30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka miwili ya kitendawili ndege ya Malaysia

MTZ UCHUMI HII SAFI.inddMACHI 8 ilitimia miaka miwili tangu kutoweka kitatanishi kwa ndege namba MH 370 ya Shirika la Malaysia muda mfupi baada ya kuruka kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing, China.

Hiyo ilikuwa usiku wa Jumamosi ya Machi  8, 2014 ndege hiyo aina ya Boeing 777 ilipotoweka ikiwa na abiria na wafanyakazi 239 wengi wao wakiwa raia wa China na Malaysia.

Kipande kimoja cha bawa kimepatikana, sambamba na pengine na sehemu za mkia, lakini bado kilichoisibu ndege hiyo kinabakia kuwa kitendawili katika sekta ya anga duniani.

Licha ya mengi kusemwa, wachunguzi wanaotaka kujua kile kilichoisibu ndege hiyo nao wamekiri sababu ya kutoweka kwake bado ni kitendawili.

Timu ya kimataifa ya wataalamu wa safari za anga iliyoundwa kuchunguza kisa cha kutoweka kwake imetoa repoti ya kila mwaka yenye kuelezea hatua zilizofikiwa lakini taarifa yao hiyo fupi haina maelezo ya kina juu ya kile kilichoisibu.

Mkuu wa timu hiyo ya uchunguzi, Kok Soo Choon alisoma taarifa hiyo kwenye televisheni mjini Kuala Lumpur Jumanne iliyopita wakati wa kuadhimisha miaka miwili tangu kutoweka kwake, hali iliyozidisha simanzi kwa ndugu waliopoteza wapendwa wao wengine wakitishia kwenda mahakamani.

Choon anasema; “Kwa wakati huu timu ya uchunguzi inaendelea kukamilisha uchanganuzi wake, kile ilichogundua, hitimisho, mapendekezo ya usalama kwa maeneo manane husika yanayohusishwa na kutoweka kwa ndege hiyo kwa kuzingatia taarifa zinazostahiki.”

Lakini pia Malaysia na Ausralia zimesema bado zinaendelea kuwa na matumaini kwamba juhudi zao za kuitafuta katika eneo la bahari ya Hindi inakoaminika imeangukia zitasababisha kujulikana kwa kitu fulani katika data za kurekodi safari ya ndege hiyo na hatimaye kubainisha kile kilichosababisha kutoweka kwake kipindi kile.

Wabunge wa Malaysia Jumanne iliyopita walikaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka abiria na wafanyakazi wanaohofiwa kupoteza maisha katika kisa hicho.

Waziri Mkuu wa Malaysia, Naijib Razak anasema katika taarifa yake uchunguzi wa hivi sasa wa kuitafuta ndege hiyo unatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu na kwamba wanaendelea kuwa na matumaini ndege hiyo itapatikana.

Familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao ziliandamana mjini Beijing, China Jumanne iliyopita kushinikiza kutatuliwa kwa kitendawili cha kuanguka kwa ndege hiyo.

Dai Shukin, ambaye dada yake na familia yake walikuwamo katika ndege hiyo iliyotoweka anasema; “hatujuwi iwapo wako hai au wamekufa. Hatujui wako katika hali gani mbaya au nzuri. Tuna wasi wasi mkubwa, tuna msongo wa kisaikolojia aina fulani ya chuki na dhiki.”

Kwa uwapo wa satelaiti zinazofuatilia kila kinachoendelea angani na teknolojia ya juu kabisa na kisasa ya unasaji vitu, imekuwaje ndege tena kubwa namna hiyo ipotee kirahisi?

Na kwanini haijapatikana, hata baada ya kipande cha bawa kugundulika katika kisiwa kilichopo Bahari ya Hindi?

Hebu tuangalie kilichoikumba MH370 kwa ufupi saa chache baada ya kuruka na baadhi ya nadharia zenye uwezekano wa kilichoisibu.

Ndege hiyo hiyo iliondoka Kuala Lumpur saa 6:41 usiku ikitarajia kuwasili Beijing, karibu saa sita baadaye yaani 12:30 asubuhi za majira ya huko.

Lakini ilipofika saa 7:07 usiku, ndege hiyo ilituma ujumbe wake wa mwisho kupitia Mfumo wa Kuripoti mawasiliano ya Ndege (ACARS), mfumo ambao husambaza moja kwa moja taarifa za kila ndege ikiwamo hali mbaya ya hewa, matumizi ya mafuta na tatizo lolote la kiufundi la ndege.

Mamlaka za Malaysia ziliripoti kwamba kuwa audio ya rubani, Kaptani Zaharie Ahmad Shah, au msaidizi wake mkuu, Fariq Abdul Hamid, ilisikika ikisema, ‘Sawa sawa, usiku mwema’.

Serikali baadaye ikabadili maelezo kwamba sauti ya mwisho kusikika kwa waongozaji wenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur saa 7:19 usiku ya Machi 8 ilikuwa ‘Usiku mwema Malayasia tatu-saba-sifuri.”

Baada ya dakika 40 za safari, saa 7:21 usiku, mfumo wa kusambaza sauti wa ndege ukatoweka na mawasiliano na ardhini kupotea.

Saa 8:14, ikiwa ni saa moja na nusu tangu ndege iondoke Kuala Lumpur, rada ya jeshi la Malaysia ilitambua ndege hiyo ikiwa sehemu za kaskazini za Mkondo wa Malacca.

ACARS iliendelea kusambaza mapigo kwenda satelaiti kwa saa nne hadi tano, kwa mujibu wa maofisa wa Marekani.

Ishara ya mwisho kuchukuliwa na satelaiti ilikuwa saa 2:11 asubuhi ya siku iliyofuata, ikiashiria kuwa MH370 ilibadili mkondo wake kutoka njia yake ya kaskazini kuelekea Beijing na ilikuwa mahali kwingine katika kikonyo kuanzia Kazakhstan hadi Bahari ya Hindi mashariki mwa  Australia.

Wakati uchunguzi ukiendelea na ambao ulielekezwa katika sehemu tofauti tofauti mara kadhaa, ubawa wa ndege hiyo ukapatikana Julai mwaka jana, huku vipande vyingine viwili vipya vya mabaki ya ndege vikipatikana visiwa vya Reunion na Msumbiji na kuthibitisha kuanguka kwake.

Licha ya ushahidi unaoaminika kwamba ilianguka, kitendawili kilichobakia na ambacho ni muhimu kwa ajili ya kujifunza hali ya baadaye ya kiusalama ni nini kilichoisibu ndege hiyo?

Kutoweka kitatanishi kwa  MH370 kuliibua nadharia mbalimbali kutoka kwa wataalamu na wadau wa sekta. Zifuatazo ni baadhi ya nadharia hizo.

Abiria na wafanyakazi kukosa hewa

Juni 26, 2014, Bodi ya Uchukuzi ya Usalama ya Australia (ATBS) ilitoa ripoti yenye kurasa  55 ambayo ilihitimisha kwamba abiria na wafanyakazi walipoteza fahamu kwa kukosa hewa, na hivyo ndege kukosa mwongozaji na kuishia kuanguka baharini.

Ripoti ilidai kwamba wachunguzi walifikia hitimisho hilo kwa kulinganisha na hali inavyokuwa katika ndege kwa kutumia uzoefu wa majanga ya nyuma, lakini haikutoa ushahidi wa kilichotokea ndani ya ndege hiyo.

Wachunguzi waligusia kwamba, miongoni mwa mambo mengine ukosefu wa mawasiliano na njia isiyofaa ya ndege kumechangia.

“Kutokana na uchambuzi huu, hatua za mwisho za wafanyakazi kutoweza kuitikia kunaonekana kuendana na ushahidi unaopatikana kwamba kipindi cha mwisho cha MH370 kilikuwa wakati ikielekea katika njia ya kusini,” ripoti ya ATSB ilisema.

 

Utekaji nyara

Wakati ndege MH370 ilipotoweka, baadhi ya wachambuzi walidhani kuwa huenda ilitekwa nyara na wana mlengo mkali wenye ajenda ya kisiasa.

Baada ya data za satelaiti kuonesha kwamba MH370 ilibadili mkondo mkali wa njia yake kuelekea magharibi, baadhi walichukulia hilo kama uthibitisho wa wa kutekwa angani.

Hata hivyo, hakuna kundi lolote lenye itikadi kali lililojitokeza kudai kuhusika na kitendo hicho.

Hujuma

Ndege  MH370 ilionekana wazi kubadili makusudi mwelekeo wa njia yake na hivyo kuzua pia nadharia ya uwapo wa hujuma.

Machi 14, 2014, ofisa mwandamizi wa polisi Malaysia alisema, “tunachoweza kusema tunaangalia uwezekano wa hujuma, pamoja na utekaji nyara.”

Matatizo ya kiufundi

Chris Goodfellow, rubani wa Canada mwenye uzoefu wa miaka 20 kwa kazi hiyo alikuja na nadharia, ambayo ilichapishwa tena katika jarida la Wired.

Goodfellow aliandika kuwa kulikuwa na uwezekano wa kutokea tatizo la kiufundi hasa moto ambao ulimlazimisha rubani kugeuza njia mara moja, kuelekea kiwanja cha ndege kilicho karibu kwa ajili ya kutua.

Kwa kutegemea data za satelaiti kuhusu kule MH370 ilikokuwa ikielelea baada ya kuachana na njia yake ya Beijing, Goodfellow anaamini rubani alitegemea kuelekea uwanja wa ndege ulio mita 4,000 kule Pulau Langkawi, kisiwa kilichopo kaskazini mwa Malaysia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles