Escrow mpya

Pg 1*Zitto ataka Bunge kuunda kamati teule kuchunguza ufisadi wa trilioni 1

 

Na Elizabeth Hombo, Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameibua Escrow mpya, baada ya kulitaka Bunge kuunda kamati teule kuchunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni dada ya Stanbic Tanzania juu ya mkopo wa hatifungani wa dola za Marekani milioni 600 ambao umegubikwa na ufisadi.

Pia amesema Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa wabunge kuhusu masuala hayo ili kuzuia ukiukwaji wa sheria ambazo Bunge limejitungia.

Alisema Benki ya Stanbic kupitia tawi lake hapa nchini siku waliyopata dili la ‘bondi’, ndiyo siku hiyo hiyo walipewa kazi na Serikali ya kufungua akaunti ya Escrow kuhusu fedha za bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Zitto alitoa kauli hiyo mjini Dodoma, wakati akichangia mjadala wa hotuba za bajeti za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Utawala Bora bungeni jana.

Alisema Machi 8, 2013, Serikali ya Tanzania ilikopa dola za Marekani milioni 600 kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard Bank ICIC Plc.

“Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda (floating rate), umeanza kulipwa Machi, mwaka huu, kama kweli Serikali imeanza kutekeleza mkataba huu, utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana.

“Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba la dola milioni  897 (takribani Sh trilioni mbili).

Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, alisema mkopo huo umegubikwa na ufisadi na baadhi ya Watanzania wamefikishwa mahakamani kuhusu suala hilo.

“Sitapenda kueleza upande wa waliopo mahakamani. Kesi iliyopo mahakamani inahusu dola milioni sita ambazo inasemekana (kwa mujibu wa nyaraka za mahakama) kuwa zilitumika kuhonga maofisa wa Serikali ili benki hiyo iweze kupata biashara iliyopata.

“Jambo la kushangaza wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa.

Waliopo mahakamani ni wale waliotumika kupeleka rushwa.

“Mjumbe kashtakiwa, aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku zijazo.

“Mheshimiwa Spika, hapa mbele yangu nina barua ambayo kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 kutoka kona zote za dunia wamesaini kutaka Benki ya Standard ya Uingereza ichunguzwe kwenye suala hili la hatifungani,” alisema Zitto huku akishangiliwa na wabunge wa upinzani.

Alisema kimsingi biashara ya akaunti ya Escrow katika benki hiyo ni kubwa zaidi kwa sababu ina kazi ya kutunza fedha za bomba la gesi kwa miaka 20.

Zitto alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walitumia taarifa ya Taasisi SFO ya Uingereza kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hilo, lakini SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard Bank.

“Hatujui ni kwa masilahi mapana ya Uingereza au ni kwa kupitiwa. Tanzania tumejikuta tunafuata matakwa ya Uingereza katika jambo hili, kiasi cha hata kutumia ushauri wa kitaalamu wa Waingereza.

“Leo hii, Takukuru inasaidiwa katika kesi hii na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu benki ya Uingereza. Watanzania walioandika ‘petition’ kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote kujulikana – Standard Bank walihusika kwa kiwango gani kutoa rushwa ili kupata biashara?,” alisema.

Alisema Takukuru wanapaswa kufanyia kazi jambo hilo kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, mashtaka ya kutoa rushwa ili kupata biashara.

“Takukuru inaogopa wazungu, kuwaudhi watu wanaowapa ushauri wa kitaalamu kuhusu kesi za rushwa,” alisema Zitto.

Alisema endapo Tanzania itafanikiwa kujua Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini, itafaidika kwa namna mbili.

“Mheshimiwa Spika, masilahi ya Tanzania hapa ni makubwa mno. Moja itakuwa ni fundisho kubwa kwa makampuni ya kimataifa, kwamba Afrika si mahala pa kuhonga na kupata kazi na kutoadhibiwa.

“Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake. Tutakuwa tumeokoa zaidi ya Sh trilioni mbili katika deni la Taifa na kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi wetu kwenye afya na elimu.

“Takukuru waongozwe na masilahi mapana kwa Taifa, badala ya kutafuta sifa ndogondogo za ‘wangapi wamefikishwa mahakamani’, lazima taasisi zetu sasa zianze kutazama mambo kwa picha kubwa,” alisema.

Alisema Tanzania isikubali kubeba makubaliano ambayo SFO inafanya na makampuni ya kimataifa.

“Ni lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya. Haiwezekani wawe Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha wanaotoa wanaendelea na biashara zao kama kawaida,” alisema Zitto.

Alisema kuna taarifa hata fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huo hazikufika kunakotakiwa.

 

UCHUNGUZI WA IPTL

Alisema uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka akaunti ya Tegeta Escrow kwenda Benki ya Stanbic Tanzania, umekuwa ni jipu kubwa ambalo Serikali imekuwa ikilikimbia.

“Naomba tupate kauli ya Serikali kuhusu jambo hili, ni moja ya jipu kubwa… Serikali inaogopa nini? Inamwogopa nani? Kwanini kesi ya ufisadi wa IPTL inakaliwa kimya?” alihoji.

Alisema pamoja na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilifanya uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, lakini katika taarifa zote ambazo Takukuru imekuwa ikitoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna hata siku moja wameitaja IPTL.

Aliitaka Ofisi ya Rais Ikulu kuzingatia sheria na taratibu kwa kuwa madhara ya kutofuata ni makubwa.

“Kwa mfano, hivi sasa bajeti za taasisi hazimo kwenye vitabu vya bajeti ya Serikali kinyume na sheria ya bajeti, wabunge wanapaswa kuwa na nyaraka za bajeti hizo, lakini hazipo,” alisema.

 

MWAKA 2014

Hii ni mara ya pili kuibuka sakata la Escrow ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014 baada ya Zitto ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, kuwasilisha hoja bungeni akihoji uchotaji wa dola za Marekani milioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Akaunti hiyo, ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na Kampuni ya Independent Power Limited (IPTL)

na kuuzwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Sakata la Tegeta Escrow liliwang’oa vigogo mbalimbali waliotajwa kuhusika, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospether Muhongo, Katibu wake, Eliackimu Maswi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here