25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA HECHE YAJICHIMBIA KUJADILI KIFO


 Na MWANDISHI WETU-TARIME    |

FAMILIA ya Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), imesema kwa sasa wapo kwenye majadiliano ya kifamilia kabla ya kutoa tamko juu ya kifo cha ndugu yao, Suguta Marwa (27), mkazi wa Kijiji cha Sirari, Kata ya Sirari, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, ambaye aliuawa kwa kuchomwa kisu na polisi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Heche alisema kwa sasa bado wapo kwenye majadiliano ya kifamilia na mara baada ya kukamilika watatangaza tarehe ya mazishi, ikiwa ni pamoja na hatua ambazo familia wameamua kuchukua kutokana na kifo hicho.

Alisema tukio la Suguta kuchomwa kisu ni kisa cha tatu cha polisi dhidi ya familia yao, kwani mwaka juzi, Enock Heche, alipigwa na polisi na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu, aliunda tume na mmoja wa wajumbe wake alikuwa Barnabas Mwakarukwa na ilibainika alionewa.

Alisema askari wanne waliohusika katika tukio hilo walisimamishwa kazi na Kamanda wa Polisi aliyekuwapo alidai aliondolewa kwa fitna zilizosukwa na chama kimoja cha siasa (kimaadili hatuwezi kukitaja kwa sababu wahusika wake tulishindwa kuwapata kutolea ufafanuzi).

Alilitaja tukio la pili kuwa ni kitendo cha yeye binafsi kuwahi kutishiwa kuuawa na polisi na hadi sasa yapo mambo mengi juu ya tukio hilo ambayo hayajasemwa.

“Kwa hili nadhani linapaswa kufika mbali na tunataka kuona watalimalizaje, ndio maana tupo vikaoni kujadiliana na hatujaamua tutazika lini, hadi Jumatatu tutakapokaa kikao cha mwisho,” alisema Heche.

Suguta aliuawa Aprili 26, mwaka huu saa 6:30 usiku wakati akiwa chini ya ulinzi wa polisi wawili, ambao walimkamata kwa madai ya kuwarushia chupa wakati wakiwa wamemchukua mmiliki wa Baa ya Casablanca iliyopo Sirari, Neila Peter Jacob (31) kwa kosa la kufanya biashara hiyo hadi saa 6:30 usiku.

Akizungumzia tukio hilo, juzi Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, alisema Suguta alichomwa kisu na askari mwenye namba E. 1156 Koplo William Marwa wakati akikaribia kufikishwa kituoni baada ya kutokea kutoelewana naye kutokana na kushambuliana kwa maneno kwa lugha ya Kikurya.

Alisema askari hao wakiwa katika doria ya gari, walifika kwenye baa hiyo, lakini wakati wakimkamata mmiliki wake kwa kosa la kufanya biashara nje ya muda, Suguta alianza kuwarushia chupa, hivyo walirudi kumkamata, lakini walipompekua walimkuta na kisu ambacho Koplo Marwa alikaa nacho.

“Baada ya askari kumkamata na kumpekua, walimkuta na kisu na kuchukuliwa na Koplo Marwa, sasa wakiwa wanaelekea kituoni, kulitokea ugomvi kati ya marehemu na askari huyo na walikuwa wakijibishana kwa lugha ya Kikurya, jambo ambalo askari wengine hawakuelewa, lakini walipofika karibu na kituo cha polisi, askari huyo alimjeruhi kwa kisu,” alisema.

Tangu jana, kamanda huyo alitangaza kushikiliwa kwa askari huyo ambaye alimjeruhi sehemu ya mgongo upande wa kulia na kufariki njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime kutibiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles