23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN: WANAOTAKA UONGOZI KABLA YA WAKATI KUKIONA


Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR   |   

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amefanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na mabalozi wa Shina na matawi ya chake huko Unguja na Pemba.

Ziara hiyo iliyoanza Mei 2, mwaka huu na kumalizika jana, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kutowaunga mkono wale wote walioanza kutangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi katika majimbo kabla ya muda uliowekwa na chama hicho kufika na badala yake aliwataka waendelee kuyaimarisha mashina yao ili kuipa ushindi CCM.

Katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini Unguja, Dk Shein aliwaeleza mabalozi hao kuwa wapo baadhi ya wanachama wa chama hicho wameanzisha makundi ya watu wachache na kujipanga katika kutafuta nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kabla ya muda kufika.

Alisema baadhi yao wanavunjiana heshima na kukivunjia heshima chama chao na kusisitiza kuwa huo si mtindo mzuri na si utaratibu wa chama hicho.

Makamu Mwenyekiti huyo alionya wanachama hao kuacha tabia hiyo mara moja na iwapo wataendelea CCM haitosita kuwachukulia hatua kali za nidhamu kwani tayari imeshatoa maelekezo kwa viongozi wake wote wa ngazi za juu.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza mabalozi hao kutangaza mafanikio ya Serikali na chama chao yaliyofikiwa katika maeneo yao na kusisitiza haja ya viongozi hao kujitolea.

Alitumia fursa hiyo kueleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa Zanzibar na ambayo tayari imeanza kutekelezwa ukiwamo mradi wa Mji wa Fumba na kueleza nia ya Serikali kushirikiana na wawekezaji kujenga mji wa kisasa maeneo ya Chumbuni, Kwahani, Kisima Majongoo na sehemu nyingine.

Aliwapongeza viongozi wa CCM wa wilaya na mkoa kwa kufanikiwa kuvuna wanachama wapya 1457 na kueleza haja ya kuzisoma na kuzirejea ahadi zinazotolewa na wanachama wa chama hicho wakati wakila viapo vya kujiunga katika chama hicho ili waweze kukitumikia vyema chama chao.

Dk. Shein pia aliahidi ujenzi wa barabara ya Mboriborini kumalizika na kuwashukuru WanaCCM kwa kuwapigia kura nyingi viongozi wote wa chama hicho katika Mkutano Mkuu wa CCM uliopita.

Miongoni mwa wanachama wapya waliojiunga na CCM na kukabidhiwa kadi na Makamo Mwenyekiti huyo ni pamoja na aliyekuwa mgombea Ubunge wa Chama Cha CUF mwaka 2015 Jimbo la Gando, Salim Mussa Omar.

Kisiwani Pemba

Akiwa katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Mohamed JUMA Pindua iliyopo Mkanyageni, Wilya ya Kusini Pemba, Dk. Shein alisema kazi kubwa ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia Shina hadi Taifa ni kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi Mkuu na ule wa Serikali za Mitaa na hatimaye kukamata dola ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Aliwaambia mabalozi hao kuwa kuchaguliwa kwao ni kwa lengo la kukitumikia chama cha CCM ili kushinda uchaguzi na kuongoza dola kwani CCM ni chama kinachopendwa na wananchi wenyewe na chenye wafuasi wengi sana na hayo ni maelekezo ya Katiba ya CCM kuwa chama hicho ni lazima kishinde chaguzi zake zote.

Alisema kuwa CCM ni chama halisi cha Watanzania halisi na Wazanzibari halisi wanayoipenda nchi yao na hakina mbadala kwa Tanzania huku akisisitiza kuwa suala la ushindi katika uchaguzi ni lazima kwani ni maelekezo ya Katiba na Kanuni ya chama hicho na kuzingatia historia ya TANU na ASP.

Dk. Shein alieleza kuwa kuwa kazi kubwa ya viongozi wa CCM ni kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho huku mabalozi pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbali mbali ndio wenye jukumu la kuhakikisha Ilani hiyo inatekelezwa kwa vitendo.

Alieleza kuwa CCM ni chama chenye mtandao mkubwa sana wa utumishi na uongozi unaokwenda kwa kasi na kusisitiza haja ya kila kiongozi kutekeleza wajibu wake na kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alisisitiza haja ya kuwa makini na kutekeleza vyema majukumu yao na kukiimaraisha Chama Cha Mapinduzi na kutumia fursa hiyo kueleza wajibu wa mabalozi kwani ni watu wakubwa sana ndani ya chama hicho.

Aidha, alisisitiza haja ya kujengwa kwa majengo ya chama na kueleza umuhimu wa mashina na kusisitiza kuwa mabalozi ndio mhimili mkuu wa chama hicho kwani wao ndio wawakilishi wa CCM katika nyumba zao wanazoziongoza.

Alieleza kuwa hakuna mkataba kuliko hati za Muungano ambayo ndio makubaliano makubwa waliyosainiwa kati ya Marehemu Mzee Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere na kuwataka mabalozi yatakayowapotezea mwelekeo.

Dk. Shein alisema WanaCCM wapo macho na wapo tayari kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Pia aliwataka viongozi hao kutoogopa kuwataja watoaji na wapokeaji wa rushwa na wala wasinun’gunike pembeni kwani hata vitabu vyote vya dini vinakataza rushwa huku akiwataka mabalozi hao kushirikiana na viongozi wa CCM wa majimbo, wilaya na hatimaye viongozi wa ngazi za juu katika kuwataja watoaji na wapokeaji rushwa.

Akizungumzia maendeleo ya elimu, Dk. Shein alisema Serikali imetangaza kuwa elimu ya msingi kuwa ni bure na ifikapo Julai katika Bajeti ya 2018/2019, elimu ya Sekondari itakuwa bure, huku akisisitiza suala la pesa si tatizo na kuwataka wale wote watakaotoza pesa kuanzia muda uliowekwa Serikali itapambana nae.

Akizungumzia afya, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inao uwezo mkubwa wa kutekeleza huduma za afya bure kwa wananchi kwa kutekeleza azma ya Marehemu Mzee Karume.

Wilaya ya Micheweni

Akiwa katika Skuli ya Micheweni, Dk. Shein aliwahakikishia mabalozi wa Wilaya ya Micheweni kuwa CCM itashinda kwa kishindo katiks Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020 kwani hakuna mbadala wa CCM.

Alieleza kuwa CCM imefanya mambo mengi na uongozi wa CCM ndio ulioleta amani ya kudumu na wengine hawawezi kuleta amani hiyo kama ilivyoletwa na chama hicho kikubwa.

Alisema kuwa CCM lazima ishinde ili ipate kuendelea kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo alisema yamemnufaisha kila Mzanzibar na kuwataka kuanza kuandaa mazingira ya ushindi huo.

Akizungumzia udhalilishaji wa kijinsia, Dk. Shein alisema tayari sheria mpya ya udhalilishaji wa kijinsia ameisaini hivi karibuni ambayo itafanyiwa kazi na kuonya watakaopatikana na tuhuma hizo watahukumiwa kwa mujibu wa sheria hiyo ili kuifanya Zanzibar kuendelee kuwa na heshima yake kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Aliwahakikishia mabalozi hao kuwa changamoto ya huduma ya umeme katika Kijiji cha Kijangwani Micheweni itapatiwa ufumbuzi pamoja na kujengwa kwa bweni la skuli ya Chwaka Tumbe na ujenzi wa Barabara ya Micheweni-Kiuyu na Kiuyu- Maziwang’ombe pamoja na kuendelea kuwaajiri walimu.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi aliwapongeza mabalozi wa Wilaya ya Micheweni kwa uvumilivu mkubwa walionao hatua ambayo imewafanya kuendelea kupata mafanikio makubwa katika maeneo yao.

 

Akizungumza na mabalozi wa Wilaya ya Chake Chake katika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, Dk. Shein aliwataka kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM sambamba na kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta za maendeleo ikiwamo elimu, afya, miundombinu ya barabara, mawasiliano, maji na umeme.

Wete

Akiwa katika ukumbi wa Jamhuri, Dk. Shein aliwaeleza mabalozi kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika kutokana na uongozi thabiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuonya hatokuwa na msamaha kwa yeyote atakaebainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Dk. Shein alisema kuwa uchumi wa Zanzibar umezidi kuimarika kwa kiasi kikubwa na kutumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza kauli yake aliyoitoa katika maadhimisho ya kilele cha Mei Mosi mwaka huu kwa wale wote wanaodiriki kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Alisema kutoka na uwezo huo wa fedha, Serikali yake imeweza kuongeza mishahara mara nne katika uongozi wake sambamba na kuimarika kwa sekta za maendeleo.

Dk. Shein aliendelea kusisitiza kauli yake kuwa ataendelea kuiongoza Zanzibar kwa uadilifu mkubwa.

Unguja

Akiwa katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kilichopo Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja,, Dk. Shein alisema Serikali yake barabara ya kisasa katika eneo la Mwanakwerekwe na daraja la kisasa katika eneo la Kibondemzungu.

Alisema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi huo katika maeneo hayo ambayo hayapitiki wakati wa mvua kubwa na kuleta usumbufu kwa wananchi hasa wa Mkoa wa Kusini na wale wa Wilaya ya Magharibi.

Dk. Shein alisema kuwa ujezi huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu na tayari fedha zimetengwa katika Bajeti ya 2018/2019 kwa ajili ya ili ujenzi huo ili uanze mara moja.

Aliongeza kuwa tayari wataalamu wako katika mchakato wa kuangalia namna ya ujenzi utakavyotekelezwa katika maeneo yote hayo mawili ambayo yamekuwa yakileta usumbufu mkubwa kwa wananchi katika kipindicha mvua hasa za Masika.

Dk. Shein alisisitiza kuwa kuwa kuanzia Bajeti ya 2018/2019 hakuna mzazi atakayetozwa ada ya mtoto wanaosoma Skuli ya Sekondari na Msingi na Serikali imeamua kwa makusudi kutekeleza azma ya Marehemu Mzee Abeid Karume ya Elimu Bure.

Akiwaeleza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Dk. Shein, aliwaeleza viongozi hao kuendelea kusimamia amani na kuongeza kasi katika suala hilo kwani CCM ndio inayosimamia amani, utulivu na mshikamano.

Alisema kuwa ndani ya CCM kuna kundi moja tu na kuwataka mabalozi kuendelea kuwafahamisha wana CCM na kuwataka kutoruhusu wale wanaoingia ndani ya chama hicho kutaka uongozi na baadaye kutowatendea majukumu yao wananchi waliowachagua.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles