Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ameonya baadhi ya watu wanaovunja sheria kwa kuvamia maeneo ya watu na ya umma katika kipindi cha chaguzi wakitegemea hawatochuliwa hatua na kuonewa huruma na watawala.
Waziri Silaa ametoa onyo hilo mkoani Tanga leo Desemba 1, 2023 alipofanya ziara ya kufuatilia maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro ya vijiji 975 nchini.
Aidha, amewataka viongozi na watumishi wa umma kusimamia sheria za umiliki wa ardhi bila kusita kwa watu wote wanaozalisha migogoro kwa kujiingiza kwenye maeneo ya watu na maeneo ya hifadhi kisa wataonewa huruma na viongozi sababu ni kipindi cha uchaguzi.
Amesema mwaka 2024 na 2025 ni miaka ya uchaguzi, hivyo wananchi wasijiingize kwenye uvamizi wa ardhi za watu kiholela kwa kutegemea huruma ya sheria jambo ambalo baadae husababisha migogoro.