23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO, TUMIA TEKNOLOJIA KUPAMBANA NA UHALIFU

KUTOKANA na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea  kupoteza maisha ya watu katika maeneo ya Kibiti na  Rufiji  mkoani Pwani, pamekuwapo  mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi, kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na hali hii.

Wakati  mitazamo tofauti  ikiibuka  kuhusu kukabiliana na uhalifu, wananchi walio wengi wakiwamo wanasiasa wamekuwa hawatoi ushauri na mwelekeo utakaowasaidia polisi wetu  kuibuka kidedea.

Pamoja na  Jeshi la Polisi kushauriwa kushirikiana na raia, lakini limekuwa likilaumiwa sana kuliko uhalisia kwamba  limeshindwa kabisa,  huku baadhi ya wananchi  wakiendelea kuwa na mawazo mgando kuwa Jeshi  la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndicho chombo pekee kinachoweza kutoa suluhisho na kusahau  kwamba hata JWTZ  ni binadamu wanaotumia damu.

Katika makala yangu yaliyopita nilitoa ushauri kwa Mkuu mpya wa  Jeshi la Polisi (IGP) Sirro kuunda kikosi imara cha upelelezi chenye uadilifu  na uwezo mkubwa katika kubaini vitendo vya uhalifu kabla havijaleta madhara  katika jamii.

Hata hivyo kuna haja  Jeshi la Polisi   kutumia teknolojia mpya kulingana na mabadiliko ya dunia yanayosababisha   uhalifu kutekelezwa kimkakati

Polisi wetu wanaweza kujifunza kutoka Idara ya Polisi katika Jiji la  Chicago nchini Marekani  ambalo limeamua kutumia mikakati ya teknolojia kubwa na zana za kisasa  kutokana na  kuongezeka vitendo vya mauaji na magenge yanayofanya ghasia.

Afisa Mnadhimu wa Polisi jijini Chicago, Eddie Johnson wakati akizungumza na waandishi wa habari Februari Mosi mwaka huu, alisema kuwa, Idara ya Polisi kwa sasa inatumia mikakati ya teknolojia ya kisasa  ili kukabiliana na uhalifu.

“Tumebadilisha utamaduni wa kupambana na uhalifu katika idara ya Polisi ya Chicago,” Johnson alisema, huku  akiongeza kuwa anaamini teknolojia itasababisha kukamata wahalifu wa ghasia na hivyo kupunguza idadi ya mauaji na mashambulizi.

Afisa huyo alionesha namna maafisa wa polisi watakavyotumia haraka iwezekanavyo programu za kompyuta ili kusoma na kutambua ni wapi pamefyatuliwa risasi  huku  wananchi wakionyeshwa namna mfumo wa kompyuta utakavyoweza kutambua mara moja ni wapi kuna ghasia.

Kiongozi huyo aliendelea kueleza namna idara ya polisi imepanua teknolojia ijulikanayo ‘‘ShoSpotter’’ ambayo inatumika katika miji mikubwa ili kusaidia kutambua uhalifu ambapo zaidi ya vitambuzi (sensors) 100  vimewekwa  huku vikiwa vimeunganishwa kwenye simu za viganjani (smartphones) ambazo huunganishwa kwenye  kompyuta na kutambua ndani ya sekunde chache mwelekeo wa  bunduki ilikotumika.

Wakati  huohuo polisi wameongeza idadi ya kamera zinazoongozwa kwa ‘remote’ pamoja na  teknolojia ya kutambua bunduki katika miji hiyo huku vifaa hivyo vikiwa vimewekwa kwenye mfumo ujulikanao ‘Strategic Decision Suport Center’ ambapo kila kituo cha polisi kimeunganishwa.

Pia kila kituo kina mfumo wa kompyuta ujulikanao Hunch Lab ambao hujazwa taarifa za ukamataji na data nyingine zinazoweza kubashiri maeneo ambayo uhalifu unaweza kujitokeza.

Jiji la  Chicago limekuwa kitovu cha ghasia zinazohusisha matumizi mabaya ya bunduki ambapo inakadiriwa mwaka  jana pekee takribani watu wapatao 762 waliuawa ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya miji miwili ya New York na Los Angeles.

Mafanikio ya polisi jijini Chicago katika matumizi ya teknolojia ni matokeo ya Serikali ya Marekani  kuwekeza vyakutosha katika chombo hicho, ambapo hata Serikali ya Tanzania haina budi kufanya hivyo haraka  ili kukabiliana na uhalifu.

Hata hivyo hakuna  mazingira yoyote yawe ya kisiasa kama inavyohisiwa huko Kibiti na Rufiji, au  mazingira ya kiuchumi na kijamii yanayoweza kupindua zana ya uhalifu kuwa halali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles