25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Harakati zinazofanyika kumaliza mzozo Sudan Kusini

MWANDISHI WETU

TANGAZO la hivi karibuni la Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, kuhusu kupunguza majimbo nchini humo kutoka 32 hadi 10 ni tamko lililopokelewa kwa hisia tofauti ndani na nje ya taifa hilo.

Kiongozi wa upinzani ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani Dk. Riek Machar, amekaribisha tanganzo hilo la Kiir na kusema ni hatua muhimu katika mchakato wa kuleta amani ya kudumu katika taifa hilo changa duniani ambalo limezongwa na mapigano ya umwakigaji damu ya wenyewe kwa wenyewe.

Siku ya Jumamosi, akiwa Mji Mkuu wa Juba, Rais Kiir alitangaza kwamba Sudan Kusini, imerejea mfumo wa utawala wa zamani wa majimbo 10 na kuwafuta kazi magavana wote wa majimbo hayo.

Alisema hatua hiyo itatoa fursa ya kuundwa kwa serikali ya muungano na hatimaye kumaliza vita vya kikabila ambavyo vimekumba taifa hilo kwa miaka mingi.

Chimbuko mzozo wa majimbo

Tofauti kati ya Rais Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar kuhusu majimbo limekuwa suala nyeti katika mazungmzo ya kuleta amani Sudan Kusini. Hii ni kwa sababu mipaka ya majimbo ni kigezo muhimu katika kugawana madaraka wakati wa kuundwa kwa serikali ya muugano.

Wakati Sudan Kusini ilipojinyakulia uhuru mwaka wa 2011, taifa hilo lilikuwa na majimbo 10 kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Lakini badaye Rais Kiir aliongeza idadi ikawa majimbo 28 na kisha badaye 32, jambo ambalo lilipingwa vikali na upinzani.

Kiir pia alianzisha maeneo matatu ya utawala ya Pibor, Ruweng na Abyei.

Kiir alikuwa amekataa kata kupunguza idadi ya majimbo lakini kutokana na shinikizo za kimataifa, amesalimu amri.

Dk. Machar alikuwa ametishia kwamba hangerejelea wadhifa wake wa makamu wa rais katika serikali ya muungano inayotarajiwa kuundwa ikiwa idadi ya majimbo ingebakia 32.

Peter Manawa, Msemaji wa Dk. Machar amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema upinzani umepokea kwa furaha na matumaini makubwa, hatua ya Rais Kiir  kupunguza majimbo. Alisema ni uamuzi bora na ushindi kwa raia wote wa Sudan Kusini wanaongojea amani ya kudumu kwa hamu na ghamu.

Wasiwasi kuhusu maeneo mapya ya kiutawala

Ingawa tangazo la Rais Kiir la kupunguza idadi ya majimbo ni hatua ambayo imeshangiliwa na wengi, wadadisi wa mambo wanasema kuundwa kwa maeneo matatu ya kiutawala huenda kukawa kizungumkuti kwenye mazungumzo ya amani na maridhiano.

Upinzani umekataa kuundwa kwa maeneo hayo ya kiutawala. Maeneo hayo ya Pibor, Ruweng na Abeyi yameshuhudia mapigano makali ya kikabila wakati wa mzozo wa Sudan Kusini.

Kwa mfano, eneo la Ruweng ni kituo muhimu kinachozalisha mafuta kwa wingi nchini Sudan Kusini na huenda utata mpya ukazuka kuhusu umiliki wa eneo hili.

Mazungumzo tasa ya amani

Salva Kiir na Riek Machar wamekuwa wakishiriki katika mazungmzo ya kujaribu kuleta amani Sudan Kusini bila mafanikio.

Viongozi hao wawili walifikia makubaliano ya amani mwaka 2018 kutokana na shinikizo la mataifa ya kiafrika, Umoja wa Mataifa na nchi zenye ushawishi mkubwa duniani.

Katika maafikiano hayo, walikubaliana kuunda serikali ya umoja ifikiapo Mei 2019, lakini hilo halikufanyika kufuatia mizozo kuhusu mipaka na utaratibu wa kiusalama.

Makataa ya pili ya Novemba mwaka jana, ya kuunda serikali ya muungano pia yalipita bila mafanikio na kuahirishwa tena kwa siku 100, hali iliyosababisha Washington kumtoa balozi wake mjini Juba, pia kuwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wakuu wa serikali ya Sudan Kusini kuhusiana na mchango wao katika kupalilia mzozo kwenye taifa hilo.

Shinikizo la kimataifa

Rais Kiir na Machar wanakabiliwa na shinikizo la kimatifa kuafikiana kuhusu ugomvi wa madaraka na kuundwa kwa serikali ya muungano kabla makataa ya Febrauri 22, mwaka huu.

Marekani na mataifa mengine yenye ushawishi mkubwa yalionya kwamba itamuwekea vikwazo yeyote atakayeonekana kuwa kizuizi au kwenda kinyume na mchakato wa kupatikana kwa amani ya Sudan Kusini.

Papa Francis na kiongozi wa kanisa la Kianglikana duniani, askofu mkuu wa Canterbury Justin Welby, wanasema watatembelea taifa la Sudan Kusini punde tu serikali ya muungano itakapoundwa.

Wiki iliyopita, Marekani, Uingereza na Norway zilitoa wito kwa Rais Kiir na kiongozi wa upinzani Machar kuafikiana kuhusu muundo wa serikali ya muungano ili wajiepushe kurejea kwenye mzozo wa kivita.

Athari za vita

Mapigano ya umwagaji damu ya wenyewe kwa wnyewe yaliyonza miaka sita iliyopita nchini Sudan, yamesababisha vifo vya takribani watu 400,000 na kuwaacha mamilioni bila makwao katika taifa hilo changa duniani.

Uchumi umedhoofika na wengi wanaishi katika dimbwi la umaskini unaochochewa na njaa na kiangazi cha muda mrefu.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles