25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HATUTARAJII BAJETI HII YATOKEE YALE YALE

JUZI Serikali iliwasilisha makadirio ya Mapato  na Matumizi ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 ya Sh trilioni 31.7, ambayo pamoja na mambo mengine, imeonekana kuleta nafuu kwa upande fulani  na maumivu kwa upande mwingine.

Baadhi ya werevu wa masuala ya uchumi  wanaona kuwa katika bajeti hii ya sasa iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango, Dk. Philip Mpango, ina tofauti kwa kiasi fulani na ile iliyowasilishwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, kwa maana imetanua wigo wa ukusanyaji wa kodi.

Katika hilo, wanasema bajeti ya sasa pamoja na kuainisha vyanzo vipya vichache, ni rahisi kuonekana inaleta maumivu ya taratibu kuliko yale ya haraka tuliyoyazoea siku za nyuma.

Eneo mojawapo ambalo wameliangalia ni hatua ya serikali kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari (road licence).

Katika eneo hilo wanasema licha ya wengine kuona bajeti hiyo itajibu kero au kutatua matatizo ya wananchi, lakini wanaona kuwa hatua ya kuongeza Sh 40 kwa lita ya mafuta ya petroli, dizeli na taa inaweza kusababisha gharama za usafiri kupanda na hivyo hali ya uchumi kwa ujumla kutokuwa rafiki.

Pamoja na maoni hayo, kwa upande mwingine sisi tunaona kwa kiasi fulani bajeti ya sasa imeakisi kile tulichokiandika mwaka jana kupitia ukurasa huu kwamba bajeti ile ilipaswa kuteleza ahadi zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli wakati wa kampeni zake za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa ya viwanda.

Tunakumbuka vyema tulishauri kuwa huwezi kuzungumzia masuala ya viwanda pasipo kuwa na maandalizi maalumu kuhusu suala hili.

Kwamba sekta ya viwanda haiwezi kuendeshwa na Serikali peke yake, ushiriki wa sekta binafsi unapaswa kuwa mkubwa na uliowekwa wazi.

Hilo tumeliona sasa, hasa ukizingatia uamuzi wa serikali wa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza  gharama za ununuzi, uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.  

Pamoja na hatua hiyo, tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa upande wa serikali kuhakikisha uamuzi huu unaleta tija, kwa maana ya bajeti hii  inakwenda sambamba na Mpango wa Taifa wa  Maendeleo na vipaumbele vyake, ukiwamo ukuzaji wa uchumi wa viwanda ili utekelezaji wake ulete tija kwa wananchi.

Si hilo tu, tumeona katika bajeti ya sasa maumivu ya kodi yakiwaelekea wachimbaji wadogo wa madini ambao sasa wataanza kutozwa Kodi ya Zuio kwa asilimia 5 kwenye bei ya kuuzia (Total Market Value)  ambayo itakuwa kodi ya zuio ya mwisho  (Final Withholding Tax).

Pamoja na uamuzi huo, mwaka jana tulishauri juu ya  kiwango kikubwa cha msamaha wa kodi kwenye sekta ya madini ambayo ni asilimia 75, tulidhani hili lingeguswa, lakini imekuwa ni tofauti kidogo, pengine Rais Dk. John Magufuli atakapomaliza kupokea ripoti za wataalamu wa masuala ya serikali wanaounda kamati ya kumshauri katika sekta ya madini anaweza kulitazama hili.

Pamoja na hayo yote, tumeona katika bajeti iliyopita fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo ni ndogo mno, tofauti na matarajio, na hii kwa kiasi kikubwa imevunja matumaini, ni vyema wasaidizi wa Rais Dk. Magufuli wakaendelea kukuna vichwa kuona jinsi ambavyo bajeti hii inaweza kutekelezeka kwa vitendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles