25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Ruvu Shooting tegemea kasi mwanzo mwisho

Winfrida Mtoi

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019-20, umepangwa kuanza Agosti 24 ukishirikisha timu 20.

Timu zinazotarajia kushiriki patashika hiyo, zimejichimbia mbalimbali nchini, zikiendelea na maandalizi.

Msimu ujao wa ligi hiyo, unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, zikipigania kutwaa  ubingwa na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Ruvu Shooting yenye maskani yake mkoani, Pwani, ni miongoni mwa timu hizo, ikitarajia kufungua dimba na Yanga, mchezo utakaopigwa Agosti 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Je kikosi hicho ambacho kina msemaji  mwenye maneno mengi siku zote, Masau Bwire, kimejiandaaje?

Maandalizi

Katibu Mkuu wa Ruvu Shooting, Seleman Maoa, anaeleza jinsi maandalizi ya kikosi hicho, yanavyoendelea na kuweka bayana kuwa kila kitu kinakwenda sawa hadi sasa.

Anasema wamekuwa wakikiangalia kikosi hicho kwa ukaribu kwa sababu wanataka kuingia katika ligi wakiwa na kasi zaidi tofauti na msimu uliopita.

Maoa  anafafanua kuwa, kutokana na usajili walioufanya, wanaamini timu yao itakuwa moto mwanzo hadi mwisho na hakutakuwa na hali ya  kuchoka katikati ya safari.

“Tutakuwa na timu nzuri msimu huu,  tunaingia  kushindana, jambo zuri tupo katika ligi kwa muda mrefu, tunajua ni changamoto gani tunatakiwa kuzitatua na tumefanya hivyo.

“Ukiondoa usajili tuliofanya, pia tumechukua kocha mwenye uzoefu wa muda mrefu ambaye ni Salum Mayanga, atashirikiana na viongozi wengine wa benchi la ufundi,” anasema.

Anasema  wanafanya maandalizi mazuri kwa kuwa, moja kati ya malengo yao ni kumaliza katika nne za juu, ili kupata  nafasi  ya kushiriki michuano ya kimataifa kama ilivyofanikiwa KMC.

Usajili

Ruvu Shooting imesajili wachezaji 28, watakaotumika  msimu ujao, huku wakimrejesha mkali wao wa mabao Abdulrahman Mussa.

Mussa  aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/2017,  akiwa na kikosi hicho, akifunga mabao 14 sawa na Simon Msuva, lakini msimu uliopita  alichezea JKT Tanzania.

Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa na Ruvu Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa ni kipa Mohammed Makaka kutoka Stand United, Edward Christopher, Eladius Mfulebe (Kagera Sugar) na Kassim Mohammed, African Lyon.

Wengine ni Jamal Mnyate(Lipuli FC), Meshack Abel(Biashara United), Rajab Zahir(Singida United) Saddat Mohamed(Newala), Ismail Mgunda (Afrika Kusini) na Rajab Adam, Dar City.

 Kambi ya timu

Timu hiyo ilianza kambi rasmi mwanzoni mwa mwezi huu katika makao yake eneo la Mlandizi na kucheza mechi za kirafiki kadhaa.

“Wachezaji wote wapo kambini, mwalimu anafanya program zake inavyotakiwa na sisi kama uongozi tunahakikisha kila kinachohitajika kinapatikana, licha ya kwamba mambo ya kifedha bado ni changamoto,” anasema.

Mechi za kirafiki

Kabla ya kuingia katika mikiki ya Ligi Kuu , Ruvu Shooting imenoa makali yake kwa kucheza mechi tano za kirafiki, ilianza kuivaa Kombaini ya Jeshi na kuchapwa 2-1.

Mechi  ya pili ilikutana na  Dar City na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, kisha ikakabiliana na Azam na kutoka  suluhu, kisha  Polisi Kombaini na kushinda 2-0.

Kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya mwisho ya kirafiki Agosti 20, mwaka huu dhidi ya Namungo FC, utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ukarabati wa uwanja

 Ruvu Shooting imekuwa ikitumia uwanja wake unaofahamika Mabatini.

Jina hilo lilitokana na uwepo wa uzio wa mabati katika uwanja huo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, klabu hiyo imeondoka uzio huo na kuanza ujenzi wa mwingine  unaokidhi viwango.

Hayo yote yanafanyika ili kukidhi matakwa ya kanuni za Shirikisho la Soka Afrika(Caf).

Caf inataka timu inayoshiriki Ligi Kuu kuwa na uwanja wenye viwango.

“Tumeanza kujenga uzio mpya wa uwanja wetu na kurekebisha vitu mbalimbali, kwa sababu tuliambiwa uwanja wa mabati msimu huu hautatumika.

“Hatuhitaji kuongeza gharama nyingine za kwenda katika viwanja nje ya nyumbani kwetu, tumeanza ujenzi na ni matumaini yetu utakuwa umekamilika hadi kuanza kwa ligi,” anasema Maoa.

Timu hiyo msimu uliopita, ikiwa chini ya kocha Abdulmutik Haji, ilimaliza katika nafasi ya 15,  kati ya 20 zilizoshiriki, ikikusanya pointi 45, kupitia michezo 38, iliyoshuka dimbani, ikishinda 11, sare 12 na kupoteza mechi 16.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles