25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta shujaa au msaliti?

Samuel Sitta
Samuel Sitta

Na Waandishi Wetu

HATUA ya Bunge Maalumu la Katiba kuhitimisha kazi yake kwa kupitisha Katiba inayopendekezwa, imemjengea taswira mbili tofauti Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.

Wakati wengine wakitafsiri matokeo ya kupata theluthi mbili kila upande ili kupitisha Katiba inayopendekezwa kuwa yamembebesha Sitta taswira ya mtu shupavu na shujaa, upande unaompinga unamuona msaliti na kiongozi anayeweza kusababisha kuibuka na kukua kwa ufa mkubwa miongoni mwa jamii.

Hatua yake ya kuliongoza Bunge hilo hadi kuhitimisha kazi yake juzi licha ya upinzani mkali kutoka katika makundi kadhaa ya wananchi, imeonekana kugusa hisia za wachambuzi wa masuala ya kisiasa, viongozi, wasomi wanaoheshimika na watu wa kada mbalimbali.

Pamoja na hayo, imeibuka hofu juu ya mazingira ya kura mbili zilizofanikisha kupatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Zanzibar.

Wenye hofu hiyo wanakumbukumbu na kauli iliyopata kutolewa na Sitta mwenyewe akisisitiza juu ya uwezekano wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa kile alichokieleza juu ya uwepo wa kura mbili alizokuwa akizitegemea kutoka kwa wajumbe wa Ukawa waliomueleza kuwa wako tayari kwenda kupiga kura pindi muda wa kufanya hivyo utakapowadia.

Pia watu wenye mtazamo kama huo wanayazungumzia matukio yasiyo ya kawaida ya kubadili kanuni kuwawezesha baadhi ya wajumbe kupiga kura kupitia email, fax na mitandao mingine kwamba zote hizo huenda zilikuwa njama za kupata kura mbili zilizofanikisha zoezi hilo.

Profesa Kitila Mkumbo ni miongoni mwa wachambuzi maarufu wa siasa nchini, anasema ni lazima Sitta aonekane shujaa kwa sababu amekamilisha jukumu alilopewa.

Profesa Kitila alikwenda mbali na kusema Sitta hastahili kulaumiwa kwa kukosekana maridhiano ya kisiasa, kwa sababu wenye dhamana ya kutafuta maridhiano hayo ni vyama vya siasa na si yeye.

“Ni lazima aonekane shujaa kwa wale waliolazimisha ushindi, ameliongoza Bunge hilo kwa mujibu wa sheria hadi tamati yake, licha ya mivutano na mipasuko iliyojitokeza, kwanini asiitwe shujaa kwa wale waliozalisha Katiba inayopendekezwa,” alihoji Profesa Kitila.

Hata hivyo, aligusia mustakabali wa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu kwa kusema utategemea busara ya rais ajae, kwamba itambidi atafute maridhiano na vyama vya siasa kabla ya kuruhusu kura ya maoni, tofauti na hapo Katiba Mpya itasababisha mivutano mikubwa kwa wananchi kama iliyoshuhudiwa.

Hata hivyo, katika jicho jingine alisema licha ya Katiba inayopendekezwa na Bunge kupita, lakini bado mchakato ni mgumu huku akisema kuwa kilichofanyika ni kwa wale waliopenda Katiba iwe hivyo, kwamba kuna kundi lililosusia mchakato pia jamii nayo ina sehemu yake ya uamuzi.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honest Ngowi, alisema Katiba ni kitu kitakatifu akimaanisha kuwa pamoja na kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa na Bunge, lakini bado kunahitajika mchakato usioacha shaka.

“Tumeambiwa Katiba imepatikana sawa lakini imepatikana bila kuwepo kwa maelewano, ieleweke kuwa Katiba ni kitu nyeti hivyo unahitajika umakini wa hali ya juu katika maridhiano, lakini kilichofanyika sasa ni kama kuburuzana, kwa mtindo huu hiyo Katiba iliyopatikana itakosa Legitimacy (uhalali) kwahiyo itakuwa Katiba lakini siyo Katiba bora,” alisema Dk. Ngowi.

Dk. Ngowi alisema kutokana na utakatifu wa Katiba, ilipaswa kuwepo kwa maridhiano kwa ajili ya kuondoa vinyongo vya watu wenye mitazamo tofauti.

“Wahusika walipaswa kukaa na kuridhiana na wenzao lakini si kufanya bora lipite, kwasababu tunaambiwa kura zilizofanya mabadiliko ni kura mbili, huku kuna wengine wanatilia shaka upigaji kura, sasa mambo haya kwa busara hutakiwi kuyaacha hivi hivi wananchi hawataelewa.

“Ni vyema wakatambua kuwa hii Katiba tunataka kuishi nayo ikiwezekana miaka 50 ijayo au 100, kwahiyo mchakato wake ulitakiwa usiache shaka kabisa lakini hadi sasa hivi tunaona namna ambavyo umeacha shaka,” alisema Dk. Ngowi.

Wakati baadhi wakiwa na mtazamo huo, upande unaomuunga mkono Sitta kwa dhana ya ushujaa na hasa upande wa chama chake, umeamua kumuandalia mapokezi makubwa ya kumpongeza.

MTANZANIA limedokezwa kuwa huko mkoani kwake Tabora kumekuwa na maandalizi ya kumpokea kishujaa baada ya kufanikisha kazi aliyopewa na kuleta Katiba inayopendekezwa na Bunge.

“Yameandaliwa malori ya kwenda kuchukua watu kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Sitta,” kilisema chanzo chetu hicho kutoka mkoani Tabora.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Urambo, Martha Susu, ambaye alithibitisha kuwapo kwa maandalizi hayo.

“Tunataraji kumpokea Sitta Oktoba 10, katika Kijiji cha Itundu nje kidogo ya mji na kisha kuandamana mpaka Urambo mjini, hivi ninavyokwambia tupo kwenye maandalizi makubwa ya kufanikisha shughuli hiyo,” alisema Susu.

Wakati kukiwa na maandalizi hayo, wazee wa Jimbo la Urambo Mashariki ambako ndiko alikopewa dhamana ya ubunge wiki hii waliibuka na kauli ya kumtenga Sitta.

Mmoja wa wazee hao, Ibrahim Mpazi alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa wazee wa jimbo la Urambo Mashariki hawana imani tena na Sitta kutokana na tabia zake za kuendesha siasa kwa fitina na kugombanisha wananchi.

“Msimuone hivyo Sitta akiunguruma na uwaziri, uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba au Uspika, jimboni kwake kumemshinda amekuwa ni kiongozi wa kuishi Dodoma na Dar es Salaam, tangu 2010 amefanya mikutano miwili tu ya hadhara, hana cha kujitetea, Urambo Mashariki haina maendeleo kuanzia maji hata miundombinu…sasa tumemchoka na sisi wazee tumeamua kutangaza rasmi leo kumtenga,” alisema.

Siku moja baada ya Katiba inayopendekezwa kupitishwa, mjumbe wa Ukawa, Ismail Jussa aliandika ujumbe katika mtandao wa Facebook uliosomeka:

“Nimefurahi sana na yaliyojiri Dodoma asubuhi hii. Nawashukuru kwa kuturahisishia kazi…Niliwahi kuandika “Naiona ileee!”

“Wengi hawakunifahamu. Sasa leo naiona Zanzibar yenye Mamlaka Kamili kama alivyoizungumza Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, imesogezwa karibu na inakaribia kuegesha bandarini.

“Wazanzibari wenzangu, sisi tuna viongozi makini na imara wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad. Watatupa mwelekeo ambao nakuhakikishieni utatufikisha tunakokutaka Inshallah”.

Kisha akamalizia na neno Wallahi raha sanaaaa…….!

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe naye aliandika ujumbe kama huo kwenye mtandao wa Facebook akisema: “Afadhali igizo la BMK limekwisha na sasa watu watajielekeza kwenye ufisadi unaolitafuna Taifa, mfano ‪#‎TegetaEscrow‬ ‪#‎IPTL‬”.

Ni pamoja na hayo, Sitta ambaye kwa muda mrefu amekuwa kiongozi kipenzi kwa wale wanaompinga sasa kutokana na jinsi alivyofanikiwa kuliongoza Bunge la tisa kwa kaulimbiu ya kasi na viwango, hata hivyo katika siku za hivi karibuni taswira yake imeonekana kubadilika na kuchukua mwelekeo wa lawama zaidi kuliko sifa.

- Advertisement -

Related Articles

6 COMMENTS

  1. Korongo kati ya wananchi, lililosababishwa na kuchanwa moyo wa rasimu ya pili ya Tume ya Warioba ni eneo la kulelea uhasama baina yao. Busara kubwa inahitajika kuliziba ili kuzuia u-interahamwe miongoni mwa watanzania. Ukitokea, CCM haiwezi kukwepa lawama.

  2. Sitta ni msaliti siyo shujaa. Shujaa ana sifa ya kuunganisha watu siyo kuwagawa kwa misingi ya kisiasa. Ametugawa watanzania kwa kuleta katiba yenye maslahi ya CCM. Kazi yake imewadhalilisha Wajumbe wa Kamati ya Warioba waliokutana na wananchi na kuchukua maoni yao. Pia amemdhalilisha Rais Kikwete maana imeonekana wazi aliteua watu ambao si weledi katika kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi.YETU MACHO.

  3. Ni afadhali waliotoka walifanya jambo la maana kuliko waliobaki wakijidai kuwa watapambana na majangili yaliyochakachua rasimu.Viongozi wa dini wakiyasifia yanafurahi na wakiyakosoa yanawaita wapuuzi. Mi nayafananisha na mfalme Nebkadneza

  4. sitta, nikisikia jina hili nasikia kichefu. Shujaa ni warioba na tume yake. BMK watajuta si muda mrefu na watajificha kwa maamuzi yao ya kijinga. Watanzania watafanya maamuzi magumu na CCM waache kukalili mambo ya kisiasa.

  5. Sitta anafahamika kwa visa, anaependa hata sifa hana, anabifu na mh warioba sasa amefanya kweli sasa ametufanya sisikuwa kafara kwa mika 50 ijayo lakini kwa taarifa yake “mchuma janaga ula na wakwao” wazee wa tabora hawamtaki kabisa,wananchi wengi hasa wa vyama vya upinzani wasomi, wanazuoni,watu mshuhuri na maasikofu pia majuzi anamtukana mke wake bila sababu anamlazimisha kupiga kura ya ndiyo na akipiga kinyume “ungekiona” alikaririwa sitta akisema aliingia kwenye bunge km mke au mjumbe halali.kwa kifupi sitta amefanikiwa kuwagawa wananchi wa bara na visiwani lakini zaidi ccm mwaka ujao sijui watapata wabunge wapi?sababu wapinzani wamepewa ujiko kwa kuondoa maoni ya wananchi bila ridhaa yao.waliyoyaweka na kubeza ya tume ya warioba eti imesahau mambo ya msingi lakini hayo waliyoyaongeza yaliwekwa kando ili yawekwe kwenye katiba za washiriki wa muungano, sitta kwa unafiki tuu

  6. Shujaa kwa waliomtuma na chama chake. Lakini chama chake hicho hicho kitamwonyesha mlango wa kutokea, amesahau walivyomfanyia kwenye uspika miaka michache iliyo pita

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles