26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

CCM YAMPA LIKIZO KINANA

ABRAHAM GWANDU NA ELIYA MBONEA

-ARUSHA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimempa mapumziko ya muda ambao hakijautaja Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kiongozi huyo ameruhusiwa kupumzika ili kuangalia afya yake hadi hapo itakapoimarika.

Polepole alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake iliyolenga kukagua uhai wa CCM mkoani hapa, ikiwa ni eneo linalotajwa kuwa ngome ya chama kikuu cha upinzani, Chadema.

Kauli hiyo ya Polepole imekuja ikiwa ni muda sasa Kinana hajaonekana hadharani, hatua ambayo imezusha maneno mengi, huku baadhi wakienda mbali na kuhusisha kitendo hicho na mgomo kutokana na uamuzi wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kumvua uwaziri wa Habari, Vijana Sanaa na Michezo ‘kijana wake’, Nape Nnauye.

Kuwapo kwa hisia za namna hiyo kunatokana na kile ambacho CCM ilidai kuwa ni uvumi, kwamba Kinana alitaka kuitisha mkutano na wanahabari siku moja baada ya Nape kuondolewa kwenye wadhifa huo na saa chache baadaye wakati akielekea kuzungumza na vyombo vya habari kutishiwa kwa bastola na mtu ambaye haijajulikana anafanya kazi wapi.

Ni wakati huo Rais Magufuli alilazimika kuzungumzia mahali alipo Kinana, akisema alikuwa amemtuma kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.

Rais Magufuli alitoa ufafanuzi huo wakati akiwaapisha Mawaziri Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Dk. Harrison Mwakyembe aliyechukua nafasi ya Nape.

Akitoa ufafanuzi kuhusu afya ya Kinana, baada ya kuulizwa swali na Mwandishi wa MTANZANIA aliyetaka kujua ukimya wa Kinana na kutoonekana kwa kipindi kirefu, Polepole alisema wamekubaliana achukue muda wa kutosha ili kutazama afya yake, baada ya kufanya shughuli nyingi za chama na serikali.

Imezoeleka kiongozi yeyote anapougua viongozi wenzake kwenda kumjulia hali hospitalini anakopatiwa matibabu au nyumbani kwake, lakini kwa Kinana imekuwa ni tofauti.

Hadi sasa hakuna picha yoyote inayomwonyesha kiongozi au mtu yeyote amefika nyumbani kwa Kinana kwa ajili ya kumjulia hali, jambo ambalo limezidi kuzua maswali.

 “Hili swali la Katibu wetu Mkuu ndugu Komrade Abdulrahmani Kinana limesemwa sana na mimi ninafurahi kwamba tunaanza kurejesha utamaduni ambao maisha ya viongozi wetu yanakuwa sehemu na maslahi ya umma wa Watanzania,” alisema Polepole na kuongeza:

“Lakini unapoona Katibu wetu Mkuu wa CCM anaulizwaulizwa yuko wapi na hata watu wasiokuwa wana CCM, hii inaonyesha kiwango cha imani cha Watanzania kinarejea kwa kasi kubwa, hasa katika kipindi hiki tunapofanya mageuzi makubwa ndani ya chama chetu. 

“Na kwa hakika najua viongozi wa vyama vingine wasioonekana hawauliziwi na mtu yeyote, kwetu sisi ni dalili njema sana. Nipende tu kuwaambia jana nimeongea na Komrade Kinana bado yuko kwenye mapumziko ya kujitizama afya yake.

“Ninyi wote ni mashahidi mzee wetu huyu alifanya kazi kubwa ndani ya CCM na kwenye Serikali na pia kwenye wigo wa kimataifa, hasa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

“Lakini amefanya kazi kubwa zaidi kwenye chama ya kukijenga na kukiimarisha, hasa kwenye uongozi na utendaji kama Mtendaji Mkuu wa Chama.

“Leo labda niseme kwa sehemu mpaka wakati tunamaliza Mkutano Mkuu Maalumu ambao ulipitisha marekebisho na mabadiliko ya Katiba Ndugu Komrade Kinana alikuwa anafanya yote haya, lakini akiwa mgonjwa, akiugulia na sisi kwenye chama tuna utaratibu na tunawapenda viongozi wetu.

“Kwa hiyo ikakubalika achukue muda wa kutosha wa kuitazama afya yake nje ya nchi na kiongozi wa aina yake anaporejea, mgonjwa akitoka hospitali hakimbilii kazini au shambani moja kwa moja, inashauriwa kitaalamu atumie muda wa kupumzika ili kuimarisha afya yake.

“Na jana (juzi) nimezungumza naye anaendelea vizuri, yuko madhubuti kabisa kuliko jana, kwa hiyo nashukuru wale wote wanaofuatilia habari zetu za CCM na iwe mfano kwa vyama vingine,” alisema. 

Mbali na hilo, Polepole pia alizungumzia hali ya siasa katika Mkoa wa Arusha, akisema baada ya kufanya ziara yake hiyo amebaini kuwa tofauti na miaka michache iliyopita, chama hicho sasa ni bora na madhubuti.

“Nina furaha kuwa chama chetu sasa baada ya kufanya uamuzi wa kuondoa wale wote ambao walikuwa wamekosa uadilifu, wala rushwa na wabadhirifu wa mali za CCM, hali ya uhai ni bora na madhubuti kuliko jana.

“Uongozi wa awamu ya tano umejikita katika kurejesha nidhamu na uadilifu serikalini na ndani ya chama, hatuna ajizi katika kuchukua hatua ya kukisafisha chama chetu kwa kuwaondoa viongozi na wanachama wote waliofanya uzembe, wabaguzi, wanaopendelea kwa misingi ya dini na ukabila,” aliongeza Katibu wa Itikadi na Uenezi.

 Polepole alisisitiza agizo la CCM kwa serikali kuhakikisha kuwa inapeleka chakula kitakachouzwa kwa bei nafuu kwa wakazi wa wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,922FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles