22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango atoa motisha ya Sh milioni 50 Sekondari ya Tumbi

Na Gustafu Haule, Pwani

MAKAMU wa Rais Dk. Philipo Mpango amemzawadia Sh milioni 50 Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tumbi iliyoko Kibaha Mjini mkoani Pwani baada ya kufurahishwa na matokeo ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha Nne.

Dk. Mpango ametoa fedha hizo ikiwa ni sehemu ya kutoa motisha kwa walimu 50 wa Shule hiyo kutokana na kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha wanafunzi wao wanafaulu kwa kiwango cha juu.

Hatua ya Makamu wa Rais ya kuwapa motisha walimu hao ilikuja baada ya Mkuu wa Shule hiyo, Haule kusoma taarifa ya matokeo ya ufaulu ya ya wanafunzi hao ya mwaka 2022 ambapo daraja la kwanza waliofaulu ni 40, daraja la pili (46), daraja la tatu(31), daraja la nne(36) na waliopata 0(3).

Dk. Mpango alitoa motisha hiyo katika siku ya maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ambapo kabla ya maadhimisho hayo alifanya ziara shuleni hapo na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuzindua mpango wa upandaji miti shuleni hapo.

“Nimefurahishwa sana na matokeo haya ya kidato cha nne binafsi nimpe pongezi kubwa Mkuu huyu wa Shule ndugu Haule na kwakusema hivyo nitatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya motisha kwa walimu 50 wa Shule hii,”amesema Dk. Mpango.

Amesema shule zinazofanya vizuri kama hiyo zinapaswa kuangaliwa zaidi na kwamba Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ili kusudi Taifa liwe na wasomi wengi ambao wataisaidia nchi yao hapo baadae.

Kwa upande wake, Haule amemshukuru makamu wa rais kwa hatua kubwa ya kutoa motisha hiyo kwa walimu wake huku akiahidi kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2023.

“Namshukuru sana Makamu wa Rais kwa kutuona na kutuzawadia motisha hii kubwa, mimi nasema kwa sasa tunajipanga na walimu wangu ili tufanye vizuri zaidi na ikiwezekana mwakani tupate daraja la kwanza 70 na kusiwepo na daraja la 0,”amesema Haule na kuongeza kuwa:

Tayari wamezindua mpango maalum na mkakati wa shule ambapo lengo lake ni kuhakikisha ufaulu unaishia daraja la pili ili kusudi kuendelea kumtia moyo makamu wa rais na hata kama akifanya ziara shuleni hapo akute motisha yake kwa walimu imefanyakazi vizuri.

Aidha, Haule ameipongeza serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisaidia shule hiyo kwani wamepokea kiasi cha  Sh milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

Amesema fedha hizo zinatumika katika ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara, madarasa 16, vyoo, barabara, miundombinu ya maji na mahitaji mengine ya shule ambapo mpaka sasa ujenzi wake unaendelea vizuri.

“Nitumie fursa hii kuipongeza serikali yetu chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake akiwemo Makamu wa Rais kwa kuendelea kupambana dhidi ya changamoto ya elimu na sisi hapa kwetu tumeletewa Sh milioni 200 ambazo zinafanya kazi vizuri ya kuboresha S=shule yetu,”alisema Haule

Zephania Malindila na Rose Edwin ni kati ya walimu wa shule hiyo ambapo wamesema kuwa wanamshukuru makamu wa rais kwa motisha aliyoitoa nakwamba watafanyakazi kwa bidii ili kuongeza kiwango cha ufaulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles