25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ilinde biashara yako kuepuka kupoteza kila kitu

Na Makirita Amani

KUNA changamoto nyingi katika kuendesha na kukuza biashara. Changamoto nyingine zinaweza kuzuilika au kuzuiwa kuleta madhara ya moja kwa moja.

Leo tutajifunza umuhimu na jinsi ya kulinda biashara yako ili kuepuka kupoteza kila kitu hasa pale unapokutana na ajali. Pamoja na changamoto za kawaida za biashara, bado pia kuna ajali zinazoweza kutokea. Mara nyingi ajali hizi huwa zinakuja kwa wakati ambapo hukujiandaa kukabiliana nazo au kuondoa madhara.

 

Kwanini ni muhimu kulinda biashara yako?

 Kama tulivyoona hapo juu, biashara zina changamoto nyingi na licha ya changamoto hizo kuna ajali pia. Unapolinda biashara yako na mara nyingi ni juu ya ajali au dharura unajiweka mahali salama hasa pale ambapo ajali imetokea na wewe huna maandalizi. Kulinda biashara yako kutakupa uhakika wa kuendelea nayo hata kama umepata changamoto kubwa. Kwa mfano; kama eneo lako la biashara limeungua moto, na wewe ulikuwa umelinda eneo hilo dhidi ya ajali za moto, utanufaika hata baada ya moto kuteketeza eneo lako.

Pia kulinda biashara yako kunakufanya uondokane na hofu zisizo muhimu na hivyo kupata muda mzuri wa kuzingatia yale ambayo ni muhimu. Mara nyingi unapokuwa na wasiwasi juu ya jambo usilotarajia kutokea, unashindwa kuweka juhudi katika maeneo ambayo ni muhimu kwa biashara yako. Wasiwasi utakuzuia wewe kujibidiisha.

Kuilinda biashara yako kutakupa wewe uhuru wa kuchukua fursa ambazo kwa wengine zinaweza kuonekana ni hatari. Kunakupa kujiamini na unaweza kufanya mengi ukilinganisha na wale ambao hawajazilinda biashara zao. Hata katika ukuzaji wa biashara kama una uhakika umeilinda, itakuwa rahisi kuikuza kuliko ambaye hajailinda. Wakati ambaye hajailinda atakuwa anaogopa akikuza sana atapata hasara, wewe utakuwa na uhakika kwamba kuikuza zaidi biashara ni kitu muhimu kwako.

 

Unailindaje biashara yako?

Njia ya uhakika ya kulinda biashara yako ni kukata bima, hiki ni kitu muhimu mno kwa sababu biashara inajumuisha vitu vingi. Kila kitu kinachohusika katika biashara kina bima yake na hivyo unahitaji kukaa chini na wataalamu wa bima ili wakushauri ni maeneo gani unaweza kuyalinda.

Kwa kuanzia maeneo muhimu ya kulinda biashara yako ni pamoja na miundombinu muhimu ya biashara kama majengo, vifaa vya uzalishaji, vyombo vya usafiri na hata wafanyakazi wa biashara yako. Kila kitu hapa kinahitaji kulindwa na bima, majengo yanahitaji bima ili kama ajali yoyote itatokea basi uweze kufidiwa. Vyombo vya usafiri vinahitaji bima ili kama vitapata shida yoyote kama ajali au moto uweze kufidiwa. Hata wafanyakazi wako wanahitaji bima ili kama wataugua au kupata shida kutokana na kazi wanayofanya basi waweze kufidiwa.

Kinachowakwamisha wengi kulinda biashara zao ni kuona kama ni gharama za ziada zisizo za msingi. Lakini ukweli ni kwamba bima si gharama za ziada bali ni za msingi. Wakati unatoa mchango wa bima utakuuma hasa kama hupati ajali. Lakini siku utakapopata ajali utajikuta unalipwa fedha nyingi kuliko hata michango uliyotoa.

Hivyo, ondokana na dhana kwamba kuilinda biashara yako ni gharama za ziada. Kama kweli unaijali na unataka kuona inaendelea kuwa salama kwa miaka mingi ijayo, basi unahitaji kuilinda biashara yako kwa kuikatia bima.

Mwandishi wa makala hii ni mjasiriamali na muendeshaji wa mtandao wa AMKA MTANZANIA (www.amkamtanzania.com).  Mawasiliano 0717396253 au barua pepe [email protected]

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles