Wanawake Nkasi wapongezwa kufuata uzazi salama

0
731

Gurian Adolf -Nkasi

WAJUMBE wa kikao cha kufanya tathimini ya utekelezaji mpango kazi wa mwaka 2018 ya mradi wa kukabiliana na mimba za utotoni wilayani Nkasi, wamepongeza hatua ya wanawake kubadilika wilayani humo kwa kujifungulia katika vituo vya vya afya.

Akichangia katika kikao hicho cha siku moja cha nusu mwaka cha timu za ulinzi wa mtoto ngazi ya kata na wilaya hiyo kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Afya cha Mtakatifu Bakita, Marietha Mwanisenga alisema hivi sasa wanawake wengi wanahudhuria kliniki kutokana na elimu inayotolewa na mradi huo unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Plan International.

Alisema awali kabla ya mradi huo, wanawake wanne kati ya kumi ndio walikuwa wanaona umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vinavyotoa huduma za uzazi salama.

Marietha alisema hivi sasa wanawake zaidi ya asilimia 90 ambako mradi huo unatekelezwa kumekuwa na mabadiliko kwani wamekuwa wakihudhuria kliniki kutokana na elimu iliyotolewa.

George Kayanda alisema mradi huo umesaidia kuleta mabadiliko chanya katika masuala ya uzazi, lakini changamoto kubwa ni mimba za utotoni ambazo zimekuwa zinaonekana kudumaza jitihada za mradi huo.

Alisema tatizo ni wazazi wenyewe kutokubali kubadilika na kuelewana na watu wanaowapa mimba watoto wao nje ya sheria.

Kayanda alisema hali hiyo imekuwa ni kikwazo hata kwa vyombo vya sheria kwani hata kama walimu wakizifikisha kesi hizo mahakamani wamekuwa wakiwatorosha watoto waliopata ujauzito.

Mratibu wa mradi huo, Nestory Frank alisema lengo la kufanyika kikao hicho, ni kujitathmini ili kubaini changamoto zilizopo katika kutekeleza mikakati waliyojiwekea mradi huo uweze kufanikiwa.

Alisema suala la kuchukua hatua kwa watoto waliopata mimba linahitaji mikakati zaidi kwani licha ya kuwa wao wamekuwa wakiitoa, lakini linahusu zaidi undugu na mahusiano kwani wengi wao wamekuwa wakimalizana nje ya sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here