30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

DPP aachia wafungwa gereza alilotembelea JPM

Benjamin Masese-MWANZA

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Butimba Mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, ametangaza kuwaachia huru wafungwa 325 na mahabusi katika magereza ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kati ya walioachiwa ni pamoja na askari wanane waliodaiwa kupanga njama za kutorosha dhahabu kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja mkoani Mwanza.

Mganga alitangaza jana uamuzi huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, , akiwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Agustino Mahiga.

Alisema katika gereza la Butimba amewaachia huru wafungwa na mahabusi 75,  Shinyanga  25, Kahama 43, Mugumu 52, Bunda 24, Bariadi 100 na Tarime 6  huku akiahidi leo atakuwa katika magereza ya Ukerewe na Sengerema. 

Alisema  walioachiwa alibainika kubambikiwa kesi, wagonjwa, umri na tuhuma zingine zenye harufu ya rushwa kuanzia kwa raia wenyewe kwa wenyewe, mpelelezi hadi kwa hakimu.

Mganga alisema hatua ya kuwaachia ilifikiwa baada ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wahusika.

Alisema waliokuwa watumishi wa umma wakiwamo askari polisi watarudishwa kazini isipokuwa kama kutakuwa na kesi nyingine ya msingi.

“Natoa onyo kwa umma, mamlaka na watumishi wa umma kufanya kazi kwa maadili, mtu atakayebainika kutoa taarifa za uongo na ikabainika hivyo naomba achukuliwe hatua kali ili kuthibiti hali ya kusingiziana.

“Huko magerezani tumeshuhudia watoto chini miaka 18, wazee zaidi ya miaka 79, wagonjwa, walemavu ambao baada ya kuwasikiliza nimeamua kuwaondolea mashtaka na wengine kuwafutia adhabu ya kifungo,”alisema Mganga

Kwa upande wake Waziri Dk. Mahiga, alisema katika ziara yake Kanda ya Ziwa ndani ya siku 10, kuwepo urasimu, kubambikiziwa kesi na kulazimishwa kukubali makosa.

 “Kilio kikubwa kwa wananchi ni kucheleweshwa kupata haki kutokana na upelelezi kutokamilika jambo linalosababisha magereza kujazana watu bila sababu, leo imekuwa bahati kwa gereza la Butimba maana tumekutana na Kamishna wa Magareza, DPP na mimi ndio, tumekaa wote na kuamua hivyo.

“Tumekubaliana kutembelea magereza yote nchini na kuwasikiliza wafungwa na mahabusi na kutoa msamaha, magereza yote nchini yameonekana kuzidiwa na yalijengwa miaka ya 1940 huku gereza jipya ni la mwaka 1972 na uwezo wake ni watu 200 lakini kwa sasa yanabeba watu zaidi ya 500,”alisema.

ZIARA YA JPM

Juzi wafungwa na mahabusi katika Gereza la Butimba, walimweleza Rais Dk. John Magufuli kero kubwa tano huku ya kubambikiwa kesi za mauaji ikiongoza.

Walitoa kilio hicho baada ya Rais Magufuli kutembelea gereza hilo na kuzungumza na wafungwa, mahabusu na askari magereza.

Kalikenya Nyamboge ambaye anatumikia kifungo cha miaka 30, alimtaja ofisa usalama aliyetambulika kwa jina moja la Mwasifika na kudai amekuwa akishirikiana na baadhi ya mahabusu na wafungwa kuingiza simu gerezani.

“Kuna watu umewapa madaraka wakusaidie kazi, lakini badala yake wanaleta vitu ambavyo havitakiwi, kuna ofisa usalama anawapa simu washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, matokeo yake simu zinakamatwa, tunanyang’anywa vitu.

“Huyu ofisa yupo mpaka leo, ondoka naye, tusaidie kwa hilo ili amani iwepo,” alisema Nyamboge.

Diwani mstaafu wa Kata ya Mbugani, Hashimu Kijuu, ambaye ni mahabusi katika gereza hilo, alisema watu wengi wamekuwa wakibambikiwa kesi za mauaji.

“Kuna kijana mmoja anaitwa Kulwa ana kundi la watu watano alibambikiwa kesi, yeye ni mfanyabiashara wa mafuta ya dizeli. Siku moja bajaji yake iliyokuwa imebeba lita 120 ilipofika njia panda iliharibika.

“Alipigiwa simu atafute bajaji nyingine, akatafuta toroli aje ahamishe mafuta, akapita OCCID mmoja wa Nyamagana alivyoona akawapigia maaskari waje wachukue yale mafuta.

“Yalibebwa mpaka kituoni halafu wakawa wanataka Sh milioni moja, akawaambia hana, mafuta yakataifishwa akapewa kesi ya mauaji,” alisema.

Kijuu kwa upande wake alisema aliuza shamba lake lililopo Kisesa, lakini aliishia kupewa kesi ya utakatishaji fedha.

“Askari Sangali aliniambia nitakaa jela mpaka nikute mke wangu kaolewa, maneno gani haya, uchungu umenipanda mno, nashindwa kusema. Shamba nililouza ni la kwangu, kwanini nipewe kesi ya utakatishaji,” alisema.

Shukrani Masegenya anayetumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, alimwomba Rais Magufuli kuwapunguzia vifungo.

“Pamoja na kufundishwa stadi za kazi, kuna wengine wamefungwa miaka 30 na wengine wamefungwa maisha, sasa utafundishwa stadi za kazi wakati maisha yako yote yataishia hapa gerezani?

“Tunaomba Rais utupunguzie vifungo ili hata tunapofanya kazi tujue tutakwenda kuwa kioo cha jamii tutakapokuwa nje,” alisema.

Askofu Edson Mwombeji, alimwomba Rais Magufuli aingilie kati vifungo vilivyotolewa na mahakama ili waweze kuchapa kazi.

Abdulrahman Ismail alisema alibambikiwa kesi ya mauaji na hadi sasa amekaa gerezani kwa miaka minane.

 “Askari wamekuwa wakikaa mahakamani na kusubiri watu walioachiwa kisha kuwakamata tena na kwenda kuwafungulia mashtaka mengine.

“Wanatengeneza namna ya kupata rushwa, juzi kuna mtu aliachiwa askari akawa anamvizia kwenye baraza amkamate, yule mtu akamchana kwa wembe,” alisema Ismail.

Mwita Mataluma anayetumikia kifungo cha maisha kwa kesi ya mauaji, alisema amekaa gerezani kwa miaka 40 na kumwomba Rais Magufuli ampunguzie adhabu.

“Rufaa yake ilishindikana kwa sababu aliambiwa jalada limepotea, tunakuomba katika watu unaowasamehe na huyu mzee umwangalie, tangu 1979 yupo gerezani,” alisema mmoja wa wafungwa kwa niaba ya mzee huyo.

Rais Magufuli alimtaka mzee huyo azungumze mwenyewe, lakini alionekana akishika kichwa huku akibubujikwa na machozi.

“Nilifungwa kwa kosa la mauaji kwa sababu nilimuua mke wangu kwa bahati mbaya, nimekaa gerezani miaka mingi, naomba msaada wako ikiwezekana niachiwe,” alisema.

Rais Magufuli alimuukuza; “ulimuulia wapi mke wako?” Akajibu; “Kinesi Mara.” Akamuuliza tena; “sasa ukiachiwa si utakwenda kuoa tena utamuua mwingine.” Akajibu; “siwezi kufanya lolote, tabia yangu ni nzuri, kama nitaachiwa nitakwenda kuishi vizuri.”

Mfungwa mwingine anayetumikia kifungo kwa makosa ya ubakaji, alisema hadi sasa amekaa gerezani kwa miaka 18, lakini alibambikiwa kesi kwa kuwa walikuwa wanagombea cheo cha Katibu wa Bakwata Mkoa wa Tabora.

“Kulikuwa na ugomvi, nilipewa cheo ambacho kilikuwa kinaviziwa na watu, nililetewa binti baadaye wakasema nimembaka,” alisema mfungwa huyo.

Clement Lugale, alisema ana kesi ya mauaji tangu mwaka 2014 haijaamuliwa na kumwomba Rais Magufuli amsaidie.

“Tulikuwa washtakiwa watatu na mshtakiwa wa tatu alikiri akafungwa mwaka 2014, tumebaki wawili mpaka leo maamuzi hakuna. Aliyekiri ameshamaliza kifungo na kuachiwa,” alisema Lugale.

Gideon Chacha, anayetumikia kifungo cha unyang’anyi wa kutumia nguvu, alisema alifungwa na Mahakama ya Mwanzo miaka 15, lakini aliwahi kuandika barua kumkataa hakimu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles