27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Kimeta chaua watano, ng’ombe 21 Kilimanjaro

UPENDO MOSHA-ROMBO

WATU watano na ng’ombe 21 wamekufa kwa ugonjwa hatari wa kimeta ulioibuka wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Kutokana na hali hiyo, serikali imetoa maagizo kwa maofisa afya, kilimo na mifugo kuchukua tahadhari kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo.

Akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo jana katika kikao kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Shauritanga, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, alisema kutokana na kuibuka kwa ugonjwa huo hatari, wataalamu wa afya waelimishe jamii juu ya athari za ugonjwa huo.

“Nina taarifa za kuibuka kwa ugonjwa huu hatari, nategemea wataalamu wetu watafanya kazi ya ziada katika kudhibiti usienee zaidi,” alisema Majaliwa.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alishangazwa na wilaya hiyo kuwa na zaidi ya aina 50 ya pombe za kienyeji ambazo zimechangia kuathiri nguvu kazi kwa wananchi.

“Ni jambo la ajabu kwamba mna aina nyingi za pombe na mbaya zaidi naelezwa kwamba polisi wanasaidia katika kuwalinda wapishi na wauzaji wa gongo.

“Naomba Kamanda wa Polisi Mkoa kulishughulikia hilo ili kulikomesha, nadhani Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ana jambo la kufanya.

“Maagizo haya yaende sambamba na Baraza la Madiwani la Halmashauri hii kupitisha fedha kwa ajili ya miradi ya maegesho ya malori na mabasi Kituo cha Holili, kinachohitaji Sh milioni 48 ili kiweze kuwa moja ya vyanzo vya mapato vya halmashauri,” alisema.

Majaliwa alilitaka Baraza la Madiwani kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Holili, ambalo halijakamilika kwa takribani miaka 30 na kwamba kinyume cha hapo, wamthibitishie kwamba hawahitaji mapato.

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Magreth John, alisema halmashauri inakusanya zaidi ya Sh bilioni 1.6 na kwamba watahakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ambayo imekwama.

“Kuhusu hii miradi, mara kadhaa nimeandaa bajeti, lakini madiwani wanazikataa, kwa hiyo nashindwa kuitekeleza, lakini katika bajeti ya mwaka huu nimeiweka na tutaitekeleza Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema Magreth.

Kwa upande wake Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alimuomba Waziri Mkuu kumsaidia Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili aweze kuacha jeuri pamoja na kuwa na uhusiano mzuri na watumishi wengine, wakiwamo wakuu wa idara.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,451FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles