24.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 7, 2022

DK. TIZEBA: MSIFANYE NANENANE YA MAZOEA

GRACE SHITUNDU Na DERICK MILTON – SIMIYU


WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, amewataka washiriki wa maonyesho ya 25 ya sherehe za wakulima ‘Nanenane’ kuyafanya kitofauti na miaka ya nyuma.

Dk. Tizeba alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua maonyesho hayo katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi.

Alisema maonyesho hayo yawe na majibu ya kutatua changamoto zinazokabili sekta ya kilimo, ambayo imesababisha kushindwa kuchangia asilimia kubwa ya pato la taifa.

Dk. Tizeba alisema Watanzania asilimia 65 hadi 70 wanajishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi, lakini wanachangia asilimia 30.1 tu ya pato la taifa wakati asilima 30 ya wengine katika sekta nyingine wanachangia asilimia 70.

“Hapo ndipo pa kujiuliza sababu na chanzo kinachosababisha asilimia hizo 70 za wakulima, wafugaji na wavuvi kufikisha asilimia angalau 70 sawa na sekta nyingine,” alisema Dk. Tizeba.

Alisema maonyesho ya Nanenane yaliwekwa kwa lengo la watu kujifunza na kufanya kilimo chenye tija, lakini yamekuwa yakifanywa kwa mazoea.

“Sasa tunataka maonyesho ya Nanenane kuanzia mwaka huu yawe ya kitofauti kwa watu kujifunza namna ya kufanya kilimo bora, ufugaji wa kisasa na uvuvi wenye tija,” alisema Dk. Tizeba.

Hata hivyo, Dk. Tizeba alisema sherehe za Nanenane hazitakuwa na tija endapo watumishi wa taasisi zenye mabanda hawatakuwa na utayari wa kutoa elimu ya kina kwa wananchi wanaowatembelea.

“Mfano katika Wizara ya Kilimo kuna banda la Wakala wa Hifadhi ya Taifa (NFRA) haitoshi tu kueleza kuwa ni kiasi gani wamehifadhi chakula, bali wawaeleze wananchi namna bora ya kuhifadhi mazao yao baada ya kuvuna.

“Leo wananchi wakivuna tani 100 za mazao, hupoteza tani 30 hadi 38 baada ya mavuno kutokana na uhifadhi, hivyo ni vyema wakaacha kusimulia na kuanza kuelimisha,” alisema.

Akizungumzia zao la pamba ambalo uzalishaji wake umeongezeka mwaka huu, Dk. Tizeba alisema Serikali itaendelea kusimamia umuhimu wa ushirika imara kwa faida ya wakulima wa zao hilo.

Alisema baadhi ya watu wanaleta dhana potofu kwamba ushirika unaua sekta binafsi, jambo ambalo si kweli.

“Ushirika ulikuwa umeoza kutokana na kuwapo mchwa ambao walikuwa wanakula na kuwafanya wakulima wasione faida yake, kwa kuzingatia hilo tumeshaanza kuwanyofoa mmoja mmoja ili kuweka uhai wa ushirika,” alisema.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, alisema uongozi wa mkoa huo na Kanda ya Ziwa Mashariki, umedhamiria kufanya maonyesho hayo kuwa hai kwa mwaka mzima.

Alisema lengo la kuomba kanda yao ni kuwasogezea utaalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi wananchi wa mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga, ambayo awali walikuwa wanafunga safari ndefu kuyafuata maonyesho hayo mkoani Mwanza.

“Hii ni miongoni mwa ahadi nilizotoa kwa rais wakati naapishwa, kwamba nitaubadilisha Mkoa wa Simiyu kuwa mkoa wa kiuchumi.

“Na ninaamini katika miaka ijayo, Nyakabindi itatajwa sio tu na vyombo vya ndani bali na vile vya kimataifa,” alisema Mtaka.

Maonyesho hayo ya Kanda ya Ziwa Mashariki yanaandaliwa kwa pamoja na mikoa mitatu ya Shinyanga, Mara na Simiyu, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika mkoani humo huku yakiwa na washiriki 220 kati ya 300 waliotarajiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,859FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles