Majaliwa atoa onyo kwa watorosha madini

0
1068
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza Meneja Mkuu wa Mgodi wa Stamigold, Gilay Shamika, wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Tekinolojia ya uchimbaji madini Mjini Geita jana. Wa pili Kulia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Mwandishi Wetu-Geita

WAZIRI Mkuu Kasim Majaliwa, ametoa onyo kwa watu wanaotorosha madini, badala ya kuyauza katika masoko yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali, huku Waziri wa Madini, Dotto Biteko, akisema watu hao wanatafuta kuishia jela ama kufilisiwa.

Viongozi hao walisema hayo jana mjini Geita, wakati wa kufungua maonyesho ya pili ya teknolojia ya uchimbaji madini.

Akifungua maonyesho hayo, Majaliwa alisema kuanzia Machi mpaka Septemba,mwaka huu,  tayari madini yaliyouzwa katika soko la Geita ni kilo 1,570 ambayo yameingizia Serikali zaidi ya Sh bilioni 140.

Alisema pia mchango wa madini kwenye ukuaji wa uchumi umeongezeka na kufikia asilimia 5.1 mwaka 2018 na asilimia mpaka kufikia mwaka 2025, wanategemea sekta hiyo kuchangia asilimia 10 kwenye pato la taifa.

“Sote tuna wajibu wa kulinda madini, wakuu wa mikoa mzeanzisha masoko kwenye mikoa yenu na ngazi za wilaya, masomo haya yanahitaji ulinzi, yalindwe ili wananchi wasipate madhara wanapoenda kuuza madini yao, wale wachache wanaotorosha madini wajihadhari tutawashughulikia,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri Bitteko  alisema kwa sekta ya madini inaangaliwa kwa macho yote na Serikali kuanzia Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani, Waziri Mkuu na viongozi wengine wote.

Alisema kutokana na  kuisimamia vyema sekta hiyo, matunda yameanza kuonekana ambapo sasa wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Msumbuji, wameanza kuomba kuuza madini yao nchini.

Alisema hiyo, ni fursa na hawatawabana kuingiza madini yao hayo kutoka na hali hiyo, alisema ni vyema wafanyabiashara wa madini wakafuata sheria vinginevyo wataishia pabaya.

Alisema siku zote anataka kuwa waziri wa mfano katika kulea sekta hiyo, na ili afanikiwe katika hilo ni vyema wafanyabiashara wakafuata sheria ili wasimlazimishe kuwabana.

Alisema katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mchango kwenye uchumi wa taifa, mpaka sasa wametoa leseni mbili za usafishaji madini na nne za uyeyushaji.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alionya viongozi ambao wamekuwa wakitumia vibaya fedha za halmashauri na kusema wanaozidokoa wataumia.

“Wananchi mtuambie kama kuna sehemu kuna ulaji tutaingia, hata kama kuna ukuta sisi tutaingia,” alisema Majaliwa.

Alizitaka halmashauri nchini kutumia fedha wanazokusanya kuanzisha miradi mikubwa ikiwamo ya vituo vya mabasi na barabara badala ya kuzitumia kwa posho.

“Hizi fedha zinatoka kwa wananchi ni lazima ziwarudie kwa kutekeleza miradi mikubwa siyo kusubiri tu miradi ya Serikali kuu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here