25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

“Flow Meters” jipu linaloitesa serikali zaidi ya miaka nane

  • Kampuni ya kizalendo yajitokeza kulitumbua

GABRIEL MUSHI

KATIKA moja ya mambo yaliyodhihirika kuzorotesha utendaji wa bandari ya Dar es salaam pamoja na bandari nyingine nchini, ni kutokuwapo kwa matumizi sahihi ya mita za kupimia mafuta (flow meters) yanayoletwa nchini kwa njia ya meli.

Tatizo hili kwa mara ya kwanza lilifichuliwa Februari 2016 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo na kukuta mita hizo muhimu hazifanyi kazi zaidi ya miaka mitano hali iliyochangia kuharibika na kushika kutu licha ya kununuliwa kwa gharama kubwa ya zaidi ya Dola za Marekani milioni sita (Sh bil 12.96) mwaka 2012.

Licha ya Majaliwa kuwatumbua baadhi wa vigogo wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), akiwamo Afisa Mtendaji Mkuu, Magdalena Chuwa, Septemba mwaka huohuo 2016, Rais John Magufuli naye alifanya ziara katika bandari hiyo na kukuta tatizo la  mita ya kupimia mafuta (flow meters) halijatatuliwa.

Aidha, kutokana na hali hiyo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliagizwa kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta.

Tatizo hilo liliendelea kuitesa TPA ambapo Disemba mwaka 2017, ilielezwa kuwa bandari hiyo imeamua kutoza gharama za mafuta yanaoingizwa nchini kwa kutumia vipimo vya taasisi nyingine za serikali ikiwemo wakala wa vipimo nchini-WMA- na mamlaka ya mapato nchini-TRA- baada ya flow meter zilizokuwa zinatumika kuhakiki kiwango cha mafuta kuharibika kwa muda mrefu.

Hata hivyo, hadi Oktoba mwaka jana tatizo hilo lilikuwa halijatatuliwa ambapo Waziri wa Nishati, Dk. Merdard Kalemani alisema ufungaji wa mita za kupimia mafuta, maarufu ‘flow meter’ katika bandari zote nchini, uko katika hatua za mwisho

Hayo yalibainika katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kilichokuwa kikijadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu hali ya miundombinu ya kupokelea mafuta katika bandari, maghala ya kuhifadhi mafuta na ‘flow meter’.

Alisema kwa sasa ‘flow meter’ ziko kwenye mchakato wa ununuzi na suala hilo linakwenda haraka na muda si mrefu litakamilika na kulitolea taarifa.

Kauli hii ya waziri iliendelea kudhihirisha kuwa tatizo la upatikanaji wa flow meter bado ni changamoto licha ya Serikali ya Awamu ya tano kulichukulia hatua mbalimbali kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu.

Mamlaka ya kudhibiti Nishati, Maji na Gesi (EWURA) walipoulizwa mwezi huu kuhusu suala la ‘flow meters’ walisema wasihusishwe kwani sio sehemu ya tatizo ingawa ndio wanaodhibiti masuala ya petroli nchini. Inaonekana suala hili ni kaa la moto ingawa wanaoweza kulitatua wapo lakini hawaonekani.

Kwani hayo yanajiri katika kipindi ambacho zipo baadhi ya kampuni za kizalendo nchini zenye uwezo wa kutatua tatizo hilo ikiwamo kampuni ya Petrogas ambayo inaonekana kuwa na ufunguo wa kumaliza tatizo. Ni makosa makubwa kuishi kwa kukisia wakati watoa huduma sahihi wapo na wanauwezo wa kiteknolojia na kiwakala.

Wadadisi wa mambo wanahoji kuna tatizo gani kwenye kupata suluhu ya tatizo hilo linalokosesha nchi na Mamlaka ya Kodi kiasi kikubwa cha kodi. Tuzinduke!

Flow meter ni nini?

Flow meter ni teknolojia ya mitambo ya kuhamisha umiliki kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi (custody transfer) inayopima kiwango cha ubora na ujazo wa mafuta na gesi pamoja na vimiminika vingine.

Teknolojia sahihi ni ile inayoweza kutumika kutoa ushahidi ili kumaliza ubishi kwenye migogoro baina ya mletaji na mpokeaji, muuzaji na mnunuzi ama mlipa kodi na mtoza kodi.  

Katika mazungumzo yake na MTANZANIA kuhusu teknolojia hiyo mtaalamu wa Kampuni ya Emerson yenye makao makuu nchini Marekani, William Fernandes anasema teknolojia ya Flow Meters zipo za aina nyingi tofauti yake ni ubora na kutohitaji matengenezo baada ya kufungwa kwa lengo la kupunguza gharama kwa mnunuzi.  

Anasema hadi sasa Flow Meters zinazoaminika kuwa na usahihi wa hali ya juu katika upimaji wa viwango vya ubora na ujazo wa mafuta na gesi ni Micro Motion Coriolis Flowmeters na Daniel Ultra Sonic Flowmeters.  

Mtaalamu huyo wa Emerson anafichua kuwa mgunduzi wa teknolojia ya Coriolis flow meters zaidi ya miaka 50 iliyopita ni Kampuni ya Emerson inayowakilishwa hapa nchini na Kampuni ya kizalendo ya Petrogas Field Services Limited.   

Anasema Emerson imekuwa gwiji katika sekta ya ugunduzi wa teknolojia ya flowmeters kutokana na kujikita kwa muda mrefu kwani teknolojia zake nyingine zimedumu kwa muda wa miaka zaidi ya 130 hadi sasa.   

Fernandes anaeleza kuwa katika muda huo Emerson ndio waliogundua teknolojia ya iitwayo ‘Positive Displacement’ (PD) na baadaye kuiuza kwa kampuni nyingine duniani ambazo zinauza kwa kampuni nyingi na mashirika mengi ya serikali teknolojia hiyo ambayo Emerson walishaacha kuwauzia wateja wao tangu walipobaini matatizo yake.  

Anasema kuwa miongoni mwa matatizo waliyobaini yanayotokana na teknolojia ya Positive Displacement ni pamoja na kuharibika mara kwa mara hivyo kumsababishia mteja gharama kubwa za kusimamisha mitambo na kuingia gharama za matengenezo na hivyo kusababisha upotevu wa mapato kwa upande wa serikali na hasara kwa wafanyabiashara wa mafuta na gesi.  

“Baada ya kubaini kwamba teknolojia hiyo inaingiza hasara kwa wanunuzi tukaamua kutengeneza teknolojia ya mita ambazo ni rafiki kwa wanunuzi zisizowaingiza katika gharama za kuharibika na kulazimisha kuzimwa kwa mitambo na zenye usahihi wa juu wa kupima mafuta, gesi na vimiminika vya aina mbalimbali” anasema  Fernandes.   

Katika kuhakikisha wataalamu wa sekta hiyo ya nishati na gesi wanafahamu umuhimu wa matumizi ya mita hizo za kisasa, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Petrogas Field Services Limited na Kilimanjaro International Inc., Greyson Kiondo anasema kampuni ya Petrogas kwa kushirikiana na Emerson wataendelea kutoa kozi mbalimbali kwa wataalamu wa sekta hiyo.   

Anasema katika kuwawezesha wataalamu wa Tanzania ili kuendana na dhana ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda Petrogas kwa kushirikiana na Emerson wameendelea na utoaji wa kozi kwa wataalamu wa sekta hiyo ili watambue faida za kutumia teknolojia mpya ya Micro Motion Coriolis  Flow Meters.   

“Kwa mara ya kwanza Emerson na Petrogas tulitoa elimu ya teknolojia ya mita  za Coriolis na Daniel Ultra Sonic, Novemba 2018, jijini Dar es Salaam ambapo wataalamu zaidi ya 50 walinufaika na mafunzo hayo ikiwemo na wateja kununua mita hizo,” anasema Kiondo.  

Anasema mwaka huu wamepanga kufanya mafunzo mengine Aprili 29, mwaka huu ikihusisha wataalamu mbalimbali wa sekta hiyo ya nishati ya mafuta, gesi na umeme wakiongezeka kutoka 50 wa mwaka jana na kufikia zaidi ya 70 kutoka kampuni mbalimbali nchini.  

Baadhi ya walengwa wanaotarajiwa kushiriki kongamano hilo ni pamoja na kampuni binafsi na mashirika ya umma yanayohusika na uagizaji,  uchakataji, ufuaji, usambazaji, na uuzaji wa mafuta, gesi, umeme pamoja na taasisi za serikali.

Tofauti na kongamano la mwaka jana kampuni ya Petrogas na Emerson wamejipanga kutoa uelewa mpana zaidi kwa wataalamu wa sekta hiyo nchini ili kuwawezesha kupata utaalamu wenye tija na faida kwa kampuni binafsi na mashirika ya umma na kuokoa taifa na hasara zinazotokana na matumizi ya mita zilizopitwa na wakati na ambazo hazitambuliki na wakala wa vipimo kwa mujibu wa sheria za nchi.  

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kushiriki mafunzo hayo, Meneja Uhandisi wa kampuni hiyo Baraka Mkamba anasema kutakuwa na njia mbili za kuwapata washiriki ikiwemo kuleta maombi makao makuu ya ofisi za Petrogas zilizopo barabara ya Haile Selassie Masaki au kwa barua-pepe [email protected]  

 Faida ya teknolojia ya Coriolis Flowmeters 

Akizungumzia kuhusu faida ya teknolojia ya Coriolis, mtaalamu wa Emerson, William Fernandes anasema teknolojia ya “Micro Motion Coriolis  Flowmeters” ni suluhisho la kudumu endapo zitatumiwa na wafanyabiashara  na wateja wao (kama vile kampuni za madini na ujenzi wa reli), mashirika ya umma na bandari zetu katika upimaji wa mafuta na gesi wakati wa kupakuliwa kutoka kwenye meli, malori, mabomba, ama matenki na kuhifadhiwa kwenye bohari kabla ya kuingizwa sokoni kwa mlaji mmoja mmoja.  

Anasema sababu za kupendekeza kufungwa kwa teknolojia hiyo ni kwamba zinafanyakazi kwa ufanisi mkubwa huku gharama zake za matengenezo  na uendeshaji zikiwa ni ndogo sana ikilinganishwa na teknolojia ya “Positive Displacement (PD)” ambayo inatatizo sugu la kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara. 

Iwapo teknolojia hiyo ya PD itaendelea kutumiwa italeta hasara kwa kampuni za mafuta na mashirika ya umma na serikali kwa upande wa mapato ya kodi.  

Fernandes anasema “faida ya kutumia teknolojia ya Micro Motion Coriolis  Flowmeters ni pamoja na kuwawezesha wateja wetu (muuzaji na mnunuzi)  kubaini mafuta na gesi endapo vimechakachuliwa kwa kuchanganywa na vimiminika vingine haramu kama maji au mafuta ya taa.

“Kukosekana kwa Micro Motion Coriolis Flowmeters yenye ubora wa viwango vya kampuni yetu kutamsababishia mteja alipie maji, hewa, povu, matope na uchafu mwingine vilivyo ndani ya mafuta na gesi wakati wa kupakua kutoka kwenye meli ama kupokea kutoka kwa kampuni ama mamlaka nyingine,” anasema. 

Anafafanua kuwa ni muhimu kuzingatia kigezo cha usahihi katika ununuzi wa flowmeters ili kuziba mianya ya kuibiwa ama kupunjwa katika uhamishaji wa umiliki wa mafuta na gesi. Kigezo kingine cha kuzingatia ni kwamba siyo kila mtengenezaji wa Coriolis flowmeters amethibitishwa kuwa na hadhi ya kutengeneza na kufunga mitambo inayokidhi viwango vya kimataifa vya mizani na vipimo (Custody Transfer Approved).   

“Kigezo hiki ni muhimu sana kwani huondoa migogoro ya kisheria juu ya mizani na vipimo (legal metrology) ambayo inaweza kujitokeza mara kwa mara katika uagizaji na upokeaji wa mafuta na gesi baina ya serikali na Kampuni kubwa za kimataifa kwa upande mmoja na baina ya Kampuni za mafuta nchini kwa upande mwingine.   

“Pamoja na ubora wake, Coriolis flowmeters zote hazitengenezwi kwa usawa kwa sababu kampuni zinazidiana kiteknolojia na uzoefu haswa kama sio wagunduzi na waasisi wa teknolojia husika.

“Mnunuzi ataokoa gharama akifungiwa teknolojia ya flowmeter na Kampuni moja tu yenye ujuzi, uzoefu wa miaka mingi, na uwezo wa kifedha wa kusanifu, kuunda, kutengeneza, kujenga, kufunga, kukabidhi, na kuihudumia mitambo hiyo na kuchukua dhamana na wajibu wa kuitunza badala ya kutumia kampuni za mchanyato wa teknolojia (systems integrators) zinayokusanya utitiri wa mitambo na vipuri kutoka watengenezaji mbalimbali na kukabidhi mfumo mchanyato kwa mteja na kuondoka,” anasema.

Anasema pasipo umakini mkubwa, mteja atajikuta anataabika wakati wa matengenezo baada ya kipindi cha uangalizi kuisha na kukabidhiwa mtambo na kampuni ya mchanyato wa teknolojia.

Kimsingi, mteja ataepuka gharama lukuki kabla, wakati, na baada ya kufungwa kwa mfumo wa mita za mafuta na gesi endapo atachagua miongoni mwa kampuni zinazotengeneza zenyewe chini ya nembo zao Coriolis flow meter, flow computer, valves, smart transmitters, densitometer, gas chromatograph, prover, pamoja na skid.”  

Anasema upotevu wa mafuta na gesi kwa njia za wizi ama miundombinu mibovu vinaweza kuepukwa sasa kwa kutumia mitambo ya Coriolis flowmeters.

“Zipo kampuni chache sana duniani zinazoweza kumpa mteja na wadau wake mfumo wa mita wenye uwezo wa kuona mwenendo mzima wa mihamala ya mafuta na gesi inavyoendelea kufanyika wakati wowote kupitia kwenye kompyuta na simu-janja bila mteja na wadau wake kama mamlaka za serikali za udhibiti, usimamizi, uchunguzi, na kukusanya kodi kulazimika kwenda kwenye meli ama kupanda ngazi ndefu kueleka angani kuchungulia ndani ya matenki makubwa na marefu kwenye bohari zinazopokea na kutoa mafuta na gesi.

“Teknolojia ya Micro Motion Coriolis Flowmeter ina uwezo wa kufanya hayo yote na zaidi kwa sababu itabaini kama mabomba ama matenki ya mafuta na gesi yametoboka kwa hujuma ama ubovu wa miundombinu,” anasema.  

 Anahitimisha Fernandes, “kikubwa zaidi, teknolojia ya Micro Motion Coriolis Flowmeter imetumika kutoa ushahidi na kumaliza ubishi mahakamani duniani kote kwenye migogoro baina ya mletaji na mpokeaji, muuzaji na mnunuzi ama mlipa kodi na mtoza kodi”.  

Aidha, Kiondo anasema Petrogas Field Services Ltd ni kampuni ya kizalendo kwa asilimia 100 iliyoanzishwa mwaka 2013 jijini Dar es Salaam.  

Anasema kampuni hiyo ilianzishwa kwa kutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya sekta ya mafuta na gesi lakini sasa imefanikiwa kuwa wasambazaji na wafungaji wa mitambo na vipuri vinavyotokana na sekta hiyo kwa kushirikiana na Emerson. 

“Petrogas imejiandaa katika kuhudumia sekta ya viwanda inayokuwa kwa kasi chini ya Serikali ya Rais John Magufuli. Tuna uhakika wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania na katika ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asilia mkoani Lindi kwa kutumia mitambo ya kisasa ya Micro Motion Coriolis Flowmeters na Daniel Ultra Sonic Flowmeters ambayo itazuia taifa kupunjwa ama kuibiwa mapato katika uhamishaji wa umiliki wa mafuta na gesi kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi”, anamalizia Kiondo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles