetu kwa juhudi anazofanya kufikia maendeleo ya elimu kitaifa, ikiwamo uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kuongeza vyumba vya madarasa, madawati na vifaa vya kujifunzia.

“Pia sera ya elimu msingi bure, imesaidia kuamusha ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii bila hofu ya kutokuendelea na masomo kutokana na gharama za ada,hata wanapofaulu hawana tena wasiwasi wa kulipishwa michango na ada shule za sekondari.

“Kilio kikubwa cha walimu,ni kucheleweshwa kupandishwa madaraja ya mishahara na vyeo pale wanapokuwa wamejiendeleza kielimu kutoka ngazi za chini kama kutoka astashahada hadi stashahada ama shahada,”alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alikipongeza chama hicho kwa kuandaa hafla hiyo, kwani itasaidia kuamusha molari ya ushindani wa kielimu kwa wanafunzi, walimu na shule hali ambayo itapandisha maendeleo ya elimu wilaya na Mkoa wa Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here