21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Hili la vyama vingi Rais Magufuli umenena

RAIS Dk. John Magufuli amesema anatamani kuona vyama vya siasa vya upinzani vinaendelea kuwapo ili kuleta ushindani dhidi ya chama tawala.

Hii ni mara ya kwanza Rais Magufuli kutoa kauli hii, ambayo kwa kweli ni ya kipekee na inapaswa kuungwa mkono na viongozi wengi kwa sababu tunaamini kuwapo vyama vya upinzani si dhambi.

Amesema pamoja na kutamka hivyo, anatambua wazi upinzani upo kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Hii ni kauli nzito ambayo hata wale ambao walikuwa na mawazo ya kudidimiza upinzani wanapaswa kujitafakari.

Anasema anatamani uwapo wa vyama vingi kwa sababu anaamini wazi vinasaidia kuleta changamoto dhidi ya chama tawala katika maeneo mbalimbali ambayo husimamia.

Tunakubaliana na kauli hii kwa sababu tunaamini kuwapo vyama hivi  kunasaidia kukichangamsha chama tawala pale ambapo panaonekana mambo hayaendi vizuri na mwisho wa siku wanarekebisha.

Kama waswahili wanavyosema “siasa si ugomvi”, tunaamini sasa hili litafungua milango ya vyama vya upinzani kuendelea na majukumu, ikiwamo kufanya mikutano ya hadhara ambayo imezuiwa, ikiruhusiwa kwa wabunge kufanya katika maeneo yao husika pekee.

Kwa kuwa Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa CCM, inawezenaka kwa namna moja ama nyingine ameona kuna kitu fulani kinakosekana katika ulingo wa siasa hadi kufikia kutoa kauli hii.

Pamoja na kauli hii njema, tunapingana na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ambaye anasema anatamani kuona chama kimoja tu cha siasa nchini ambacho kitaitwa ‘Magufuli Rulling Party’. Tunasema kauli ya aina hii si ya kiungwana kwa sababu mambo haya yapo kisheria.

Anasema haoni sababu ya kuwa na mfumo wa vyama vingi nchini eti kwa sababu tu Rais aliyepo madarakani amefanya mambo mengi na mema kwa nchi hii.

Tunapenda kumkumbusha Chalamila kuwa kama anataka kuondoa mfumo huu apelieke muswada bungeni ili sheria ibadilishwe, lakini pia anapaswa kupunguza mihemko ya kisiasa katika masuala nyeti ya kitaifa.

Pamoja na kuwa Chalamila ambaye pia ni kada wa chama tawala ana haki ya kutoa mawazo yake, lakini bado anapaswa kusimamia  na kuheshimu vitu ambavyo vimewekwa kisheria.

Licha ya hayo yote, tunasema rais ameonesha ukomavu wa kisiasa.

Ndiyo maana tunaamini kuwapo chama tawala na wapinzani, ni dalili nzuri ya kuchangamsha. Tunasema hili kwa sababu hata marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema  chama tawala kinapaswa kupata mawazo mbadala kutoka kwa wapinzani.

Alisema wapinzani wamekuwa na msaada mkubwa wa kukikumbusha chama tawala pale ambapo wanaona kuna mambo hayaendi sawa ili mwisho wa siku wayarekebishe kwa manufaa ya Watanzania wote.

Sisi MTANZANIA, tunasema rais katika hili umenena vema katika kipindi hiki ambacho kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wapinzani kwamba wamebanwa kufanya siasa katika maeneo mengine.

Tunashauri na kusisitiza kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania wenye moyo wa kujitolea kila kukicha, tunaamini wapinzani nao wana mchango wao ambao kwa hakika unaweza kuisaidia Serikali au chama tawala katika kuwaletea tija Watanzania wote bila kujali vyama vyao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles