25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

GGML waungana na Biteko kuanika mbinu za mapambano dhidi ya UKIMWI

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka wadau mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuhakikisha kuwa wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI nchini badala ya kutegemea wafadhili kwa kiasi kikubwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akihutubia viongozi mbalimbali wa serikali, watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI na wadau wa maendeleo ikiwamo Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika mkutano maalum wa wadau wanaoshughulikia udhibiti wa UKIMWI Tanzania uliofanyika jana mjini Morogoro.

Dk. Biteko amesema hayo Novemba 29, 2023 katika mkutano maalum wa wadau wanaoshughulikia udhibiti wa UKIMWI Tanzania uliofanyika mjini Morogoro na kuhusisha viongozi wa Serikali, watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na wadau wa maendeleo ikiwamo Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).

Amesema pamoja na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau, bado UKIMWI haujadhibitiwa inavyotakiwa, hali inayoweza kusababisha maambukizi mapya kuongezeka.

Aliwataka wadau wote wanaohusika kuendelea na juhudi za utoaji afua mbalimbali zenye lengo la kutokomeza ugonjwa wa UKIMWI.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI na nawataka TACAIDS na wadau kuhakikisha mnashirikiana kwa pamoja dhidi ya mapambano ya Ukimwi kwa kuongeza ushiriki wa wananchi pia,” amesisitiza Dk. Biteko

Aidha, akichangia mada katika mkutano huo, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dk. Kiva Mvungi aliunga mkono hoja hizo za Dk. Biteko na kusisitiza kuwa maeneo mengine ambayo Serikali inaweza kutumia na kupunguza utegemezi wa wafadhili ni kupitia kampuni kubwa zinazofanya shughuli zake hapa nchini.

“Kwa mfano GGML hushirikiana na TACAIDS kila mwaka kuandaa kampeni ya Kili Challenge ambayo  washiriki hupanda na kuuzunguka mlima Kilimanjaro na fedha zinazopatikana huelekezwa katika mfuko wa kudhibiti Ukimwi pamoja na kuwezesha afua na asasi zinazojishughulisha na masuala ya Ukimwi,” amesema.

Dk. Kiva alitaja mbinu nyingine ya kuondokana na utegemezi kutoka kwa wafadhili kuwa ni kushirikisha Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambacho kina wanachama mbalimbali wakiwamo makampuni makubwa ya madini na kampuni nyingine ambazo zitaweza kuchangia fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI.

“Kwa kutumia ATE tunaweza kushirikisha wafanyakazi wetu au kuwatia moyo wanachama  wa ATE wawe na mtazamo na kusaidia jamii na kufanya tathmini ya mahali ambapo mtu au kampuni husika inapofanya kazi. Kisha tunaingia kwenye jamii za kupima kama kweli huduma hizo muhimu za elimu ya afya zimetolewa,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Jerome Kamwela alisema mkutano huo unalenga kutoa nafasi ya mashaurinao kati ya Serikali na wadau wake katika mapambano dhini ya UKIMWI.

Alisema mkutano  huo ni muhimu hasa wakati huu ambao Tanzania inaelekea kufikia lengo la dunia la kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

“Lengo linataka kusiwe na maambukizi mapya ya UKIMWI, kusiwe na vifo vinavyotokana na UKIMWI pia, kusiwe na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles