24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

GGML yazindua program ya kuwajengea uwezo Watanzania kupata zabuni

MWANDISHI WETU


Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Geita (GGML) kwa kushirikiana na Baraza la Kitaifa la Uchumi na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), imesaini makubaliano ya utekelezaji wa programu maalumu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara mkoani Geita kushiriki kikamilifu katika zabuni zinazotolewa na mgodi huo.


Makubaliano hayo yaliyotiwa saini Julai 20, mwaka huu mkoani Geita, yatadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Juni 30, mwaka 2021.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo na kuzindua program hiyo, Makamu Rais wa GGML, Simon Shayo alisema progamu hiyo pia inalenga kuwajengea uwezo wazabuni wa Mkoa wa Geita ili kuweza kutambua na kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa na huduma zinazohitajika katika shughuli za GGML.


Aliongeza kuwa program hiyo, pia inalenga kuwaunganisha wazabuni wa GGML na mamlaka mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla zinazotoa fursa zinazowezesha kushiriki kikamilifu katika zabuni hizo.


“Programu hii itawawezesha wazabuni wa GGML kupata soko la uhakika la bidhaa na huduma wanazozalisha hivyo kujiongezea kipato cha mtu mmoja mmoja, kipato cha kaya na jamii kwa ujumla hivyo kuchangia pato la Taifa kwa upande mmoja,” alisema.

Aidha, alisema GGML itaweza kupata huduma na bidhaa zenye ubora kutoka kwa wazabuni wa ndani zitakazoongeza tija kwa wazalishaji wa ndani.


“GGML tumejitolea katika maendeleo endelevu ya jamii inayotuzunguka. Tunapenda kuacha urithi, hata wakati madini yatakapokuwa yameisha kuchimbwa. Kusudi letu ni kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye shughuli za mgodi ili tuweze kusaidia jamii ambayo tunafanya nayo kazi. Tumekuwa tukionyesha haya huko Geita kwa kuwa washirika dhabiti na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii, elimu, afya na kilimo, “alisema Simon Shayo


Shayo alifafanua kuwa, GGML inajivunia kuwa walipa kodi bora na wakubwa nchini Tanzania ambapo mwaka 2019 pekee, jumla ya kodi iliyolipwa na GGML kwa serikali ya Tanzania ilikuwa takriban Sh bilioni 467 sambamba na kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 5000.

Akizungumza katika uzinduzi wa program hiyo, Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (sera, uratibu na uwekezaji), Dorothy Mwaluko alisema programu hiyo imetengenezwa wakati muafaka.


“Itahakikisha changamoto ambazo zinafanya kampuni za kitanzania kushindwa kupata zabuni kwenye uwekezaji unaofanyika nchini, zinatatuliwa na kumwezesha mwekezaji kutekeleza kikamilifu sheria za nchi kwa kununua bidhaa na kutumia huduma za watanzania zinazokidhi viwango.

“Nipende kuwapongeza Kampuni ya Uchimbaji wa Geita, GGML kwa kukubali kuwezesha programu hii kwa kuwa wafanyabiashara watakaonufaika na mafunzo haya mbali na kushiriki shughuli za uzalishaji katika mgodi huu, pia yatawafungulia njia kushiriki katika miradi inayotekelezwa kwenye sekta zingine,” alisema.


Aidha, Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa alisema uzinduzi wa programu hii unabebwa na kauli mbiu isemayo ‘‘Ushiriki na Ushindani wa Uwazi katika Kukuza Uchumi’’.

Alisema kauli mbiu hiyo inajielekeza katika kujenga uwezo kwa wafanyabiashara wa ndani ili wapate fursa ya kushiriki katika sekta ya madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles