28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Giza nene kifo cha mwimbaji Kizito Mihigo

KIGALI, RWANDA

SIKU mbili baada ya Jeshi la Polisi nchini Rwanda kutangaza kujiua kwa msanii maarufu wa nyimbo za injili, Kizito Mihigo(38), suala hilo sasa ni kama limeibua sura mpya.

Hatua hiyo inakuja baada ya Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, linalotaka uchunguzi ufanywe kubaini chanzo cha kifo cha mwanamuziki huyo.

Mkurugenzi wa HRW, Kanda ya Afrika ya Kati, Lewis Mudge, anasema shirika hilo linatilia shaka mazingira ya kifo chake na kwamba linataka uchunguzi huru ufanyike.

Mudge anasema kuwa Kizito Mihigo alikuwa mwakilisha wa watu wanaojaribu kushinikiza mabadiliko nchini Rwanda miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari.

“Hii sio mara ya kwanza watu kufariki wakiwa kizuizini au kuuawa katika mazingira ya kutatanisha au kutoweka,” anasema Mudge.

Anaongeza kuwa mwaka 2018 mwanasiasa maarufu wa upinzani alitoweka akiwa jela na kwamba mamlaka ya jela wakati huo zilisema mwanasiasa huyo alikuwa akijaribu kutoroka lakini tangu wakati huo hajawahi kupatikana, hatua ambayo imekuwa ikiibua hali ya wasiwasi.

Wakati HRW ikishinikiza hivyo, mamlaka nchini Rwanda zinasema msanii huyo alijiua alipokuwa anazuiliwa mahabusu katika kituo cha polisi. Itakumbukwa kuwa Mihigo alikuwa anazuiliwa kwa madai ya kujaribu kuvuka mpaka kiharamu kungia nchini Burundi.

Lakini, katikati mwa wiki iliyoisha polisi nchini Rwanda walitangaza kuwa msanii huyo maarufu wa nyimbo za injili, ‘amejinyonga.’

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mwili wa msanii huyo ulipatikana katika chumba alimokuwa anazuiliwa kwenye kituo cha polisi mtaa wa Remera, Mjini Kigali nchini Rwanda.

Taarifa ya polisi inasema kwamba amejinyonga siku tatu baada ya kukamatwa karibu na mpaka baina ya Rwanda na Burundi katika kile ambacho polisi ilisema alikuwa na nia ya kutoroka nchi na kujiunga na makundi ya waasi dhidi ya Rwanda.

Wachunguzi nchini Rwanda wanasema tayari uchunguzi juu ya kifo chake umeanzishwa.

Polisi wanasema Kizito alijitoa uhai katika kisa kilichowashangaza mashabiki wake wengi na raia wa Rwanda.

“Tayari uchunguzi umeanzishwa, mwili wake umepelekwa katika chumba cha karibu cha kuhifadhi maiti. Alikuwa katika kituo cha wachunguzi cha Rwanda katika eneo la Remera Mji Mkuu wa Kigali, ambako alikutwa akiwa amejinyonga ndani ya selo yake mapema alfajiri. Alitumia nguo aliyokuwa anatumia kulalia kujinyonga,” ilisema taarifa ya polisi.

Hata hivyo, wanaharakati wanaoishi ughaibuni wamekuwa wakipinga taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi nchini humo kuhusu kifo chake.

Raia hao wanasema mwanamuziki huyo hakutaka kujiunga na kundi la waasi nchini Burundi kama ambavyo taarifa zimekuwa zikienezwa nchini humo bali alitaka kwenda Ubelgiji alikokuwa akiishi.

Lakini mbali na hilo, wanaamini kwamba hakujiua katika kituo cha polisi alipokuwa anazuiliwa na kwamba huenda aliuawa nje ya eneo hilo kwa kuwa amekuwa akienda kinyume na serikali.

Taarifa kutoka nchini Rwanda zinatanabaisha kuwa, muziki wa Kizito ndio chanzo cha matatizo yaliyomkumba, kwani katika wimbo mmoja alipendekeza kwamba kila mtu aliyeuawa katika mauaji ya kimbari 1994 anapaswa kukumbukwa bila kujali ni Mtutsi ama Muhutu.

Wanasema mamlaka nchini humo imeliona hilo kama changamoto ya wazi dhidi yake na kwamba mauaji hayo yalitekelezwa na Watutsi.

Wakati hali ikiwa hivyo, wakosoaji wa serikali wanaamini Kizito alilengwa moja kwa moja.

Mwanamuziki huyo alikuwa ameanza kuchunguzwa kuhusiana na madai hayo pamoja na kutaka kuwahonga wananchi waliomkataa.

Mwaka uliopita, aliachiwa huru kwa msamaha wa Rais Paul Kagame, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa hatia ya kutaka kumuua rais na kuhamasisha raia kupinga Serikali.

Kumekuwapo hisia tofauti katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha ghafla cha msanii huyo wa muziki wa injili huku baadhi ya watu wakitaka majibu kutoka serikalini.

Kizito alipata umaarufu kutokana na nyimbo zake kama vile ‘Inuma’ unaomaanisha njiwa na ‘Igisobanuri cy’urupfu’ unaoelezea kifo ni nini.

Februari 14, mwaka huu, Idara ya upelelezi ya Rwanda ilisema inamshikilia mwanamuziki Kizito Mihigo baada ya kufikishwa kwenye idara hiyo na polisi Februari 13 .

Kwenye ukurasa wa Twitter idara hiyo ya uchunguzi ilisema kuwa Kizito alikuwa akishutumiwa kujaribu kuvuka mpaka kwenda Burundi kinyume cha sheria kwa lengo la kujiunga na makundi ya wanamgambo wanaoipinga serikali ya Rwanda. Pia anashutumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Awali, mwanamuziki huyo alidaiwa kutoweka kabla ya kuzuiwa na wananchi Kusini Magharibi akidaiwa kujaribu kuvuka mpaka kuingia Burundi.

Mwanamume mmoja katika eneo la Nyaruguru ambaye alimuona mwanamuziki huyo kabla ya umauti kumfika, anasema alionekana kama mtu aliyetoka kwenye safari ndefu akiwa na begi zito huku akiambatana na wanaume wawili.

Picha za mwanamuziki huyo nyota zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii juzi jioni.

“Nilikuwa hapo nilimuona, wanakijiji waliomzuia walisema alikuwa akijaribu kuvuka mpaka kwenda Burundi kwa kutumia njia za panya, kutoka hapa hadi mpakani ni mwendo wa chini ya dakika tano,” alinukuliwa akisema shuhuda huyo.

Awali, Kizito na wanaume wawili walikuwa wakikabidhiwa kwa wanajeshi na polisi walioitwa na wanakijiji. Picha za mwanamuziki huyo na wanaume wengine wawili zinazoripotiwa kuchukuliwa na wanakijiji mahala alipokamatwa zilienea kwenye mitandao ya kijamii.

Polisi nchini Rwanda awali walisema kuwa hawakuwa na taarifa kuhusu kukamatwa kwa mwanamuziki huyo.

Hivyo, bado vyombo vya kimataifa vinaendelea kushinikiza juu ya uhalali wa kifo cha Kizito zikitaka kuwapo kwa taarifa ya uwazi kutoka ndani ya jeshi la polisi inayoelezea kinagaubaga kuhusu mazingira ya kifo chake.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles