25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HOTUBA YA SUGU NUSURA IVURUGE BUNGE

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

HOTUBA ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nusura ivuruge Bunge, baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kumzuia Msemaji Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu, asisome baadhi ya maneno yaliyodaiwa kukiuka kanuni za Bunge, likiwamo suala la Ben Saanane.

Tukio hilo lilitokea wakati Sugu alipokuwa akisoma hotuba hiyo, iliyotanguliwa na Hotuba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Dalili za hotuba hiyo kuzuiwa kusomwa yote zilianza mapema, wakati Zungu alipokuwa akisoma matangazo ya Bunge baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Katika maelezo yake wakati huo, Zungu alisema msomaji wa hotuba hiyo atatakiwa kutosoma kuanzia ukurasa wa sita hadi wa 10 na ukurasa wa 37 hadi wa 47, kwa kuwa zilikuwa na maneno yaliyodaiwa kukiuka Kanuni za Bunge.

Pamoja na kutoa maelekezo hayo, alisema mbunge yeyote atakayeona uamuzi wake haukutenda haki, atatakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwa kutumia kanuni ya 5 (4).

“Hapa tunafuata kanuni na mimi hapa ndiyo nina kadi, nina filimbi na nina jezi kabisa kwa sababu nyie huko mmevaa nguo za kawaida.

“Kwa hiyo, msemaji wa kambi ya upinzani wa wizara hii, naomba atakapokuja hapa, asisome ukurasa wa sita hadi wa 10 na asisome ukurasa wa 37 hadi wa 47,” aliagiza Zungu.

Hata hivyo, wakati Sugu akiwasilisha hotuba hiyo, alikwenda kinyume na

maelekeo ya Zungu kwa kutaka kusoma na kurasa alizokuwa amezuiwa, ukiwamo ukurasa uliohusu kutoweka kwa Saanane, aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Kutokana na hali hiyo, Zungu alizima kipaza sauti cha mbunge huyo na kumtaka afuate maelekezo, jambo ambalo Sugu hakuwa tayari kulifuata.

“Mheshimiwa Sugu, nakuomba usisome hayo unayotaka kusoma, soma ukurasa wa 12 ambao sisi tunao hapa, nakuomba tafadhali maana ruling (uamuzi) yangu

ikishatolewa, huwezi kuihoji hapa,” alisema Zungu.

Pamoja na maelekezo hayo na mengine, Sugu alikataa kuyafuata na badala yake alisisitiza umuhimu wa kusoma kilichoandikwa na kambi yake kwa kuwa ndicho wanachoamini.

Baada ya mvutano huo kuongezeka, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliomba mwongozo na kueleza jinsi asivyoridhishwa na utaratibu wa kuwazuia wapinzani wasiwasilishe baadhi ya maoni yao.

“Kwa hiki kilichofanyika sasa hivi, kinaonyesha Serikali inataka kutupangia mambo ya kuzungumza sisi wapinzani.

“Lakini kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuhusu majadiliano, mbunge ataruhusiwa kuzungumza na kama ataambiwa amekosea, aliyesema amekosea atatakiwa kuwasilisha ushahidi.

“Huu utaratibu wa Serikali kuchukua hotuba za upinzani na kuamuru ni kipi kisemwe na kipi kisisemwe, hatuukubali.

“Kama ni hivyo, msemaji wa upande wa Serikali ahame kwenye kiti chake na kuja kukaa hapo ili ieleweke Bunge hili linaongozwa na Serikali,” alisema Lissu.

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, naye asimame baada ya kuomba mwongozo.

Katika maelezo yake, Jenister aliitaka Kambi ya Upinzani ifuate maelekezo ya

Zungu kwa kutosoma maneno aliyoyazuia.

“Namuelewa mheshimiwa Tundu Lissu, lakini tunapofanya kazi hapa bungeni, lazima tufuate kanuni zinazotuongoza.

“Kwa kuwa yeye ni chief whip (mnadhimu) wa upinzani, na mimi pia ni chief whip (mnadhimu) wa Serikali aelewe kwamba, aliyezuia hotuba isisomwe ni wewe mwenyekiti wala sio mimi.

“Lakini kama kuna maeneo tunashindwa kuelewana, tunatakiwa tukae pamoja ili tuangalie namna ya kutatua tatizo lililopo kwa sababu hata kanuni ya 64 inaeleza wazi ni nini kinatakiwa kujadiliwa hapa,” alisema Mhagama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema), alipoomba mwongozo na kuruhusiwa alilalamikia utaratibu wa Kambi ya Upinzani kupangiwa maneno ya kusoma katika hotuba zao.

“Hata kama kuna muda watu wananyamaza, msidhani hawana maumivu. Iweje Serikali ituamulie mambo ya kuzungumza?

“Tukitoka bungeni mnaanza kutusema, tukibaki mnatunyanyasa kwa wingi wenu, hebu tuambieni mnataka tufanye nini?

“Kumbukeni leo mpo na kesho hampo, acheni kutunyanyasa,” alisema Bulaya.

Hata baada ya mvutano huo, Sugu alisusa kusoma hotuba hiyo kwa kutoridhishwa na maelekezo ya Zungu, licha ya kuruhusiwa aendelee kuiwasilisha.

SAKATA LA BASHITE

Katika hatua nyingine, Sugu alisema Serikali imeanza kumtambua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba ndiye Bashite.

Kauli hiyo aliitoa baadaye, baada ya kususa kusoma hotuba yake alipokuwa akichangia bajeti ya Dk. Mwakyembe ya mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Sugu alimshutumu Bashite kwamba amekuwa akitumia madaraka yake vibaya, ikiwa ni pamoja na kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds, akiwa na askari waliokuwa na silaha.

Katika maelezo yake, Sugu alisema Bashite ni jambazi na amefoji vyeti na kwamba anatakiwa kufikishwa mahakamani akajibu mashtaka.

“Mheshimiwa waziri, utakapokuja hapa kutoa majibu, naomba utueleze juu ya ripoti ya Nape Nnauye (aliyekuwa Waziri wa Habari kabla ya Dk. Mwakyembe) kuhusu Bashite, kwamba wakati anavamia Clouds alikuwa na akina nani.

“Kwanini Bashite analindwa, huyu analindwa kwa maagizo ya nani? Huyu Bashite ni nani asifikishwe mahakamani wakati ni jambazi na amefoji vyeti, kwanini asishtakiwe,” alihoji Sugu, huku akipigiwa makofi na wabunge wa upinzani.

Wakati akiendelea kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, aliomba mwongozo kwa Zungu na kusema anayetajwa kama Bashite ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo, kabla hajaendelea kuchangia, wabunge wa upinzani walipaza sauti na kusema mkuu huyo wa mkoa hajatajwa jina kama Bashite, bali Bashite anatajwa kama Bashite.

Maneno hayo yalimfanya Simbachawene acheke na kusema kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam si Bashite, anaondoa hoja yake.

“Mwenyekiti, huyu anayetajwa kama Bashite ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini, kama wanasema Mkuu huyo wa Mkoa si Bashite, basi naondoa hoja yangu,” alisema Simbachawene huku akicheka.

Baada ya maneno hayo, Sugu aliendelea kuchangia na kusema kitendo cha Simbachawene kusema Bashite ndiye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ni kielelezo kwamba sasa Serikali imeanza kumtambua kuwa ndiye mkuu wa mkoa huo.

Kuhusu wasanii, aliwataka wasiendelee kushirikiana na Bashite, kwa kuwa vyombo vya habari nchini vimesusia kuandika habari zake baada ya kukiuka uhuru wa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Sugu, wasanii wanatakiwa kushirikiana na vyombo vya habari katika masuala mbalimbali, kwa kuwa vyombo hivyo vimekuwa vikitoa msaada mkubwa kwao.

Pia alimtaka Msanii Roma Mkatoliki, aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana hivi karibuni, ajitokeze hadharani na kusema kilichomkuta na waliomteka ni akina nani.

“Wasanii waache kutumika kwa sababu vyombo vya habari nchini vimemsusia Bashite na ni jambo lisilokubalika wasanii kwenda kinyume na vyombo hivyo,” alisema Sugu.

Naye Lissu aliwataka wabunge washirikiane kutunga sheria nzuri, kwa kuwa hata wao zinaweza kuwakandamiza pindi watakapokuwa na makosa.

Katika maelezo yake, Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alilalamikia sheria tatu zilizopitishwa na Bunge

kwa nyakati tofauti, kwamba hazikustahili kupitishwa na Bunge hilo.

Alizitaja kuwa ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki.

Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliitaka Serikali iwekeze kwa kununua mitambo ya kisasa kwa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) ili liweze kurusha matangazo kwa

mafanikio.

Kwa mujibu wa Nkamia, TBC haina mitambo ya kisasa na kwamba kuna

wakati shirika hilo linaazima mitambo kwa watu binafsi ili kurusha matangazo yake.

Pamoja na hayo, alisema kwa kuwa TBC halina mitambo ya kisasa ya kurushia matangazo, baadhi ya maeneo nchini wanapata matangazo ya redio za nje ya nchi kwa kuwa ndiyo yanayopatikana kwa urahisi.

MWAKYEMBE

Naye Dk. Mwakyembe alisema asilimia 90 ya wafanyakazi wa vituo vya utangazaji nchini hawana sifa za uandishi wa habari za utangazaji.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kusimamia ubora wa huduma za utangazaji kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya utangazaji kwa lengo la kuhakiki vitendeakazi na ubora wa huduma zinazotolewa na vituo hivyo.

“Maeneo yaliyohakikiwa ni pamoja na studio, vyumba vya kuandaa habari, maktaba, utaratibu wa ndani wa kuandaa na kutangaza vipindi, sifa za watangazaji na waandishi wa habari na mikataba ya ajira.

“Vituo vyote vilivyokaguliwa vilionyesha ubora katika kutoa huduma kwa wasikilizaji wake katika maeneo husika, ikiwa ni pamoja na ubora wa

usikivu ambao hauna miingiliano ya sauti, ubora wa vitendea kazi katika vituo, uelewa wa taratibu na sheria za utangazaji pamoja na uwezo wa kituo katika kutimiza haki na maslahi ya wafanyakazi wake.

“Lakini katika ukaguzi huo, asilimia 90 ya wafanyakazi walibainika hawana sifa stahiki katika taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji, jambo linaloifanya iendelee kuwa changamoto kubwa katika tasnia ya habari na utangazaji nchini,” alisema Dk. Mwakyembe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles