24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amtumbua kigogo kwa kususa mshahara

juliet-Kairuki (1)Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, ameendelea na kazi yake ya kutumbua majipu, baada ya kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Julieth Kairuki.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kwa sababu Kairuki amekuwa hapokei mshahara wake tangu alipoajiriwa mwaka 2013, jambo ambalo linazua maswali mengi.

“Pamoja na mambo mengine, hatua hii imechukuliwa baada ya Rais kupata taarifa Kairuki amekuwa hachukuwi mshahara wake tangu alipoajiriwa Aprili, 2013 hadi sasa jambo ambalo linazua maswali mengi,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo haikueleza kwa kina sababu za Kairuki kutopokea mshahara wake au kama kulikuwa na mgogoro wa kimkataba au la.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kairuki atapangiwa kazi nyingine kama atakuwa tayari kufanya kazi na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Clifford Tandari ameteuliwa kukaimu nafasi iliyoachwa na Kairuki, huku mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mtendaji mpya ukiendelea.

Kutokana na suala hilo kuibua maswali mengi, MTANZANIA ilizungumza na Wakili wa kujitegemea, Emmanuel Muga ambaye alisema kutopokea mshahara si kosa na ndiyo maana hajapelekwa mahakamani.

“Kutopokea mshahara si kosa, lakini kwa kanuni za utumishi wa umma mtu hatakiwi kujiweka kwenye nafasi ambayo inaleta picha mbaya, mfano kutopokea mshahara kunaleta maswali mengi, sasa anafanyaje kazi bila kulipwa?” alihoji Muga.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, alisema haiwezekani mtu aache kupokea mshahara pasipo sababu.

“Haiwezekani mtu afukuzwe kwa kutopokea mshahara, sisi pale chuoni zinapita hata awamu tatu hatujapokea stahiki zetu.

“Naona kama Rais ameamua kuunda Serikali mpya, ni bora angetamka anavunja bodi zote ili aunde upya kuepuka watu kufanya kazi katika hali ya taharuki kila siku, huyu katumbuliwa, kesho yule,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema haoni sababu ya kufukuza kazi mtu aliyeamua kujitolea kwa kufanya kazi bila kupokea mshahara wake.

“Kama mtu anajiweza na akaamua kufanya kazi bila kupokea mshahara, sioni sababu ya kumfukuza, ningekuwa Rais ningempa tuzo ya ufanyakazi bora,” alisema Safari.

Juhudi za kumpata Kairuki kuzungumzia suala hilo la kutumbuliwa na sababu za kutochukua mshahara wake hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles