Na Mwandishi Wetu, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi wasiwe chanzo cha kuvurugika kwa amani nchini kwa kisingizio cha harakati za kidini na kisiasa.
Hayo aliyasema jana katika hotuba yake kwenye Baraza la Idd el Hajj, lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Kiislamu Kiuyu, Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Idd.
Alisema Tanzania imefikia kuwa nchi ya amani kutokana na misingi ya uongozi bora iliyowekwa na viongozi wa awamu zote zilizopita na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kufurahia baraka zilizopo nchini kwa kufanya jitihada ili kuilinda neema iliyopo.
“Wale wote wanaofanya hivyo, watambue kuwa wanafanya makosa kwa kufikiri kwamba wana uwezo zaidi kuliko wengine wa kuondosha matatizo katika jamii kwa kutumia nguvu zao..ni vyema tukaelimishana juu ya mema na mabaya kwa busara, badala ya kiburi na dharau,” alisema Dk. Shein.
Rais huyo wa Zanzibar, aliwataka wananchi kutosahau kwamba amani na umoja ni misingi ya uhai wa nchi hii na kuwataka waumini na wananchi kwa jumla kuepuka kushabikia mambo yanayokwenda kinyume na maadili.
Alisema Serikali zote mbili zitasimamia hali ya amani na utulivu kwa uwezo wake wote kwa kutambua kwamba hakuna mbadala katika suala la amani.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kutambua kwamba wanajukumu la kupambana na maovu mbalimbali yakiwemo ujambazi, ubakaji, udhalilishaji wa wanawake na watoto, ajali za barabarani, ulevi, rushwa, dhuluma, uhasama na chuki zisizokuwa na msingi na nyinginezo.