23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HIZI NI RASHARASHA TU, NJAA HALISI MACHI MWAKA HUU

mtz10-23-2

Na David Kafulila,

NI vema Rais John Magufuli akajua kwamba kwa namna anavyowasimamia walio chini yake upo uwezekano mkubwa wa kupotoshwa na wasaidizi wake kuhusu ukweli na ukubwa wa tatizo la njaa kwa hofu ya kutumbuliwa.

Ndio maana hata Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula nchini inampotosha ilhali taarifa za kiuchumi zipo wazi kwenye tovuti ya Benki Kuu.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tathmini ya Uchumi ya Oktoba iliyotolewa Novemba 2016, (Monthly Economic Review), akiba ya chakula nchini ni ndogo sana. Inaonyesha Oktoba 2016, akiba ilikuwa tani 90,476, wakati Oktoba miaka mingine hali ya chakula ilikuwa kama ifuatavyo; mwaka 2015 zilikuwamo tani 253,656, mwaka 2014 tani 426, 999 na mwaka 2013 tani 23,5817.

Hii ni taarifa ya BoT, ambayo ni ya mwisho kutolewa kwenye tovuti ya BoT, kama wataalamu wake hawasomi hilo ni tatizo.

Hali ya njaa ilishatabiriwa na Shirika la Chakula duniani (FAO), tangu Julai 28, 2016 kwamba ukanda wa Kusini mwa Afrika utakabiliwa na njaa kuanzia mwishoni mwa Desemba hadi Machi 2017 na huenda hali ikaendelea mpaka katikati ya mwaka 2018, kama hatua hazitachukuliwa kusaidia wakulima wadogo hasa kwa kuwapatia pembejeo mapema na wapande mapema mvua za Oktoba 2016.

Aidha, kuna uwezekano wa watu zaidi ya milioni 23 kukosa kabisa chakula. Hizi ni taarifa zipo kwenye tovuti ya Shirika hilo la chakula duniani.

Nchi zilizotajwa hapo ni pamoja na Tanzania, Malawi, Msumbiji, Namibia, Swaziland, Lesotho, Zambia na Zimbabwe.

Wakati taarifa hii ya Shirika la Chakula Duniani ikitoa tahadhari hiyo na kutaka nchi husika kusaidia wakulima mbolea na dawa na kuwataka walime kwa wakati mvua za mwezi Oktoba, Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, ruzuku ya mbolea ilishushwa kutoka Sh bilioni 78 za mwaka 2015/16 mpaka bilioni 10 mwaka 2016/17. Hii inaashiria Serikali haikujua kinachoendelea kwenye kilimo na hali ya chakula duniani.

Shirika hilo limeshatoa taarifa kuhusu njaa kali pembe ya Afrika ambapo Kenya ni moja ya waathirika, ni kwa sababu hiyo kiasi kikubwa cha chakula Tanzania kimeuzwa na kuzidisha makali ya njaa nchini.

Taarifa zote hizi za BoT, FAO kuhusu baa la njaa pembe ya Afrika na uhaba wa chakula Kusini mwa Afrika, ni taarifa tosha na za mapema kwa Serikali kujiandaa lakini cha kushangaza ndiyo hivyo tena ruzuku ya mbolea inashuka huku akiba ya chakula inakuwa pungufu ya ile ya mwaka jana kwa zaidi ya asilimia 200.

Nchini Kenya katika bajeti yao ya 2016/17 moja ya mijadala mikubwa ilihusu usalama wa chakula kwa hofu hiyo waliongeza fedha kwa ajili ya akiba ya chakula na ruzuku ya mbolea kwa wakulima kama ilivyoshauriwa na FAO, sisi Tanzania ndio kwanza tukapunguza ruzuku ya mbolea.

Ni vema Serikali ikachukua hatua za kuliweka Taifa pamoja katika baa hili la njaa kuliko kuendelea kujibizana na kuligeuza suala la kisiasa, kwamba wanasiasa wajibizane kuhusu ukweli wa njaa wakati wananchi wanaendelea kuumia. Hili ni janga.

Kinachofanywa sasa kukanusha janga la njaa kinanipa hofu kwamba kama isingekuwa dunia ya utandawazi wa habari, inawezekana Serikali ingekanusha tukio hilo kwa watu wa pande nyingine za nchi yetu. Sioni sababu hata moja ya kwanini jambo hili lipelekwe hivi kiuongozi.

Kama nilivyoeleza awali kwamba kwa mujibu wa ripoti hiyo ya FAO, njaa ilitabiriwa kuanza Machi mwaka huu, hivyo njaa ya sasa ni manyunyu, yenyewe inakuja rasmi kuanzia Machi.

Na kwa sababu eneo linalopigwa zaidi na baa hili ni Kusini mwa Afrika ambapo sisi tumo na pembe ya Afrika ambao ni jirani zetu Kenya, hivyo tuna njaa yetu na tuna tatizo la njaa ya jirani yetu Kenya ambapo athari zake ni pamoja na chakula kidogo kilichopo kusombwa kupelekwa kuuzwa huko.

Nilidhani ni hekima ya uongozi kulichukulia jambo hili kwa uzani mkubwa, ilipaswa kujiandaa tangu mwaka jana na kuchukua hatua, hatukufanya na ndiyo sababu kiasi cha akiba ya chakula kipo chini ya rekodi za zaidi ya miaka mitano nyuma kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu.

Kwa kuwa hatukuchukua tahadhari ya kukabili tatizo hili, ni jukumu la Serikali kupunguza athari za baa lenyewe (ku manage damage), kwa kufanya hivyo tutapunguza vifo vya watu na mifugo kutokana na baa hili la njaa ambalo ni matokeo ya ukame kwa upande mmoja na ukali wa athari zake ni pamoja na sababu za kutojiandaa.

Kwa upande mwingine, kwa utajiri wa maji na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji tunaweza kugeuza njaa ya ukanda huu kuwa biashara kwetu.

Hakuna ubishi kuwa dunia ya sasa hatutaweza kujihakikishia chakula kwa kilimo cha kutegemea mvua. Mabadiliko ya tabia nchi yanafanya mvua isiwe ya uhakika na kasi kubwa ya ongezeko la kuzaliana karibu asilimia 3 kwa mwaka ni changamoto kwa uhakika wa chakula.

Tanzania inasomwa kama nchi ya 11 kwa mito mingi duniani na ikiwa na maziwa yenye maji baridi ya kutosha kuanzia Ziwa Victoria ambalo walau linatumika lakini Ziwa Tanganyika ambalo halitumiki kabisa. Ziwa Tanganyika peke yake kwa mujibu wa ripoti ya hali ya maji duniani, mwaka 2011, lilikuwa na kiasi cha kilomita za ujazo 5,800,000, wakati dunia nzima ilikuwa na maji baridi kilomita za ujazo 35,000,000.

Ziwa Tanganyika ambalo linagusa nchi za Zambia, DRC na Burundi, Tanzania ndiyo ina eneo kubwa la ziwa hilo zaidi ya asilimia 45. Huu ni utajiri mkubwa tunapozungumza kilimo cha umwagiliaji.

Mbali ya maji hayo, Tanzania ina fursa ya mabonde kiasi cha hekta milioni 29.4 na kwa zaidi ya nusu karne hatujaweza kutengeneza miradi ya kilimo cha umwagiliaji japo kufikia hekta 400,000.

Hivyo kwa utajiri huo wa maji ya ziwa na mito mingi sanjari na utajiri huu wa mabonde, bila kusahau japo ng’ombe, kwamba kama hatuwezi trekta basi walau ng’ombe. Tanzania ni nchi ya tatu kwa mifugo hao, tunaweza kuinua kilimo na njaa inayotikisa ukanda wetu wa Kusini na pembe ya Afrika kuwa biashara kwetu.

Inasikitisha mkulima anapolima kwa jasho lake kisha wakati wa kuuza anazuiwa asiuze nje kwa bei nzuri apate tija ya nguvu yake kwa hoja kwamba nchi ina uhaba wa chakula. Huu ni mfumo wa kinyonyaji kwa wakulima wanyonge. Serikali kama inajua kuna uhaba iwawezeshe zaidi waweze kulima na kuuza nje.

Hivyo hilo la kilimo cha umwagiliaji ni mkakati wa muda mrefu na pengine lingeanza kupewa uzito kuanzia bajeti ya 2017/18, ni lazima Serikali iweke uzito hapo kwani kutengeneza mradi wa umwagiliaji hekta 1 ni wastani wa kati ya dola za Kimarekani 1,500 mpaka dola 25,000. Hivyo inahitaji mkakati wa Serikali na wakulima wakubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles