IDADI YA MAPACHA WANAOKUFA AFRIKA INATISHA

0
1020

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA,

WAKATI katika jamii nyingi ikiwa ni fahari kuzaa watoto mapacha, kitu ambacho wengi hawana habari nacho ni kwamba uzao wa aina hiyo ni ‘hatarishi’ iwapo hautabainika mapema hasa katika mataifa masikini.

Kwamba watoto mapacha wamekuwa wakipoteza maisha kwa wingi kulinganisha na wale wanaozaliwa wakiwa mmoja mmoja kusini mwa jangwa la Sahara Afrika kutokana na sababu kadhaa tutakazoziona baadaye katika makala haya.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na jarida maarufu la sayansi la Lancet, mtoto mmoja kati ya watano wanaozaliwa mapacha katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika hufa kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano, kulingana na utafiri mpya uliochapishwa katika jarida maarufu la Sayansi la Lancet.

Utafiti huo ni wa kwanza wa kuchunguza viwango vya vifo miongoni mwa watoto mapacha Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.

Ripoti hiyo inasema kuwa mafanikio katika kunusuru maisha ya mapacha yamekuwa nyuma ya yale ya kunusuru maisha ya watoto wengine.

Viwango vya vifo miongoni mwa watoto wanaozaliwa wakiwa mmoja mmoja wenye umri wa chini ya miaka mitano ilipungua kwa nusu ilihali kwa mapacha viwango vyao vilipungua kwa theluthi moja tu.

“Idadi ya mapacha wanaofariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano inakadiriwa kuwa 315,000 kwa mwaka.”

Utafiti huo ulitumia takwimu za watoto milioni 1.69 wakiwamo mapacha 56,597 waliozaliwa katika nchi 30 za kusini mwa Sahara Afrika kati ya mwaka 1995 na 2014.

Kujifungua watoto mapacha ni hatari zaidi ya kujifungua mtoto mmoja – bila kujali ni nchi gani mama aliyojifungulia kati ya hizo 30, utafiti umeonesha.

Hatari huongezeka kwa wanawake wanaojifungua mapema, kujifungua watoto wenye uzito mdogo na wakina mama kupoteza damu nyingi.

Lakini utafiti unasema kuwa hatari hizi hupewa nguvu zaidi na huduma duni za uzazi na kushtukia uzao wa watoto wachanga bila kutarajia na hivyo kutojua la kufanya kuwahudumia miongoni mwa nchi zilizoko kusini mwa jangwa la sahara barani Afrika.

Uzao wa mapacha ni jambo la kawaida zaidi katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara Afrika kuliko kwingineko duniani, watafiti wanasema.

Kwa mujibu wa takwimu, eneo hilo lina watoto 18 mapacha kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa.

Wakati eneo la Asia Mashariki na Amerika ya Kusini huzaliwa watoto sita hadi tisa mapacha kwa kila watoto 1,000 huku Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati watoto wakiwa wanane hadi 16 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa.

Pamoja na kuongoza kwa uzazi wa mapacha, kama kawaida kutokana na umasikini, wanawake wenye mimba eneo hilo wana uwezekano mdogo zaidi ya kupokea huduma za afya au kujikuta wakizaa nje ya vituo vya afya.

“Kinachotakiwa kufanyika ni kutilia mkazo ugunduzi wa mapema wa mimba za mapacha na kuongeza vifaa na vituo vya afya kwa ajili ya wanawake wenye mapacha ili wajifungulie hospitalini,” mwandishi mwenza wa utafiti huo, Christiaan Monden kutoka Chuo Kikuu cha Oxford anasema na kuongeza:

“Kilicho wazi ili kufanikisha hilo kuna changamoto za kifedha na kiutamaduni. Ni kweli kiwango cha vifo vya mapacha kinatarajia kuwa kikubwa zaidi ya tulichobaini katika utafiti.”

Katika nchi ya Finland ambayo kwa mfano ina huduma bora za uzazi duniani – watafiti wanasema kwa kila mapacha 1,000 wanaozaliwa ni 11 tu kati yao hufa kabla ya kutimiza umri wa mwaka mmoja.

Kulingana na utafiti huo kati ya mapacha 1000 wanaozaliwa 137 hufa kabla ya kuadhimisha mwaka mmoja wa kuzaliwa kusini mwa jangwa la Sahara Afrika.

Aidha, katika eneo hili mapacha 213 kati ya 1,000 hufa kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano.

Kwa sababu hizo, watafiti walibainisha kuwa hatari hizo zinasababishwa na kiwango kikubwa cha uzazi, huduma duni za afya kwa vichanga eneo hilo, ambalo wengi wanajifungulia majumbani kitu ambacho wanasema kinapaswa kubadilika

Profesa Monden anasema: “Hadi sasa, hatima mbaya ya mapacha imekuwa ikipita bila kushuhudiwa.”

Anasema kwamba mimba za mapacha zinapaswa kugundulika mapema na wamama kuzaa mapacha hospitalini kwa msaada wa watumishi wa afya waliofuzu kuzalisha mapacha.

Hilo linapaswa kuendelea na ufuatiliaji wa karibu wa siku chache na hata miezi kadhaa baada ya kuzaliwa kwao.

Lakini hii ni changamoto kubwa kwa mataifa masikini yenye mifumo dhaifu kabisa ya afya duniani.

Familia hasa zinazoishi vijijini mara nyingi hazina hospitali karibu na wanakoishi.

Wengi hawawezi kustahimili gharama za usafiri wa kuwapeleka katika vituo vya afya achilia mbali kuigharimia huduma yenyewe hiyo ya afya.

Hata ikitokea wakaweza, vituo vya afya huwa havina wataalamu wenye uwezo wa kushughulika na mapacha katika nchi nyingi zilizoendelea.

Profesa Monden aliongeza: “Ni rahisi kusema kina mama wanapaswa kuzaa katika hospitali nzuri lakini wengi kwa hali na mazingira yao hawana jinsi.

“Kilichotushangaza zaidi ni pale tulipobaini kuwa kiwango kikubwa cha vifo miongoni mwa mapacha hakifahamiki kwa mashirika makubwa kama vile ya Umoja wa Maraifa (UN) na hivyo hakuna kipaumbele kwa kundi hili.”

Mwandishi mwenza, Dk. Jeroen Smits, kutoka Chuo Kikuu cha Radboud nchini Uholanzi anasema: “Bila kipaumbele maalumu kwa kundi hili itakuwa ngumu kufikia malengo ya maendeeo endelevu ya UN ya kuwa na vifo vichache vya wachanga 12 kwa kila watoto 1,000 na chini ya watoto 25 kwa kila watoto 1,000 wafikishao umri wa miaka mitani ifikapo 2030.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here