22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Ewura yatunuku vyeti kwa mamlaka tatu

Clara Matimo – Mwanza

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura)Kanda ya Ziwa, imetoa tuzo na vyeti kwa mamlaka tatu za maji na usafi wa mazingira za kanda hiyo  zilizofanya vizuri kiutendaji kwa mujibu wa ripoti ya  mwaka wa fedha 2018/19.

Mamlaka hizo, ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (Mwauwasa) ambayo iko katika mamlaka za maji za mikoa,  Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama- Shinyanga (Kashwasa)  iliyopo katika mamlaka za miradi ya kitaifa na  Mamlaka ya Maji Biharamulo iliyopo  kundi la mamlaka za maji ya wilaya na miji modogo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzikabidhi mamlaka  tuzo na vyeti  ofisini kwake hivi karibuni,  Meneja wa Kanda wa Ewura, George Mhina alisema vigezo walivyotumia kupata washindi  ni pamoja na kuangalia  mamlaka zilizofanya vizuri katika kudhibiti upotevu wa maji,  utoaji  huduma bora ya maji safi na usafi wa mazingira, masaa ya kutoa huduma, ubora wa maji, jinsi  zinavyokusanya mapato yake na namna zinavyolipa tozo.

Alisema tangu mamlaka hiyo ianzishwe miaka 13 iliyopita kwa kipindi cha miaka 11 mfululizo  imekuwa na utaratibu wa kuandaa ripoti ya utendaji na kushindanisha mamlaka za maji lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama huku wakilenga kuwafikia wananchi wengi.

Alisema shindano hilo liligawanywa makundi mawili ambapo  ripoti 34  za utendaji za  mikoa na miradi ya maji ya kitaifa zilishindanishwa   na zingine ni ripoti 83 za utendaji za wilaya  na miji  ya wilaya.

“Miaka yote 11 ambayo tumekuwa tukishindanisha mamlaka hizi tulikuwa hatushindanishi mamalaka za maji za miradi ya kitaifa tulikuwa tunashindanisha mamlaka za mikoa na mamlaka za miji za wilaya na miji midogo  lakini mwaka huu na zenyewe tumeziingiza kwenye shindano.

“Kwa upande wa mamlaka za maji za miradi ya kitaifa, Mamlaka ya Kashwasa imekuwa ya kwanza katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira na kuzuia upotevu wa maji, Mwauwasa imeshika nafasi ya tatu katika mamlaka za mikoa na Biharamulo nafasi ya tatu kwa mamlaka za miji ya wilaya na miji midogo  kwa kufanya vizuri katika utendaji kazi,”alisema na kuongeza

“Kwa upande wa mamlaka za mikoa iliyoshika nafasi ya kwanza ni Moshi ikifuatiwa na Tanga, mamlaka za miradi ya kitaifa ya pili ni Manawasa ikifuatiwa na Chalinze na mamlaka za miji ya wilaya  na miji midogo ya kwanza ni Makambako ikifuatiwa na Mikumi lakini hizo zitapewa tuzo na vyeti na viongozi wa Ewura wa Kanda hizo,”alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kashwasa, Mhandisi Lawrence Wasala, aliishukuru Ewura kwa kushindanisha mamlaka za miradi ya kitaifa maana wamejisikia vizuri kwa sababu juhudi zao zimetambuliwa na kwamba siri ya ushindi walioupata ni kufanya kazi kwa kushirikiana ambapo aliahidi wataendelea kushirikiana ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,502FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles