31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Halima Mdee aachiwa kwa dhamana 

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM       

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliyekuwa ameshikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa mahojiano, ameachiwa kwa dhamana.

Mdee, ambaye pia ni MwenyekitiwaBaraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha), juzi aliitwa kwa mahojiano katika kituo hicho cha polisi na baadaye kuwekwa mahabusu.

Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliliambia MTANZANIA kuwa jeshi hilo limekuwa likimtafuta mbunge huyo kwa kosa la kufanya mkutano usio na kibali.

Jana Katibu wa Chadema Jimbo la Kawe, Dorcas Francis, alitoa taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa Mdee ameachiwa huru kwa dhamana.

“Uongozi mzima Jimbo la Kawe tunatoa shukrani kwa wote kwa ushirikiano wenu wa dhati, mbarikiwe sana. Tuendelee kushirikiana,” aliandika katibu huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema Mdee amedhaminiwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest na Wakili Hekima Mwasitu.

Mrema alisema kesho Jumanne, Mdee ataripoti tena katika kituo hicho cha polisi.

Kuhojiwa kwa Mdee kumekuja ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Chadema itangaze azma yake ya kuandaa ratiba ya kufanya mikutano ‘mchana kweupe’.

Kutokana na hatua hiyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake, Ahmed Msangi, liliitaka Chadema kufuata utaratibu.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili juzi, Kamanda Mambosasa alisema Mdee alipoomba kibali ya kufanya mkutano alielekezwa asifanye kwa sababu kulikuwa hakuna askari wa kulinda mikutano yake, lakini yeye alikaidi.

 Alipohojiwa iwapo Mdee alikamatwa au aliitikia wito wa jeshi hilo kama ambavyo aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, Kamanda Mambosasa alisema mbunge huyo alikuwa akitafutwa na si kuitwa.

“Alikuwa anatafutwa, kama amejipeleka sijui, lakini alikuwa anatafutwa si kuitwa,” alisema Kamanda Mambosasa.

Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa Mdee kuachiwa kwa simu juzi, Kamanda Mambosasa alijibu kuwa bado alikuwa anashikiliwa.

“Kwahiyo ndiyo hivyo bado ameshikiliwa,” alisema Kamanda Mambosasa.

Kwa upande wa Chadema, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, juzi alisema Mdee alihojiwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi kwenye moja ya mikutano yake ya hadhara aliyofanya Jimbo la Kawe, ikiwa ni mwendelezo wa ratiba ya ziara za kuwatembelea, kuwasikiliza na kuwapatia mrejesho wapigakura wake jimboni humo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles