23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Hayatou amrithi Blatter Fifa

1162604_full-prtZURICH, USWISI

RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou, ameteuliwa kuongoza Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa muda baada ya rais wa sasa, Sepp Blatter,kusimamishwa kazi.

Hayatou raia wa Cameroon, amefungua historia mpya barani Afrika kwa kiongozi wa soka barani humu kupata nafasi ya juu kuongoza shirikisho hilo.

Blatter alisimamishwa kazi juzi usiku na Kamati ya Maadili ya Fifa kwa siku 90 (miezi mitatu) sambamba na Katibu Mkuu, Jerome Valcke na Makamu wa Rais, Michel Platini, ambaye ni Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UEFA), wakihusishwa na ufisadi ndani ya Shirikisho hilo na sasa wanachunguzwa.

Mwingine aliyekumbana na rungu hilo ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Fifa, Chung Mongjoon, ambaye ni mfanyabiashara na mwanasiasa wa Korea Kusini, amefungiwa miaka sita kutojihusisha na soka na kutozwa
faini ya Faranga za Uswisi 100,000 (pauni 67,000).

Watatu hao wamepigwa marufuku kushiriki katika michezo yoyote ya soka kwa kipindi hicho, lakini wamekana madai ya kufanya uovu wowote, ambapo Blatter alianza kuchunguzwa baada ya Jaji Mkuu wa Uswizi kufungua
mashtaka dhidi ya rais huyo mwenye umri wa miaka 79.

Blatter anatuhumiwa kwa kutia saini kandarasi isiyokuwa na umuhimu wowote kwa Fifa, mbali na kutoa malipo kwa rais wa UEFA, Michel Platini kinyume na matakwa ya Fifa. Kamati hiyo pia ilianzisha uchunguzi dhidi ya Platini kuhusu malipo hayo ya Euro milioni 2 ambayo yalifanywa miaka minane baada ya Platini kumfanyia kazi Blatter.

Valcke tayari alikuwa likizo kufuatia taarifa iliyoandikwa katika gazeti moja kwamba anahusika na kashfa ya kutaka
kujinufaisha na tiketi za Kombe la Dunia.

Hayatou, aliyeongoza CAF tangu 1988, anachukua nafasi hiyo kwa mujibu wa kanuni ya Fifa, inayoeleza kuwa kama
ikitokea rais amesimamishwa basi nafasi yake itachukuliwa na Makamu wa Rais wa Fifa aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi ndani ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo.

Mara baada ya kupewa mikoba hiyo, Hayatou alitoa taarifa na kusema kuwa amepokea vema majukumu hayo mapya.
“Rais mpya atachaguliwa kwenye Mkutano Mkuu Februari 26, 2016. Na mimi mwenyewe sitawania,” amesema kupitia taarifa hiyo.

“Hadi mkutano huo ufanyike, naahidi kwamba nitajitolea kwa nguvu zangu zote kutumikia shirikisho hili, mashirikisho wanachama, waajiri wetu, washirika na mashabiki wa soka popote walipo,” alisema.

Bosi huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na watawala na kuendeleza uchunguzi kwenye shirikisho hilo lililoyumbishwa na madai ya ulaji rushwa.

Hili litakuwa ni pigo kubwa kwa Platini na Chung Mongjoon katika mbio zao za kurithi mikoba ya Blatter kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Fifa, Februari 26, mwakani, hasa kutokana na kashfa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles