28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ewura kutumia maonesho ya biashara Afrika Mashariki kutoa elimu ya nishati na maji

Na Clara Matimo, Mwanza

Mamlaka  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura)Kanda ya Ziwa, imepanga kuyatumia maonesho ya 16 ya biashara Afrika Mashariki yanayoendelea katika uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza kutoa elimu ya  maji  nishati ya umeme  na gasi kwa  wananchi.

Meneja wa  Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina.

Akizungumza na MTANZANIA Digita kwenye viwanja hivyo jana, Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa,  George Mhina,  amesema kutokana na ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda unaopita kwenye baadhi ya mikoa ya kanda hiyo ambayo ni Kagera Shinyanga na Geita wafanyabiashara wanapaswa kufahamu fursa zilizopo ili waweze kushiriki na kujiingizia vipato.

Amesema kupitia maonesho hayo wafanyabiashara watakaofika uwanja wa Rock City Mall kwenye banda la Ewura  ambao wana nia ya kushiriki katika ujenzi wa bomba hilo la mafuta watapate elimu ya mambo mbalimbali ikiwemo  jinsi ya kujisajili, vigezo wanavyotakiwa kuwa navyo na nyaraka wanazopaswa kuzitumia katika usajili.

“Moja ya kazi zetu ni kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za nishati na maji, kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu inasema ‘tukuze uzalishaji mali kwa maendeleo ya uchumi wa  nchi  yetu’, Ewura tunasema  upatikanaji wa huduma za nishati na maji kwa maendeleo ya  uchumi wa  nchi yetu,  hivyo  uwepo wetu utawasaidia wananchi watakaokuja kutembelea maonesho haya kupata  elimu  inayohusiana na udhibiti katika sekta za nishati na maji.

“Mfano ikiwa mfanyabiashara  anataka kuanzisha kituo cha mafuta atajua ni nini afanye ili aweze kupata leseni kutoka Ewura lakini vilevile kama anataka kuwekeza kwenye masuala ya nishati ya umeme  gesi na  maji milango iko wazi, nawakaribisha waje kwenye banda letu maswali yao yote yatajibiwa vizuri pia tutawaelekeza mambo wanayopaswa kuyakamilisha,” amesema Mhina.

Mhina amewasihi wananchi kutembelea maonesho hayo bila kusahau kufika katika banda lao ili wapate elimu kuhusu bili za maji pia ikiwa  hawaliziki na sekta ambazo ewura inazisimamia  watafahamishwa ni wapi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao na utaratibu  wa kushughulikia malalamiko ukoje.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo  Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene, amesema  bidhaa tofauti tofauti zitaoneshwa kwenye maonesho hayo ikiwemo za kilimo, mifugo,  chakula, vinjwaji, viwandani, tehema, nishati na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.

“Bidhaa ambazo hatuziruhusu kwenye maonesho haya ni madawa ya kulevya, silaha, milipuko, masuala ya dini na siasa, lakini mbali na huduma na biashara mbalimbali pia kuna vivutio vya aina nyingi kama wanyama pori hai wakiwemo simba, fisi, nyoka aina ya chatu, mamba na wengine wengi pamoja na michezo ya watoto, nawaomba sana wananchi wa Mkoa huu na mikoa jirani wafike wajionee,”amesema Kenene.

Kwa mujibu wa Kenene, TCCIA imechukua tahadhari zote za kuwakinga wananchi wote wanaofika kwenye maonesho hayo na ugonjwa wa UVIKO 19 ambazo ni pamoja na uvaaji wa barako pia  kunawa maji tiririka na sabuni kwa kila mtu anayeingia kwenye viwanja hivyo, uwepo wa vitakasa mikono katika kila banda pamoja na watu kukaa mbali kwa kuachiana nafasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles