DPP akata rufaa kupinga waandishi kusikiliza kesi masheikh Uamsho

0
825

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP),  amekata rufaa Mahakama Kuu akipinga wananchi na waandishi wa habari kuingia kusikiliza na kuripoti kesi  ya ugaidi inayomkabili  Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed na mwenzake  22.

DPP amefikia uamuzi huo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde kutoa uamuzi akiruhusu waandishi wa habari kuingia katika kesi hiyo wakati unaendelea.

Mahakama iliondoa amri ya kuzuia waandishi wa habari kuandika mwenendo wa kesi hiyo kwa sababu haijafikia katika hatua ya usikilizwaji hivyo ilisemanwanaruhusiwa kuiripoti.

Katika rufaa iliyokatwa na DPP wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kuondoa amri ya Juni 18, mwaka 2015 ya kuzuia wananchi na waandishi kuingia kusikiliza kesi hiyo.

DPP anadai mahakama ilikosea kutoa amri hiyo wakati kuna amri nyingine hivyo asingeweza kutoa tena.

Jamhuri inadai mahakama ilikosea kuamuru wananchi na waandishi kuripoti kesi hiyo wakati kuna zuio.

Katika hoja ya mwisho inadaiwa mahakama ilikosea kuchambua hoja mbalimbali za Jamhuri ambazo zilikuwa zina msingi.

Awali washtakiwa kupitia mawakili wao, Abubakar Salim, Juma Nassoro na wengine waliwasilisha maombi mawili mahakamani ambapo ombi la kwanza walitaka mahakama imshauri DPP kukamilisha upelelezi ndani ya mwezi mmoja na ombi la pili mahakama iondoe amri ya kuwazuia waandishi wa habari kuripoti kesi hiyo.

Mahakama katika uamuzi wake ilimpa njia mbili DPP, moja kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ndani ya muda mfupi na njia ya pili kama anaona kuna sababu za upelelezi kuchelewa kukamilika aliondoe shauri hilo Mahakamani, akipata ushahidi atawashtaki tena.

“Katika maombi ya kuondoa amri ya  kuripoti  kesi hiyo, mahakama inaondoa amri hiyo, hiyo amri ilitolewa bila kudhamiria kwa sababu kifungu namba 34 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kinahusu mamlaka ya Mahakama Kuu, Mahakama Kuu ndio inaweza kutoa amri hiyo kwa sababu sheria inazuia kuandika jina na kutoa picha ya shahidi wakati wa usikilizaji wa kesi .

“Kwa hatua iliyofikia kesi hii, usikilizwaji bado hivyo waandishi wanaruhusiwa kuingia na kuandika kwa lengo la kutenda haki,” alisema.

Kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2014 ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti mwaka 2014.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya  kuwaingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.

Mbali na Farid na Jamal Swalehe washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.

Wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka 2014 washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.

Inadaiwa katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Pia Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na akijua, alitoa msaada kwa watu hao wa kutenda vitendo vya kigaidi kinyume cha sheria. Pia anadaiwa kuwa katika kipindi hicho akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here