Na Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ameibuka na kusema kwamba atazungumza baada ya kuisoma Katiba hiyo iliyopendekezwa.
Juzi baada ya Bunge hilo kupitisha Katiba inayopendekezwa, wananchi wa kada mbalimbali, viongozi wa kisiasa, dini, wasomi na baadhi ya taasisi walionyesha wazi kutofautiana, wengine wakihofia namna ilivyopatikana theluthi mbili ya kura za wajumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kupitia simu yake ya kiganjani kuhusiana na hatua hiyo ya Bunge Maalumu la Katiba, Jaji Warioba alisema kwa sasa anatafuta Katiba hiyo inayopendekezwa kwenye tovuti aisome na kisha baadaye atazungumza.
“Bila shaka umenipigia unataka maoni yangu kuhusiana na rasimu inayopendekezwa, lakini kwa sasa sina ‘comment’ yoyote…natafuta rasimu kwenye website halafu nisome na nijifunze nini kimetokea na baadaye ndio nitazungumza,” alisema Jaji Warioba kwa ufupi.
Jaji Warioba ambaye amekuwa hafurahishwi na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba kutokana na kitendo chake cha kubadili maudhui ya rasimu yaliyokuwa yakipendekezwa na tume yake, mara nyingi amejikuta katika vita kubwa ya maneno na upande unaompinga hasa Chama Cha Mapinduzi.
Ni katika vita hiyo wiki iliyopita alitumia maadhimisho ya miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) yaliyokwenda sambamba na kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Dk. Sengondo Mvungi, kujibu mapigo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba wa Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge kuwasilisha Katiba inayopendekezwa.
Katika hilo, Jaji Warioba alisema kuwa watakutana mtaani na wajumbe wa Bunge hilo, kutetea maoni ya Watanzania kwa kuwa mengi yameondolewa.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku, alisema hana maoni yoyote juu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge hilo.
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Butiku alisema kuwa Watanzania ndio wenye dhamana ya kupigia kura kile wanachokitambua kama maoni yao.
“Sina maoni yoyote kuhusu Katiba yao, huu si mchakato tu mwanangu? Tulianza sisi kwa kukusanya maoni, wao wamekuja na Katiba, ni vyema sasa wananchi wakaisoma na kufuatilia kila hatua na ukifika wakati wa kupiga kura ya maoni watatathimini maoni waliyoyatoa na Katiba inayopendekezwa. Binafsi hata mimi nasoma na muda ukifika tutatoa tamko,” alisema Butiku.
Kwa upande wao Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) tangu juzi wamekuwa na vikao vya muda mrefu vya kutathimini kile kilichofikiwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
MTANZANIA Jumamosi limedokezwa kuwa vikao hivyo vya siri ambavyo viliendelea hadi jana vimefanyika katika ofisi ya Chama cha NCCR-Mageuzi vikiongozwa na kamati ya ufundi ya umoja huo ambapo inaelezwa kuwa viongozi hao watatoa tamko rasmi leo.
Akithibitisha hilo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema kuwa viongozi wa chama chao walikuwa wakiendelea na vikao vya mashauriano ili kuweza kutoa tamko la pamoja na wenzao wa Ukawa.
“Viongozi wa Chadema wanaendelea na mashauriano na wenzao katika UKAWA, kupitia vikao vya ndani/mashauriano kwenye ngazi mbalimbali kama ambavyo umma wa Watanzania ulitaarifiwa kupitia kwa vyombo vya habari juzi kuwa vikao vya Kamati ya Ufundi na Viongozi Wakuu vinafanyika baada ya hapo ndiyo itatoa kauli rasmi,” alisema Makene.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lmetumia njia za kiharamia kupata 2/3 haramu kupitisha Katiba isiyotokana na maoni ya wananchi inayosimama katika misingi ya maridhiano na mwafaka wa kitaifa.
Aprili 16 mwaka huu, Ukawa walisusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba wakidai kuwa hawawezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.
Walidai kuwa vikao hivyo vilikuwa vinaendeshwa kwa upendeleo huku maoni ya wananchi kupitia rasimu ya Jaji Warioba yakichakachuliwa.
Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Evans Magege na Elizabeth Mjatta
Ni hatari sana endapo wajumbe 400 wanabeba uhalali wa watanzania wote kwa kuamini mawazo yao ni sahihi kuwa ktk katiba badala ya maoni yaliyotolewa na watanzania! Kama ndivyo ilivyo, kulikuwa na sababu gani ya kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni ya watu?
Huu ni udhalilishaji wa wazi!CCM kama walijua wao ndo wenye maoni sahihi ya kuingia kwenye katiba wangeitisha NEC yao, waandike katiba.
Siyo kutudanganya kuwa ni maoni ya wananchi huku wakibeza kazi iliyofanywa na Jaji mstaafu waryoba.Anatukanwa na kudhalilishwa kwa kuwa aliandika maoni ya watanzania!
Katiba ni maridhiano, bila maridhiano katiba hiyo itabeba taswira ya CCM, ikumbukwe kwamba, ipo siku CCM haitakuwa madarakani, hayo maslahi yenu yatalindwa na nani?
Nchini Kenya kulikuwapo chama cha KANU, sasa KANU si kitu tena! Haingii akilini wazee wasomi, na wenye uzoefu, kukosa maono na dira ya taifa ya miaka zaidi kumi ijayo!
Kiongozi anapokosa Maono na Dira hana budi kujitoa kwenye uongozi,ili apate wasaa wa kulea wajukuu, kuliko kupotosha umma kwa visingizio visivyo na mashiko!
Yaliyotendeka Dodoma, dhahiri ni ubabe wa watawala kulazimisha matakwa yao, badala ya kuheshimu uhuru wa maoni na matakwa ya watanzania kwa ujumla wao. Penye nia pana njia na penye ukweli uongo hujitenga! Ipo siku ukweli mambo utajulikana!Muda ukitimia nina uhakika ubabe utakosa nafasi, hapo nyie wababe mtashuhudia, wakati ulivyo mbaya kwa wale waliotumia muda wao wa uongozi kukandamiza wanyonge, kwa nia ya kulinda maslahi ya wachache, walioko madarakani! Malipo ya awali ni hapahapa duniani! Baadaye kila mmoja wetu awajibika kwa matendo yake, mbele za Mungu! Hapo hakuna cha ukubwa wala Utajiri wa mtu!
Mimi naamini UTANZANIA wetu ni bora kuliko Chama cha Siasa!
Watanzania tunataka ufafanuzi wa mgongano huu wa maneno ya vigogo wamiliki wa mchakato wa katiba! Kati ya Sitta anayejigamba ametengeneza katiba nzuri, Kinana anayesema watanzania hawahitaji katiba mpya, wao wanahitaji maji, barabara n.k na Nape ambaye anajinasibu kwamba, katiba mpya siyo kipaumbele cha CCM!? Nani yuko sahihi? Kama Katiba,siyo kipaumbele cha CCM, kwanini mmevuruga maoni ya watanzania yaliyokusanywa na Mh. WAryoba???????
Ni masikitiko makubwa kama ile CCM, iliyo kuwa inakubalika na wananchi enzi za mwalimu imekuwa ina wadharau na kutumia uharamia na wizi wa hali ya juu kuzika maoni na matakwa ya wananchi na kujikita na ya kwao yanayo linda ufisadi wao. shime tuwakatae wao pamoja na rasimu yao.