Hatma dhamana ya mwandishi anayedaiwa kuandika uongo Sept. 23

0
633

Francis Godwin -Iringa  

UAMUZI wa kupata ama kukosa dhamana kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa, Sebastian Atilio utajulikana Septemba 23.

Mwanahabari huyo ambaye anakabiliwa na kesi ya jinai, akituhumiwa kwa makosa mawili; kufanya kazi ya uandishi bila kusajiliwa na bodi na kuandika habari za uongo kuhusu wananchi wa Kijiji cha Ifupila, Mufindi, alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi juzi.

Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Victor Kitomari aliiomba mahakama hiyo kusogeza mbele siku ya kusikilizwa kwa mapingamizi ya dhamana na kutoa uamuzi kwa kuwa hajajiandaa. 

Naye wakili wa utetezi, Emmanuel Chengula aliiambia mahakama kuwa hoja ya Kitomari si sahihi kwani pingamizi la dhamana walipokea Septemba 11 na wao kulijibu Septemba 13, mwaka huu, hivyo alikuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa kwa kusikilizwa kesi hiyo.

Chengula alidai kuwa sababu za mwendesha mashtaka huyo wa Jamhuri kutaka kujibu kiapo kinzani ambacho hakijasikilizwa si sawa na kwamba kuna mapingamizi manne ya kisheria ambayo bado hayajasikilizwa. 

Kutokana na hilo, aliiomba mahakama kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka kwani yanalenga kumtesa mteja wake kuendelea kusota mahabusu wakati kesi yake ya msingi ina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, akiahirisha kesi hiyo, Hakimu  Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Edward Uforo, alisema hoja zote za pande mbili ni za msingi, lakini katika suala hilo busara ya pande zote na mahakama inapaswa kuhusika. 

“Hivyo naomba tupange siku nyingine ya kusikiliza hoja kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili na tupange siku ambayo haitakuwa mbali maana mtuhumiwa yupo mahabusu na kesi yake ya msingi ina  dhamana,” alisema.

Kutokana na hilo, mahakama  hiyo itatoa uamuzi mdogo baada ya kusikiliza mapingamizi yaliyowekwa dhidi ya shauri la kupinga dhamana Septemba 23, ambayo itakuwa ni siku ya kutajwa kwa kesi ya msingi.

Mwanahabari huyo amerudishwa mahabusu ya gereza la Isupilo Mufindi hadi Septemba 23 shauri hilo, litakapofikishwa tena mahakamani hapo kujua hatima ya dhamana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here