24 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU KWA WATOTO WA WAHAMIAJI ULAYA NI ‘MTIHANI’

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA


RIPOTI mpya iliyotokana na utafiti wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo Ulaya (OECD), imebainisha kuwa watoto wenye wazazi waliohamia Ulaya, wanapitia changamoto linapokuja suala la elimu na nafasi za ajira barani humo.

OECD iliyoanzishwa mwaka 1961 ikiwa na nchi 35 wanachama kwa madhumuni ya kukuza sera za kuimarisha maisha ya watu kiuchumi na kijamii duniani kote, ilisema watoto waliozaliwa Ulaya kwa wazazi wasiotoka bara hilo wanaendelea kupata changamoto nyingi yanapokuja masuala ya elimu na soko la ajira.

Aidha, utafiti wa shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Paris, Ufaransa, umegundua kuwa watoto wa wahamiaji katika bara zima la Ulaya waliowasili baada ya vita vya pili vya dunia wanaoitwa ‘wafanyakazi wageni’ wana nafasi finyu katika safari yao ya kumaliza shule ya sekondari au kupata nafasi ya ajira kuliko watoto ambao wazazi wao wamezaliwa Ulaya.

Hata hivyo, utafiti huo pia umegundua nafasi zilizopo kwa sasa kwa watoto wa wahamiaji ni nafuu kuliko hali ilivyokuwa kwa wazazi wao miaka ya nyuma.

Hata hivyo, umeonesha maisha ya kijamii na kiuchumi ya watoto hao hayaridhishi kulinganisha na watoto wengine.

Hali hii imeonekana wazi nchini Ujerumani. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 50 ya wanawake na asilimia 30 ya wanaume ambao ni kizazi cha kwanza cha wahamiaji kutoka Uturuki na iliyokuwa Yugoslavia hawakuwa na vyeti rasmi vya kumaliza masomo ya sekondari.

Lakini mwaka 2012 zaidi ya asilimia 90 ya watoto wa wahamiaji waliozaliwa nchini Ujerumani walikamilisha masomo yao.

Aidha, robo moja ya watoto wenye wazazi kutoka Yugoslavia walipata kile kinachoitwa ‘Abitur’, yaani ujuzi au sifa inayotolewa katika shule za maandalizi ya ujuzi fulani nchini Ujerumani.

Kwa kulinganisha nusu ya wanafunzi wote nchini Ujerumani wamehitimu kwa cheti cha kidato cha sita ‘Abitur.’

Aidha, idadi ya wanafunzi wa wahamiaji wanaotafuta elimu ya juu bado ni ndogo mno ukilinganisha na watoto wanaozaliwa na wazazi kutoka Ulaya, ukizingatia  nafasi za kuvutia zinazotolewa na  shule za mafunzo ya ajira.

Ripoti hiyo imekuja huku nyingine kutoka Baraza la Ushauri la Mifuko ya Kijamii na Mchangamano Ujerumani (SVR), ikionesha wanafunzi wenye asili ya nje ya bara Ulaya bado wanaonekana kutengwa.

Ripoti hiyo ilionesha uchaguzi wa shule kwa watoto nchini Ujerumani unazidi kutegemeana na asili yao ya kijamii na rangi. Lakini aina hii ya ubaguzi inakuja na athari hasi kwa wahamiaji.

Ni mwenendo ambao umekuwa ukizidi kukua nchini Ujerumani kwa miaka mingi licha ya jaribio la nchi hiyo kuleta mchangamano na mjumuisho wa kijamii.

Ubaguzi umezidi kukua hasa katika vitongoji masikini katika majiji makubwa kama vile Cologne, Frankfurt na Berlin, ambayo ina idadi kubwa ya wahamiaji.

Shule nyingi katika vitongoji hivyo, wanafunzi wengi wanazungumza Kituruki wawapo nyumbani kuliko Kijerumani.

Familia za Kijerumani zinazoishi maeneo hayo hupeleka watoto wao katika shule nzuri zilizopo katika vitongoji vingine – mbali na kule wanasiasa wanakokuita ‘maeneo moto ya kijamii’.

SVR imechapisha utafiti unaoangazia madarasa yenye idadi kubwa ya wanafunzi wahamiaji, ambao mara nyingi wanakabiliwa na mazingira mabaya linapokuja suala la kujifunza na mazingira ya kazi,” anasema Jan Schneider, Mkuu wa Idara ya Utafiti ya SVR.

Badala ya kujikita juu ya sababu ya utengano, watafiti walijikita kuangalia namna shule na mamlaka zinavyokabiliana na tatizo hilo.

SVR inashauri hatua za kisiasa dhidi ya kuwalazimisha wazazi ambao huzungumza Kijerumani kupeleka watoto wao katika shule zinazohudhuriwa na watoto wenye chembe ya uhamiaji ili kuondoa matabaka.

Kwa mujibu wa utafiti huo, hatua kama hizo hazitasaidia mchangamano zaidi ya kuchochea hasira na upinzani wa kisiasa na kijamii.

“Ni kwa sababu hiyo, SVR ilijikita zaidi katika kuangazia njia za kuboresha mazingira kwa wasichana na wavulana kwenye shule zinazoepukwa na wazazi wa Kijerumani.

Shule ya Bertolt Brecht iliyopo katika moja ya vitongoji vya jiji la Bonn, zaidi ya theluthi ya wanafunzi wake wana asili ya kigeni.

Baadhi yao hawana muda mrefu nchini Ujerumani na wengine wamezaliwa humo lakini hawazungumzi Kijerumani na wazazi wao nyumbani.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Reinhold Pfeifer ameweka kipaumbele cha kuimarisha stadi ya lugha kwa wanafunzi wake. Anafahamu ujuzi sahihi wa Kijerumani ni muhimu kupiga hatua kuelekea ‘Abitur’, shahada ya juu ya Kijerumani.

Pfeifer na walimu wenzake hutoa changamoto kwa wanafunzi wa umri mdogo: “Tunachofanya ni kwamba kila darasa la Kijerumani linapangiwa walimu wawili ili mmoja wapo awe na kazi maalumu kuchagua watoto wachache wa makundi maalumu ya kujifunza.

Mbali ya kujikita kwa stadi ya lugha ya Kijerumani, Shule ya Bertolt Brecht pia inatoa kile kiitwacho madarasa ya kimataifa.

“Ni madarasa ambayo tunaunda makundi ya watoto kati ya miaka 14 na 16, ambao watahudhuria madarasa ya ngazi tofauti katika makundi ya kimataifa kwa sababu hawazungumnzi kabisa Kijerumani,” anasema.

“Madhumuni ya madarasa haya ni kuwafunza wanafunzi stadi ya lugha ya Kijerumani ili baada ya miaka miwili au mitatu wajumuishwe kwenye mfumo uliozoeleka wa shule. Mtaala kwa madarasa haya ya kimataifa ni pamoja na masomo 12 ya Kijerumani kila wiki.

Mtaalamu wa elimu nchini humo, Diana Sahrai kutoka Chuo Kikuu cha Duisburg-Essen pia alitathimini elimu na kupongeza mpango wa kutoa kipaumbele stadi za lugha katika shule ya Bonn.

Lakini Sahrai ana wasiwasi na utaratibu wa kutenga madarasa kwa watoto wasiozungumza Kijerumani: “Iwapo madarasa hayo yataendelea kwa muda wa mwaka moja au miwili, wanafunzi, ambao hawazungumzi Kijerumani watabakia kutengwa na kuona ugumu wa kuchangamana na wale wanaozungumza Kijerumani,” alionya.

Lakini Mwalimu Mkuu Reinhold Pfeifer anatetea utaratibu huo, akisema hakuna athari kwa vile utengaji watoto madarasani ni wa muda na wenye manufaa kwa walengwa hasa kutoa kipaumbele kwa walio nyuma katika lugha kuwafikia wenzao: “baada ya muda wanafikia kiwango cha juu hata kufaulu Abitur, anasisitiza.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles