22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali zatumia maji ya vinyesi

SAM_1430Na Asifiwe George, Dar es Salaam

UTAFITI uliofanywa umebaini kuwa asilimia 46.5 ya hospitali za nchini zinatumia maji yenye vimelea vya kinyesi (Ecoli).

Kauli hiyo ilitolewa juzi Dar es Salaam na mtafiti ambaye pia ni mtaalamu wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Robert Njee, katika mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu usafi wa mazingira na maji, yaliyoratibiwa na Taasisi ya Tanzania Water and Sanitation Network (TaWaSaNet).

Alisema hayo yamebainika katika utafiti uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana ukihusisha wilaya saba, huku Hospitali ya Wilaya ya Mbarali mkoni Mbeya inaongoza kwa kuwa na matumizi ya maji yenye vimelea vya kinyesi (Ecoli) kwa asilimia 57.9.

Njee alisema kuwa hospitali za wilaya za Temeke, Dar es Salaam na Mufindi mkoani Iringa, zinashika nafasi ya pili katika matumizi ya maji yasiyo salama kwa asilimia 57.1 zikifuatiwa na Hospitali ya Mkoa wa Mbeya yenye asilimia 45.5.

Alizitaja hospitali nyingine kuwa ni Makete kwa asilimia 40.7, Njombe asilimia 38.1 pamoja na Iringa yenye asilimia 30.8.

Mtaalamu huyo wa mazingira, alisema kuwa wilaya hizo saba zilifanyiwa utafiti kwa lengo la kuunga mkono Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kuboresha huduma za afya kupitia unawaji, utoaji wa huduma kwa mama na mtoto na kudhibiti utumiaji wa maji.

Njee alisema lengo jingine lilikuwa ni kuangalia na kutathimini utoaji wa huduma kwa jamii kwa kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na utakasaji mikono.

“Utafiti unaonyesha kwamba zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya, ikiwamo mifumo ya bajeti, vipaumbele kuwa vidogo, miundombinu mibovu ya maji pamoja na watumishi wa usafi mikoani kutofanya usafi na badala yake kukimbilia kazi za kitaaluma,” alisema Njee.

Kwa upande wake, Dk. Hamiss Malebo wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alisema yapo magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira pamoja na maji na yamekuwa yakisababisha vifo 760,000 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa mwaka.

Aliyataja magonjwa hayo kuwa ni kuhara, kipindupindu, minyoo, taifodi, magonjwa ya ngozi, macho, nimonia, TB na uvimbe kwenye kichwa unaotokana na maji.

Kwa upande wake, Mhandisi Wilhemina Malima kutoka Water Supply and Sanitation Collaborative Council (WSSCC), alisema magonjwa mengi ya milipuko ikiwamo kipindupindu yanasababishwa na matumizi ya maji ya visima vilivyochimbwa pembezoni mwa vyoo.

Alisema visima hivyo vimeonekana kutokuwa na ubora kutokana na kuchanganyika na mtiririko wa maji ya vyoo na havijathibitishwa na wataalamu.

 

MATUMIZI YA MAJI NA KIPINDUPINDU

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuambukiza wa kuharisha unaosababishwa na vijidudu vya bakteria. Ugonjwa huu hutokana na matumizi ya maji yasiyo safi au chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi.

Ugonjwa huu ni wa ghafla na kwa watu wengi hauleti dalili kali sana. Ingawa unatibika, unaweza kuwa hatari sana na kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

 

MAAMBUKIZI

Kipindupindu hutokana na maambukizi ya vijidudu vya bakteria viitwavyo Vibrio cholera ambavyo hukaa kwenye majimaji, ambapo wadudu kama nzi wanaweza kuvihamisha kutoka sehemu moja mpaka nyingine.

Maambukizi hutokea pale ambapo usafi wa maji, chakula, mazingira na binafsi haujazingatiwa. Kwa njia ya chakula, vijidudu huingia kwenye utumbo na kisha kushambulia seli za utumbo.

 

NAMNA YA KUJIKINGA

Usafi binafsi, chakula na mazingira ni muhimu ili kujikinga na kuzuia ugonjwa wa kipindupindu ambao husambazwa kwa kutozingatia usafi.

Kuzuia ugonjwa huu unapaswa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kila baada ya kutoka chooni.

Kunawa mikono kwa maji safi kabla na baada ya kula chakula au matunda na kuyaosha kwa maji safi kabla ya kula.

Kutumia maji ya kunywa safi yaliyochemshwa au kutakaswa kwa dawa na kuhifadhiwa katika chombo kisafi.

Kuhakikisha unakula chakula ambacho hakijapoa. Kiwe cha moto na kimehifadhiwa katika chombo kisafi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles