26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

EWURA yatangaza bei mpya za mafuta

*Yatahadharisha kupanda kwa bei Machi na Aprili

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetaja bei mpya za mafuta ya taa, petroli na dizeli kwa mwezi Februari, 2022 huku ikidai Machi na Aprili kuna uwezekano wa bei za mafuta kupanda kutokana na mwenendo wa mafuta katika soko la dunia.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo Februari mosi, kuhusu mwenendo wa bei za mafuta nchini Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema bei za rejareja za mafuta ya taa, dizeli na petroli yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa Sh 21 kwa lita (Petroli), Sh 44 kwa lita (Taa) na  Dizeli Sh 13 kwa lita.

Amesema bei za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini ikihusisha Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimepungua kwa Sh 123 kwa lita (petroli) na Sh 92 kwa lita(dizeli).

Amesema kutokana na kumalizika kwa mafuta ya taa kwenye maghala ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo wa EWURA ameeleza kuwa bei za rejareja za mafuta ya taa kutoka mikoa hiyo ya Kaskazini itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

Mhandidi Chibulunje amesema mwenendo wa bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kusini ikihusisha Mtwara, Lindi na Ruvuma zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Serikali la Januari 5, mwaka huu kutokana na mwezi huo kutokuwa na shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza mwenendo wa bei za mafuta kwa mwezi Machi na Aprili mwaka huu kwa kufuatilia bei za soko la dunia kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa bei za mafuta.

“EWURA itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta kwa ukaribu ili kuona namna ya kuishauri serikali hatua za kuchukua katika harakati za kupunguza makali ya bei,”amesema.

Amesema katika kuhakikisha kunakuwa na ushindani sawa katika bei zinazoanza kutumika kesho ununuji wa mafuta katika maghala sasa kutakuwa na bei mbili ambazo ni bei kikomo ambayo muuzaji hatakiwi kuzidisha na bei ya chini ambayo muuzaji hatakiwi kushusha zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles