20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

MBINU, NYENZO ZA MATAPELI DAR ZINATISHA

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM                 |            


MBINU na nyenzo zinazotumiwa na watekaji na wanaofanya vitendo vya kitapeli katika Jiji la Dar es Salaam zinaonekana kuvuka mipaka.

Hayo yamebainika wiki hii baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kuteka watu na kuomba kulipwa fedha kutoka kwa ndugu zao ili kuwaachia.

Watu hao kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa, walikamatwa Julai 26, maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakiwa na gari lenye namba T 452 CD 639.

Gari hilo namba zake ambazo kwa kawaida hutumiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), lilikamatwa likiwa na mateka watano ndani yake.

Waliokamatwa ni Hussein Shilingi (30), mkazi wa Kimara Mwisho na Martin Pumba (35), mkazi wa Tabata.

“Baada ya kufanya upekuzi ndani ya gari hilo, tulifanikiwa kukamata vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na wahalifu hao, ambavyo ni radio call moja, pingu jozi tatu, plate namba za magari za mashirika ya Serikali, namba za Umoja wa Mataifa na namba za watu binafsi.

“Pia walikuwa na kitambulisho cha kughushi chenye nembo ya polisi, chenye jina la Martin Pumba, simu za mikononi za aina mbalimbali, kadi za simu, panga moja, sime mbili, nondo moja, marungu matatu, visu vikubwa vinne, maganda matatu ya risasi yanayodhaniwa kuwa ni ya bunduki aina ya SMG, mkasi mkubwa mmoja na karatasi za maelezo ya watu mbalimbali waliowateka pamoja na hirizi mbili,” alisema Mambosasa.

Alisema baada ya kuwafanyia mahojiano, watu hao waliotekwa walieleza kuwa walitekwa kati ya Julai 23 na 25, mwaka huu na walitakiwa kutoa shilingi milioni sita.

Kwamba watekaji hao walikuwa wakiwapigia simu ndugu au jamaa zao kudai fedha hizo ili waweze kuwaachia huru.

“Jeshi la Polisi linaendelea na mahojiano na watuhumiwa ili kubaini watu wanaoshirikiana nao na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao,” alisema Mambosasa.

Wakati huo huo, Mambosasa alisema wamejipanga kuimarisha ulinzi wakati wote wa michezo ya majeshi ya polisi ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (EAPCCO), inayotarajiwa kuanza kesho.

Mambosasa alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha doria na misako katika maeneo mbalimbali ya jiji, hususan maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na maeneo yanayokizunguka, ambako wageni watafikia.

Aidha Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Dar es Salaam limekusanya zaidi ya Sh bilioni 2.5 kuanzia Julai Mosi hadi 31, mwaka huu, kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za barabarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles