26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

DPP akwamisha   dhamana ya   Mbowe, Matiko

PATRICIA KIMELEMETA

MAHAKAMA Kuu imesimamisha  usikilizaji wa maombi ya dhamana yaliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha notisi katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi mdogo uliotolewa mahakamani hapo na Jaji Sam Rumanyika wa kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa la kutaka rufaa ya Mbowe na Matiko isisikilizwe.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na jopo la mawakili, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Dk. Zainab Mango huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Peter Kibatala, Jeremiah Ntobesya na Jebra Kambole.

Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Rumanyika, alisema baada ya kutupilia mbali hoja ya Jamhuri, mawakili hao wamewasilisha notisi katika Mahakama ya Rufaa ya kupinga uamuzi huo.

Kimsingi, alisema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ana haki ya kisheria ya kufungua maombi ya kukata rufaa wakati kesi ikiendelea katika ngazi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa lakini hana haki hiyo katika mahakama za chini.

“Kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili yaani Jamhuri na utetezi, kwa mujibu wa sheria zilizopo, nimesimamisha mwenendo wa kesi hii hadi mahakama ya rufaa itakapotoa uamuzi,” alisema Jaji Rumanyika.

Awali, Jaji Rumanyika, alitupilia mbali hoja ya upande wa Jamhuri ya kutaka kutoendelea na hatua ya usikilizaji wa kesi hiyo na kusema haina mashiko na kwamba haijakidhi matakwa ya kisheria.

Kutokana na hatua hiyo, aliahirisha kesi hiyo hadi saa nane mchana ili aweze kuendelea na hatua ya pili ya usikilizaji wa rufaa ya maombi ya dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Ilipofika saa nane, upande wa Jamhuri uliwasilisha notisi hiyo na kuomba mahakama hiyo kutoendelea na kesi hiyo hadi mahakama ya rufaa itakapotoa uamuzi.

Wakili Kadushi alidai kuwa hoja yao ni ya msingi kwa sababu DPP ana mamlaka ya kisheria ya kusimamisha kesi hiyo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotolewa uamuzi.

“Ninaomba mahakama yako, kusimamisha mwenendo wa kesi hii hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi,” alidai Kadushi.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Kibatala na aliyedai haina mashiko na kuomba mahakama hiyo kuendelea na hatua ya usikilizaji kama ilivyosema hapo awali.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Rumanyika, alisema hoja ya DPP ina mashiko na kwamba hawezi kuendelea na kesi hiyo hadi uamuzi utapotolewa na Mahakama ya Rufaa.

Awali, kabla ya kesi hiyo kuanza, wafuasi wa Chadema na Chama cha Wananchi (CUF), walikutana katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kusiliza uamuzi wa kesi mbili tofauti, moja ya Mbowe na nyingine ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, iliyokuwa itolewe hukumu kama ni mwenyekiti halali wa chama hicho au la.

Baada ya wafuasi hao kufurika mahakamani hapo, Jeshi la Polisi lililazimika kuimarisha ulinzi ili kuepusha vurugu.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye wafuasi hao walianzisha vurugu za kutaka kuingia ndani bila utaratibu na kusababisha polisi kuwazuia na kuwataka waondoke katika maeneo hayo lakini baadhi yao waligoma kuondoka na huku wengine wakikamatwa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles