Badi Mchomola
DIRISHA la usajili nchini England lilifungwa Agosti 8, mwaka huu huku uhamisho uliotikisa ni ule wa beki Harry Maguire akitokea Leicester City na kujiunga na Manchester United.
Mchezaji huyo raia wa nchini Uingereza alikamilisha uhamisho wake kwa kitita cha pauni milioni 80 kwa mkataba wa miaka mitano.
Mkaba huyo utamfanya mchezaji huyo awe anachukua kiasi cha pauni 190,000 kwa wiki, ambazo ni zaidi ya milioni 527 za Kitanzania.
Maguire ametajwa kuwa beki wa kwanza duniani kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika historia ya soka.
Kuna sababu mbalimbali zinazowafanya wachezaji kuhama timu moja kwenda nyingine na wengine kuamua kukaa kwenye timu moja kwa kipindi kirefu.
SPOTIKIKI leo inakuonesha tofauti ya uhamisho wa Maguire na kiungo wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil, Oscar dos Santos ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Shanghai SIPG inayoshiriki Ligi Kuu nchini China.
Kwenye soka kila mchezaji anakuwa na ndoto zake, wapo ambao wanakuwa na ndoto za kucheza soka kwenye klabu kubwa barani Ulaya, wengine wanaangalia klabu ambayo atapata fedha nyingi kwa ajili ya kuikomboa familia yake na mambo mengine mengi.
Harry Maguire
Kikubwa kilichomfanya Maguire ajiunge na Manchester United sio fedha, lakini kulikuwa na mambo mawili nakubwa.
Jambo la kwanza lililomfanya ajiunge na Manchester United ni kutimiza ndoto zake, tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Sheffield United mwaka 2011, ndoto zake kubwa zilikuwa kuja kucheza soka ndani ya Manchester United.
Alijua sio kazi rahisi kufanikisha hilo, lakini aliamini kwenye suala la kujituma kungeweza kumfanya awindwe na klabu yoyote duniani.
Mchezaji huyo alikuwa kwenye kiwango kizuri kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka jana huku England ikifanikiwa kufika hadi hatua ya nusu fainali na baadae kuwania nafasi ya tatu lakini ilijikuta ikiishia nafasi ya nne.
Baada ya hapo Manchester United wakaanza kuingia vitani kuwania saini ya beki huyo, hivyo ikiwa ni sehemu moja wapo ya kutimiza ndoto zake.
Suala la pili lilikuwa kuweka rekodi ya uhamisi wake. Pauni milioni 80 haijawai kutoka kwa beki yeyote kuwekewa mezani kiasi hicho kikubwa cha fedha, hivyo aliona bora aingie kwenye historia ya kipekee duniani kuwa beki wa kwanza kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Mbali na kusajiliwa kwa fedha hizo, lakini mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City walikuja na ofa ya pauni 278,000 kwa wiki ambazo ni zaidi ya milioni 771 kwa wiki, lakini Maguire alikataa na kutaka kutimiza ndoto za kucheza Manchester United.
Hivyo kilichompeleka Manchester United sio fedha, ila ni kutimiza ndoto zake, kama ni fedha angeenda Man City ambapo angekuwa anachukua kiasi kikubwa cha fedha kuliko anachochukua sasa Man United.
Oscar dos Santos
Alikuwa mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa kwenye kiwango kizuri wakati anakipiga katika klabu ya Chelsea kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 alipoondoka na kujiunga na klabu ya Shanghai SIPG inayoshiriki Ligi Kuu nchini China.
Maamuzi ya mchezaji huyo kujiunga na Shanghai SIPG yaliwashangaza wengi hasa kutokana na umri wake kuwa na miaka 25 wakati huo.
Huo ni umri ambao wachezaji wengi wanalitangaza jina katika klabu kubwa mbalimbali kutokana na ubora wao, Oscar alikuwa na ubora husiopingika ndani ya Chelsea kutokana na kuitawala safu yake ya kiungo.
Wachezaji wengi wanataka kuonekana duniani, soka ambalo linaongozwa kutazamwa kwa kiasi kikubwa duniani ni Ligi ya England pamoja na Hispania, lakini ofa ambayo iliwekwa na Shanghai SIPG, Oscar hakufikiria suala la kuonekana tena.
Shanghai SIPG waliweka mezani kiasi cha pauni milioni 60, pamoja na kitita cha pauni 400,000 kwa wiki baada ya makato ya kodi ambapo ni zaidi ya bilioni 1 za Kitanzania.
Wakati awali alikuwa anachukua kiasi cha pauni 90,000 kwa wiki zaidi ya milioni 249 za Kitanzania, hivyo alikuwa na kila sababu ya kuondoka.
Hii ilionesha wazi kuwa, ndoto za mchezaji huyo ni kuingiza fedha kwenye mchezo wa soka na sio kuangalia anakwenda kucheza soka kwenye klabu gani.
Tangu amekimbilia China, jina lake limeshuka kwenye ramani ya wachezaji wanaotikisa soka duniani tofauti na wengi walivyotarajia makubwa kutoka kwa mchezaji huyo, hata kwenye kikosi cha timu ya taifa Brazil haonekani kwa kuwa yupo kwenye ligi ambayo haina ubora mkubwa.
Kwa kuwa ndoto zake zilikuwa ni kuwa tajiri kwa kuingiza fedha nyingi bila ya kuangalia anacheza kwenye timu gani au ligi gani, ndoto hizo amefanikiwa, bado anaingiza fedha kila wiki zaidi ya bilioni 1.