22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Adaiwa kumuua mkewe, kuteketeza mwili kwa moto

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

NI masikitiko. Ndivyo unaweza kusema baada ya Jeshi la Polisi, kueleza namna Hamisi Luwongo, ambaye anashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mkewe, Naomi Marijani, alivyofanya mauaji hayo na baadaye kuteketeza mwili wake kwa moto.

Inadaiwa Naomi  alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Mei mwaka huu, ambapo picha na taarifa zilizodaiwa kuandaliwa na mumewe Luwongo, zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai atakayefanikisha kupatikana kwake, atapa zawadi ya Sh milioni moja.

Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake, Kamanda Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Amon Kakwale,  alisema Mei 19, Luwongo alifika katika Kituo cha Polisi Gezaulole, Kigamboni na kufungua jalada la taarifa kuwa mkewe, Naomi ametoroka.

Kamanda Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Amon Kakwale

Alisema kama ilivyo taratibu za Polisi walianza uchunguzi ambapo Juni 12, Luwongo alifika tena kituo hicho cha polisi na kueleza kuwa Naomi ametelekeza mtoto anayeitwa Grecious mwenye umri wa miaka saba.

Kamanda huyo alisema baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa hizo, kesi hizo zilianza kufanyiwa kazi.

Alisema wakati wanaendelea na uchunguzi juu ya suala hilo, ndugu wa Naomi nao walifika katika kituo cha Polisi Chang’ombe, wakieleza kuwa ndugu yao alikuwa amepotea na wana shaka na mumewe kuhusu kutoweka kwake.

Alisema kutokana na maelezo hayo ya ndugu wa Naomi, Jeshi la Polisi likamtia mbaroni Luwongo kwa ajili ya mahojiano.

Kamanda Kakwale alisema Julai 15, akiwa mbele ya jeshi hilo akaeleza kuwa taarifa alizokuwa ameeleza awali hazikuwa za kweli na kwamba akaanza kueleza ukweli wa namna mkasa mzima ulivyokuwa.

Hamisi Luwongo

“Luwongo alilieleza Jeshi la Polisi kwamba walikuwa na ugomvi na mkewe ambapo siku hiyo asubuhi wakati Naomi anatoka kumpeleka mtoto shule, kukatokea ugomvi ambao ulisababisha umauti.

“Akaeleza kuwa baada ya kubaini kwamba amepoteza uhai alichukua mwili mpaka kwenye banda la kuku, ambapo aliweka magunia mawili ya mkaa na kuweka mafuta ya taa na kuwasha moto.

“Katika maelezo yake hayo, akaendelea kueleza kuwa baada ya kuhakikisha kwamba mwili wote umeungua moto akachukua mifupa na kuweka kwenye gari lake na kwenda nayo katika shamba lake huko Mkuranga mkoani Pwani.

Naomi Marijani, enzi za uhai wake

“Alipofika katika shamba lake hilo akachimba shimo na kufukia na akapanda mmea wa mgomba juu yake,”alisema Kamanda Kakwale

Aidha, kamanda huyo aliendelea kueleza kuwa baada ya taarifa hizo za Luwongo timu ya Jeshi la Polisi wakaongozananaye kwenda Mkuranga.

“Walipofika Mkuranga akaonyesha mahali ambapo amechimba shimo na timu hiyo ikabaini mabaki na mifupa na wakayachukua na tayari wamekabidhiwa kwa wenzetu wa kitengo cha sayansi kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha DNA,”alisema.

Alisema hatua inayofuata sasa ni kuhakikisha wanapata matokeo ya DNA ambapo itachukuliwa damu ya mtoto au ya ndugu wa Naomi ili waweze kuamini kuwa mabaki hayo ni ya marehemu.

“Baada ya matokeo hayo sasa jalada litaenda kwa AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) halafu yeye atalifikisha mahakamani na mtuhumiwa atajibu tuhuma hizo,”alisema.

Akizungumzia kuhusu chanzo cha ugomvi, Kamanda Kakwale, alisema ni wivu wa mapenzi ambapo kulikuwepo kutoaminiana baina ya wanandoa hao.

Aidha alitoa wito kwa Watanzania kuwa pale wanapopata taarifa kuwa mtu fulani amepotea wasiishie tu kusema kuwa ametekwa na watu wasiojulikana bali watoe fursa ya kujiridhisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles