31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

USIOGOPE, KUJARIBU HAKUNA MWISHO

Na ATHUMANI MOHAMED

SIYO ajabu kusikia watu wakilalamika wana maisha magumu, mambo hayaendi. Kifupi ni malalamiko juu ya malalamiko kuhusu namna gani mtu anaweza kufanikiwa kwenye jambo fulani.

Hiyo ipo kwenye biashara, maendeleo nk, katika maisha yetu ya kila siku. Watu wanataka kufanikiwa lakini wanaishia kulalamika tu.

Ukifuatilia kwa makini utagundua kuwa tatizo kubwa hapo ni kujaribu. Watu ni waoga wa kujaribu. Wanapenda mafanikio lakini wanaogopa kuthubutu.

Ndugu zangu ikiwa tunataka kufanikiwa, lazima tujipe nafasi ya kujaribu mara kwa mara. Ukikataa kujaribu ni vigumu kujua ugumu au urahisi wa jambo unalotamani kulifikia.

 

UNAJARIBU KITU GANI?

Tunapozungumzia kuhusu kujaribu, haina maana kwamba kila kitu unatakiwa kujaribu. Angalia kwanza ni kitu gani unachotaka kujaribu. Labda ni biashara, si vizuri sana kuiga biashara za wenzako.

Haina maana kwamba kwa sababu Juma Athumani anapata faida kubwa kwenye biashara yake ya kutengeneza na kuuza mikate, basi na wewe utafanikiwa, la hasha!

 

NINI KIU YAKO?

Angalia ndani yako. Unadhani nini biashara ya ndoto zako? Unaipenda biashara husika? Mfano, inawezekana biashara ya bucha la nyama ya ng’ombe ina faida, lakini ndani yako hupendi kushika nyama mbichi na pengine unahisi vibaya, ikiwa ndivyo hutaweza kufanya biashara husika kwa ufanisi.

Fikiria kujaribu angalau kitu ambacho kipo ndani ya moyo wako, inaweza kukupa mafanikio kwa hakika zaidi kuliko kufanya kwa kujilazimisha. Hiyo humaanisha kuwa, kabla hata hujafanya jaribio lako, tayari utakuwa umeshafeli.

 

PATA UZOEFU KWA WALIOKUTANGULIA

Utaweza kupata mbinu mpya kwa kupitia watu waliofanikiwa kwenye kitu kinachokusumbua kwa muda mrefu. Labda ni biashara au mipango fulani ya mafanikio.

Mfano, ulikuwa na nia ya kujenga nyumba kwa muda mrefu, lakini unaogopa, unahisi labda ni fedha nyingi sana. Fuatilia wenzako waliofanikiwa hilo, wamewezaje?

Acha kusikiliza watu wanaojaribu kukukatisha tamaa. Kuna watu wa vipato vya kawaida kabisa, lakini wamejenga. Fanya utafiti, wamewezaje? Wametumia mbinu gani?

Usiogope ukubwa wa samaki, uliza bei! Mfano, sehemu nyingi bado kuna watu wanauza sehemu ya viwanja vyao kwa bei ndogo, tena unalipa kwa awamu.

Usiishie kuamini maneno ya kutishwa, kwamba labda ujenzi ni gharama. Huwezi kujenga kabla ya kuwa na kiwanja. Anzia hapo. Fika sehemu za madalali na uanze kuuliza bei.

Lakini ukiachana na hilo, kuna suala la biashara. Mfano unataka kufanya biashara ya kuuza mazao, watu wanakutisha kuwa mtaji unatakiwa mkubwa, puuza. Chunguza peke yako.

Ukijipa muda, utashangaa kumbe kwa muda mrefu ulikuwa unaogopa tu bure kujaribu, maana ni biashara nzuri ambayo inaweza kubadili maisha yako. Utajuaje bila kujaribu?

 

PIMA USHAURI

Kama umeamua kuomba ushauri wa moja kwa moja kwa watu au mtu wako wa karibu, penda kuwa na tabia ya kuchuja ushauri. Sikiliza yote, lakini chuja ulichokisikia.

Binadamu hatufanani, mwingine anaweza kukuchekea usoni, lakini moyoni anatamani kuona ukishindwa kila kitu kwenye maisha yako.

Baada ya kupata maarifa hayo tena kwa kujiridhisha kabisa, jipe muda wa kuyafikia malengo yako. Haina maana kwa kujua kwako namna ya kufanya leo, basi kesho uanze jambo hilo.

Maisha ni mipango, kumbuka hakuna mafanikio utakayoweza kuyapata kwa usiku mmoja, jipange. Kama ni fedha inahitajika, anza kukusanya na kuhifadhi.

Ukiamua kuingia kwenye utekelezaji wa jambo husika, uwe tayari una hakika na unachokwenda kufanya. Usiogope kujaribu katika maisha yako. Jaribu kila siku mpaka ufikie ndoto zako. Kumbuka kujaribu hakuna mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles