24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI BARACK OBAMA LAKINI…

150723174958-obama-family-christmas-2014-restricted-super-169

NA MARKUS MPANGALA,

ZIMESALIA siku nne tu Rais wa Marekani, Barack Obama, kung’atuka madarakani.

Rais huyo anatarajia kumkabidhi Ikulu ya Marekani Rais mteule, Donald Trump, Ijumaa wiki ijayo.

Kabla ya tukio hilo kufanyika hivi karibuni Rais Obama alitoa hotuba ya kuaga taifa hilo akiwa mjini Chicago, nchini humo.

Kama kawaida yake, aliongea kwa pozi, sentensi moja na nyingine zilitawaliwa na tuo, alivuta pumzi, akatuliza kichwa.

Midomo yake ilitamka maneno yanayowavuta wapigakura, wanasiasa, viongozi na zaidi kuvuta usikivu miongoni mwa wanajamii.

Obama alikuwa yuleyule wa mwaka 2004 alipotikisa nchi hiyo alipokuwa Seneta Illinois. Obama alikuwa yuleyule wa mwaka 2008 akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

Alikuwa Obama yuleyule jasiri na mwenye nguvu za hoja zilizomshinda John McCain wa Republican wakati wa midahalo ya kuwania urais. Alionyesha uimara wake wa kuivuta hadhira, maneno yake yalijaa hekima, kiunganishi na kujenga umoja.

Na pengine ndiyo desturi ya Chama cha Democrat kuunganisha wananchi na hata viongozi wa ulimwengu kuliko Republican wenye taswira kama ya Donald Trump, George W. Bush mkubwa na George W. Bush mtoto au kina Henry Kissinger na wengineo.

Ni Obama yuleyule aliyemshinda Mitt Romeny wa chama cha Republican mwaka 2012 katika kinyang’anyiro cha urais.

Alikuwa Obama aliyesimama imara, akajenga hoja, aliongea kama kiongozi thabiti na mwenye kufurahia maisha binafsi ya kifamilia, uongozi na jeuri ya kuzaliwa Marekani. Na huo ni upande wa mwonekano wa mhutubiaji katika kuwasiliana na hadhira yake.

Katika hotuba yake kulikuwa na mambo mengi ambayo tunaweza kuyagawa katika makundi ya vilio, furaha yenye kutia moyo, kusikitisha na mafunzo kadha wa kadha katika anga za masuala ya siasa ulimwenguni hususani uongozi na demokrasia.

Ni mafunzo ambayo yamekuwa adimu kutolewa kwa baadhi ya wanasiasa, lakini Obama amedhihirisha kuwa bado kinara wa kuhamasisha, kutia moyo, uwezo mkubwa wa ushawishi kwa wapigakura na zaidi anakuwa kiongozi wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika kumaliza kipindi cha miaka 8 madarakani. Obama anaondoka akiwa na rekodi mbalimbali za kiutendaji, ikiwemo mazuri na mabaya yake.

Mathalani kwenye hotuba yake alisema: “Baada ya miaka nane ya kuwa rais wenu, bado naamini kwamba na ieleweke si suala la imani pekee bali mapigo ya mioyo yetu Wamarekani, tumekumbatia uzoefu na mtindo wetu wa kuunda Serikali ya kipekee kila mara.”

Nini tafsiri ya nukuu tuliyochukua? Ni dhahiri Obama anathibitisha kuwa muundo wa Serikali na sera za Marekani zimekuwa za kipekee na dunia imeshuhudia yote hayo.

Katika upande wa furaha Marekani imeleta mambo mengi yenye kuheshimika kuanzia viunga vya Umoja wa Mataifa, hisa zake katika Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani ni miongoni mwa mashirika makubwa ambayo yamekuwa yakitumiwa na mataifa mbalimbali kujipatia mikopo.

Aidha, muundo wa kipekee wa Marekani ni pamoja na kuileta dunia katika ardhi yao. Wanaweza kuweka mikakati katika masuala ya ulinzi, kulinda masilahi yao, kushikamana na mataifa rafiki na hata kuwa tayari kupambana kwa silaha za moto ili kuhakikisha masilahi yao yanakuwa kwenye mikono sana.

Anadhihirisha kuwa nchi yao imekuwa kwenye mkondo wa kuendesha mambo inayoyataka kwa wengine bila bughudha na kuhakikisha mawazo yao ya Kimarekani yanatawala dunia.

Hakuna biashara kubwa ambayo Marekani inafanya kama kuuza mawazo yake. Biashara hii imekuwa muhimu na ndio msingi wa sera mbalimbali, tangu ilipoiga hayo kutoka kwa wakoloni wa jamii za Ulaya hususani Uingereza. Tukumbuke pia jamii za Uingereza nazo zilijikita kwa jamii za Italia.

Sehemu nyingine anasema: “Kwa miaka 240, suala la ukazi wa wananchi katika taifa letu limetupatia kazi na umuhimu wa kukiachia mafunzo kizazi kimoja hadi kingine. Ni hicho kinachotuongoza, ni uzalendo wetu tuliochagua kama taifa, kuanzia chipukizi hadi wakongwe, toka zama za utumwa hadi ushujaa wa kutengeneza reli ya mafanikio ya nchi.”

Tafsiri ya nukuu hiyo ni kwamba, utaifa wa Marekani umeundwa Kimarekani, ndio maana katika mitaala ya elimu hapa nchini tuliwahi kufunzwa juu ya ubeberu wa Kimarekani (America Capitalism) ambayo ilielezwa kuwa tofauti na ubeberu wa Uingereza (British Capitalism). Sababu kubwa ni moja; Marekani walitafuta uhuru wao, wakatengeneza mawazo yao, wakayauza kote duniani.

Kisha wakabuni silaha na vita kama bidhaa muhimu kwenye soko la biashara. Maeneo mengi ambayo Wamarekani wapo yanakuwa na bidhaa mbili kuu; silaha na vita.

Kwa wataalamu wa masuala ya siasa ya kimataifa wanaelewa ninachosema kuwa silaha na vita ni miongoni mwa bidhaa muhimu mno kwenye mafanikio ya nchi kama Marekani.

Mifumo yao ya uchaguzi ya kura za moja kwa moja za wananchi (Electoral Vote) na kura za wajumbe wa majimbo (Electoral College) ni wa kipekee ambapo iwapo mgombea hajapata kura nyingi za wajumbe anaangushwa hata kama alipata kura nyingi za wananchi.

Ni mfumo wa kipekee wa Kimarekani, ndiyo ufahari wa Obama anaozungumzia kwenye hotuba yake juu ya miaka 240 ya fikra za Kimarekani.

Aidha, tumejionea vilio ambavyo Obama anaviacha duniani. Obama anaondoka akiwa hajatatua suala la Afghanistan. Anaondoka akiwa Marekani hajatatua suala la Irak.

Obama anaondoka akiwa ameshindwa kukamilisha mradi wa kuwakabidhi wapinzani wa Rais Bashar Al Assad wa Syria. Katika mgogoro wa Syria tumeshuhudia malumbano makali baina ya Urusi na Marekani, lakini mwishowe Obama akaweka ‘silaha’ chini na kumwacha Vladimir Putin akiibuka mshindi.

Obama anaondoka akiwa ameacha wingu la jeuri huko Libya, ambapo Serikali yake ilishirikiana na majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) kumwangusha Rais Muammar Gaddafi.

Katika kipindi hicho, Obama alikaribia kuvunja sheria za nchi badala ya kusubiri kuidhinishiwa jeshi la kwenda vitani kwa siku 60 kutoka bungeni, lakini alikuwa tayari kuivunja.

Obama anaondoka katika kiti chake akiacha kilio cha Ukraine, ambao wametibuana na jirani yake Urusi kutokana na sakata la Jimbo la Crimea. Tumeshuhudia mapigano baina ya Ukraine na Urusi ambapo jimbo la Crimea lilitaka kujiunga na kuwa sehemu ya Shirikisho la Urusi kuliko kuwa sehemu ya Ukraine.

Obama ametuliza tu mgogoro wa silaha za nyuklia baina ya Iran na Marekani pamoja na nchi za Magharibi. Mgogoro wa Georgia uliolipuka zaidi Agosti mwaka 2008 dhidi ya Urusi haijamalizika.

Migogoro ambayo hajaimaliza licha ya kuingilia kati ni baina ya Israel na mataifa ya Asia hususani Iran, Irak, Mamlaka ya Palestina na Lebanon kwa kuzitaja chache. Ni mambo muhimu ambayo hakupaswa kuyaweka kiporo.

Na sifa kuu ya mwisho ya Marekani itakuwa kumkabidhi madaraka, Donald Trump kwa amani, tofauti na Yahya Jammeh wa Gambia anavyoshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria kumkabidhi Adama Barrow. Lakini je, ufahari wa Obama kiuongozi na chozi lake juu ya hali ya Libya ni furaha au kilio?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles